Mfuko wa wasanii watengewa Sh1.5 bilioni, kuanza kazi Julai

Saturday May 29 2021
mfuko pic
By Nasra Abdallah

Mfuko wa Utamaduni wa Sanaa nchini umetengewa Sh1.5 bilioni huku wasanii wakitakiwa kujiandaa kuandika madokezo ya kuomba fedha hizo.

Hayo yamesemwa leo Jumamosi Mei 29, 2021 na Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sanaa kutoka Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Leah Kihimbi kwenye hafla ya uzinduzi wa Chama cha Waigizaji Dar es Salaam (TDFAA).

Mfuko wasanii ulianzishwa rasmi Novemba mwaka 2019 katika kongamano la Sanaa la Mwalimu Nyerere lililofanyika jijini Dar Salaam na kuanzishwa kwake kulikuja kufuatia ombi la wasanii ili uwawezeshe katika uendeshaji wa shughuli zao za sanaa .

Akiuzungumzia, Mkurugenzi huyo amesema Mchoma amesema kuwa ni kiasi hicho cha Sh1.5 bilioni kimetengwa na zitaanza kutumika rasmi Julai mwaka huu mpya wa fedha na kuwataka wasanii wajipange katika kuziomba badala ya kuwa  waoga kufanya hivyo.

"Msiogope kuomba hela pindi mfuko utakapoanza, kwani kadri zitakapotumika ndipo serikali itaona kuna uhitaji wa kutoa au kuongeza,lakini zikirudi wataona hamna haja nazo na hivyo kushindwa kuendeleza kazi zenu," amesema Leah.

Kutokana na hatua hiyo, Mwenyekiti wa Taifa wa chama cha Waigizaji Taifa, Chiki Mchoma amewataka wasanii wasilaze damu katika kuuchangamkia kuzipata fedha hizo.

Advertisement

"Tumelia kwa muda mrefu kuhusu kukosa hela za kuboresha kazi zetu, sasa mfuko wetu huo tayari umejazwa hela, ni wakati wa kuanza kuandika madokezo kwa kuwatumia wataalam mbalimbali sio kusubiri muda ufike ndio tuanze kukimbizana," amesema  Mchoma.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TDFAA, Piere Mwinuka amesema wamefanya uzinduzi huo sambamba na kuja na kampeni ya 'Kipaji ni Kazi' lengo likiwa kutumia vipaji walivyo navyo kujiingizia kipato.

Kupitia programu hiyo, Mwinuka alisema wasanii watapewa elimu, kuundwa vikundi vidogovidogo ndani ya chama  na kuongeza wanachama.

Awali Katibu wa TDFAA, Doris Kante, amesema wakati uingozi mpya ukiwa na miezi mitano tangu uwekwe madarakani, wamefanya mambo mbalimbali ikiwemo kufanya ziara ya kutembelea wasanii.

Huko amesema waligundua changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wamitaji,kutokuwepo bei elekezi ya uuzaji filamu na baadhi ya wasanii kutojua haki zao.

Wakati kuhusu maombi yao kwa serikali, ameomba iwe inawatumia katika hafla mbalimbali za kitaifa kama inavyofanya wa wasanii wa muziki.

Advertisement