Miaka 18 ya 2Pac udongoni

2pac Amaru Shakur
Muktasari:
Sababu za mshituko huo zilichangiwa na kuondoka kwa nyota changa, kutengeneza heshima ya soko la muziki huo nchi za Magharibi na duniani pamoja na uwezo wake mkubwa.
NI kama mbalamwezi iliyoibuka na kuzimika ghafla katika uso wa dunia ndani ya kipindi cha miaka 25 tu. Wengi hawakuamini na ilisababisha mshituko wa dunia hususan kwa mashabiki wa Hip Hop.
Sababu za mshituko huo zilichangiwa na kuondoka kwa nyota changa, kutengeneza heshima ya soko la muziki huo nchi za Magharibi na duniani pamoja na uwezo wake mkubwa.
Hapa namzungumzia 2pac Amaru Shakur, ambaye ni mwasisi na msanii aliyetia chachu kubwa ya kukubalika kwa soko la Muziki wa Hip Hop nchini Marekani na duniani kote.
Leo Jumamosi anatimiza miaka 18 tangu alipofariki dunia huku utata wa hali ya juu uliobatizwa jina la Mkasa wa Las Vegas, ukijenga maswali mengi huku uzushi wa habari za kuwa bado yu hai ukisambazwa katika mitandao mbalimbali duniani.
Hata hivyo, kilichowatia wazimu zaidi mashabiki wengi wa mwanamuziki huyo miaka ya 1990 ni pamoja na utunzi wa mashairi yake kupitia traki za ‘Wanted Dead or Alive, Who Do U Believe In, To Live and Die in LA na Still Ballin. Nyimbo hizo zilihusiana na mambo ya kifo ama kutoweka kwake.
Kuzaliwa kwake
2pac alizaliwa Juni 16, mwaka 1971, katika miaka yake ya awali aliianza kama mwigizaji na mwanaharakati wa haki za binadamu kabla ya kuhamia kwenye harakati za muziki wa Hip Hop nchini Marekani. Dogo huyo alikuwa mtoto wa Afeni Shakur, ambaye alikuwa mwanachama wa chama cha kisiasa kiitwacho ‘Black Panther Party (BPP).
Upekee wa tukio la kuzaliwa kwake unakumbukwa baada ya mama yake mzazi kujifungua kichanga mwezi mmoja baada ya kutolewa jela.
Mara nyingi washkaji zake walipenda kutumia jina la 2Pac, Pac, Makaveli huku mwenyewe akijitambulisha kwa jina la ‘The Don Kiluminati. Enzi zake 2pac alionyesha uwezo wa juu katika muziki huo hatua iliyosababisha kuishikilia rekodi ya mauzo ya juu kuliko msanii mwingine wa Hip Hop kupitia ‘Guinness World Record.
2pac alipigwa risasi wakati akiendesha gari lake mjini Las Vegas, Nevada ikiwa ni siku saba kabla ya kifo chake kilichotokea tarehe kama ya leo mwaka 1996. Msanii huyo alikuwa akitokea kutazama pambano la Mike Tyson mjini humo.
Vyombo vya habari, mitandao na wadadisi na wachambuzi walieleza taarifa mbalimbali zilizohusisha kifo chake.
Baada ya saa tano tu za kupigwa risasi kwa 2Pac, sehemu ya vyanzo vilianza kumhusisha rafiki yake kipenzi ‘Notorious B.I.G akiwa na Puff Daddy, ambao walionekana katika jengo lililokuwa likipokea mwili wa 2Pac.
Kuhusishwa kwao kulitokana na ishara zilizoonyeshwa na 2Pac akiwatusi kwa vidole wasanii hao wakati akiwa amebebwa kwenye machela kuwahishwa hospitali ili kunusuru uhai wake.
2Pac na Biggie walikuwa ni marafiki wazuri, ambao walipenda kufanya mazoezi ya freestyles na shoo ya pamoja. Kabla ya kifo chake, 2Pac alikuwa tayari ameshahisi uadui mkubwa kati yake na wasanii hao.
Tukio lililokumbushwa ni pamoja na utunzi wa mashairi yaliyochochea dalili za uadui huo kupitia traki ya ‘Who shot ya’ iliyoandaliwa na Biggie baada ya 2Pac kuanzisha kundi linalounga mkono kazi zake.
Biggie alianza kutengeneza ukomavu wa makundi mawili ya wasanii hao kutoka Ukanda wa Magharibi na Ukanda wa Mashariki baada ya kutoa albamu yake ya pili huku wakianza harakati nyingine za kugombea mashabiki.
Haikuchukua muda mrefu Biggie naye alipigwa risasi ambapo taarifa zilidai kuwa hiyo ilikuwa ni sehemu ya kulipiza kisasi baada ya kusambaa kwa hisia hizo.
Albamu zilizobamba baada ya kifo
Mnamo miaka hiyo ya 1990 mauzo yaliyofikia kopi milioni 74 kwa hesabu ya dunia nzima na milioni 44 kwa mauzo ya Marekani pekee. Hatua hiyo ilimfanya kuwa miongoni mwa wasanii wa Hip Hop waliouza rekodi nyingi zaidi duniani.
Albamu za Studio ni kama vile 2Pacalypse Now, Strictly 4 My N.I.G.G.A.Z, Thug Life: Volume 1, Me Against the World, All Eyez on Me na The Don Killuminati: The 7 Day Theory.
Hata hivyo, kuna albamu zilifanya vizuri zaidi sokoni baada ya kifo chake ambazo ni ‘R U Still Down? (Remember Me), Still I Rise, Until the End of Time, Better Dayz, Loyal to the Game na Pac’s Life.