Miaka mitatu Diamond akiwa 'single'

HATIMAYE staa wa Bongofleva toka WCB Wasafi, Diamond Platnumz ametimiza miaka mitatu bila kutangaza rasmi uhusiano wake mpya kwa umma tangu kuachana na mrembo kutokea nchini Kenya, Tanasha Donna.
Kulingana na historia ya msanii huyo huko nyuma, hii ni mara ya kwanza kufanya hivyo jambo linalozipa nguvu tetesi kuwa yupo na Zuchu ila mwenyewe alishasema huyo ni msanii wake tu na sio vinginevyo!
Imezoeleka Diamond anapokuwa na baby mpya siyo mtu wa kujificha sana, kumbuka alivyokuwa na Wema Sepetu, Penny, Zari The Bosslady hadi Tanasha Donna, kila mtu alijua na walionekana pamoja sehemu mbalimbali kama wapenzi.
Zimepita zile nyakati ungemuona akiwa visiwani Zanzibar na Zari wakipunga upepo, zile nyakati za kumzawadia Wema Sepetu gari kwa ajili birthday tu, zile nyakati za kujiachia kwenye Yacht ufukweni na Tanasha.
Ni kweli mambo yamebadilika sana kwa Diamond, tangu Machi 2020 alipoachana rasmi na Tanasha ambaye wamejaliwa kupata mtoto mmoja, Naseeb Junior, Simba ameshusha mapanga chini, amekuwa mtulivu sana!
Utakumbuka tetesi za Diamond kuachana na Tanasha zilianza Februari 2020 mara baada ya ‘kususia’ uzinduzi wa EP ya Tanasha, DonnaTella EP uliofanyika katika Ukumbi wa Sarit Centre Expo, Nairobi, Kenya. Diamond na Tanasha walianza kuwa pamoja Desemba 2018, Tanasha bado alikuwa ni Mtangazaji wa Kituo cha Redio, NRG, Kenya, karibia kila wikiendi Tanasha angeonekana uwanja wa ndege Dar es Salaam, lengo la safari yake ni kumuona Diamond.
Uhusiano huo ulichipuka takribani miezi 10 tangu Diamond kuachana na Zari The Bosslady hapo Februari 2018 wakiwa wamejaliwa watoto wawili, Tiffah na Nillan ambao sasa wanaishi Afrika Kusini na mama yao.
Ikumbukwe Zari ndiye aliyetangaza kuachana Diamond kwa madai ya kuchoshwa na habari za usaliti hasa kitendo cha Diamond kuzaa nje ya uhusiano wao na kuvunjiwa utu wake kwenye mitandao ya kijamii.
Hivyo ulikuwa ni muda mfupi tu kwa Diamond kufunga ukurasa wa Zari na kuufungua wa Tanasha, miezi 10, lakini imekuwa ni muda mrefu sasa tangu kuufunga ukurasa wa Tanasha, miaka mitatu bila kuufungua mwingine!
Kuna tetesi huenda wawili hao wakaja kurudiana maana Tanasha naye hajaweka wazi uhusiano wake tangu kuachana kwao, wikiendi iliyopita Diamond alionekana akiwa na mtoto wake na Tanasha na hiyo sio mara ya kwanza mrembo huyo kumleta nchini Naseeb Jr kumuona baba yake.
Hata kipindi Diamond anaachana na Wema Sepetu ilichukua kipindi kifupi sana kuhamishia moyo wake kwa Zari, hivyo hivyo alivyoachana na Wema haikupita miezi akahamishia moyo wake kwa Penny ila sasa Diamond kabadili mtindo wa maisha.
Ukimya huo ndio unasababisha kutajwa kwamba anatoka na Zuchu ila ukitazama mambo yao huwezi kulinganisha hata kidogo na ilivyokuwa kwa kina Zari, Penny, Wema na Tanasha.
Ni kama tunalazimishwa kuamini hivyo.
Hata hivyo, kumekuwa na hoja kuwa Diamond ameamua kuweka usiri uhusiano wake ili kutoa nafasi kwa Zuchu kukua kimuziki, tangu amsaini Zuchu WCB Wasafi, Aprili 2020 hajawahi kuweka wazi yupo na mrembo yupi hasa.
Pengine anajua kufanya hivyo kutapelekea mashabiki wapunguze kumzingatia Zuchu tofauti na sasa ambavyo wengi wanaamini Zuchu ndiye mtu wake, hilo linafanya jina la Zuchu kukua hata nje ya muziki.
Lakini Diamond akizungumza na kipindi cha The Switch cha Wasafi FM hapo Januari 2023 alisema ana uhusiano na mrembo ambaye alianza kumfuatilia tangu mwaka 2013. Hivyo ni vigumu kusema ni Zuchu aliyekuwa anafuatilia tangu wakati maana alikuwa bado mwanafunzi.
“Ni mzuri sana, yaani sana, sana, nikikwambia tena sana, anajua kuishi na familia, ni mtu hana makuu, ni mkali sana. Nilianza kumtongoza 2013 akanikubalia mwaka jana, kanizungusha nafikiri, kanikubali mwaka jana (2020).” alisema Diamond.
Kauli hiyo Diamond ikaibua tetesi kuwa anayemngumzia ni mrembo kutokea nchini Afrika Kusini, Andrea Abrahams ambaye amewahi kuwa Miss Mamelodi Sundowns Mpumalanga na Miss 7 Continents 2016. Hata hivyo, hilo linaonekana kutokuwa kweli na sasa imetimia miaka mitatu Diamond akiwa single kimtindo!