Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MAMA NGWEA: Ikipigwa ‘She Gotta Gwan’ nahisi Ngwea yupo na mimi

Muktasari:

  • Marehemu Ngwea ameondoka duniani akiwa kwenye kilele cha umaarufu kutokana na kazi zake alizofanya, leo ni miaka 11 bila uwepo wake na Mwanaspoti limefanya mazungumzo maalumu na mama yake, Denisia Constantine Nandi na anafunguka mengi ikiwemo maisha ya bila ya mwanae kwa miaka hiyo 11.

MEI 28, 2013 Tanzania ilipoteza nguli wa muziki aliyekuwa na ushawishi mkubwa, Albert Mangwea ‘Mangwea’ au ‘Ngwea’ ambaye alifariki dunia ghafla akiwa Afrika kusini alikokwenda kufanya shughuli zake za kimuziki.

Marehemu Ngwea ameondoka duniani akiwa kwenye kilele cha umaarufu kutokana na kazi zake alizofanya, leo ni miaka 11 bila uwepo wake na Mwanaspoti limefanya mazungumzo maalumu na mama yake, Denisia Constantine Nandi na anafunguka mengi ikiwemo maisha ya bila ya mwanae kwa miaka hiyo 11.


MIAKA 11 BILA NGWEA, MAISHA YANAENDAJE?

Mama Ngwea anayeishi Kihonda, Makoti, anasema maisha yanaendelea vizuri. Anaishi na mtoto wake mmoja wa kike na wajukuu zake na hawana changamoyo yoyote.

Ikipita miaka hiyo 11 sasa, mama Ngwea anasema hayupo lakini ni kama yuko naye kwani wanamkumbuka sana.

“Ni kipindi kigumu sana kwetu kuishi bila mtu ambaye tulimzoea kwa muda wote huo, lakini kilichotokea ni mipango ya Mungu na tulishazoea, maana kaka zake, dada zake wote tupo kwa ushirikiano na kikubwa, pamoja na kwamba kimwili hatuko pamoja lakini kiroho tuko pamoja.”


ALIVYOGUNDUA KIPAJI CHA MANGWEA

“Kujua kipaji chake mimi ndiye nilianza kuona viashiria, maana alipokuwa anasoma sekondari huko Dodoma, alikua akija likizo Morogoro muda mwingi anachukua karatasi na kalamu, anakaa pembeni amejitenga. Sasa mimi na baba yake (Marehemu) tukawa tunajiuliza kwa nini anajificha kila wakati na kujitenga, tukawa hatupaji jibu, kumbe hapo ndipo alikuwa anaandika muziki kwa lugha ya kisasa mnaita  ‘Mistari’. Baadae alimweleza dada yake ambaye wanafuatana na akamwambia yeye anaandika muziki na anataka kuwa mwanamuziki mkubwa.”


ILIKUWAJE ALIVYOMRUHUSU?

“Ilifikia wakati ambao rafiki zake wakija kumtembelea wanajitenga pamoja, sasa mimi baada ya kugundua anataka kuwa msanii, nikamwombea ruhusa kwa baba yake kufanya anachopenda, basi familia tukamruhusu na hapo ndipo akaanza kufanya muziki mpaka alipokuwa maarufu na kujulikana Tanzania nzima.”


ATAJWA MICHAEL JACKSON

“Wakati anaanza harakati zake za muziki, mara nyingi tulikuwa tunaangalia mikanda ya Michael Jackson, kumbe mwenzetu alikua anaangalia anavyoimba na kuweka kichwani, ndiyo maana kuna vitu alikua anafanya vinafanana kama Michael Jackson, basi tukamwacha afanye kile anachotaka.”


WATOTO WA MAMA MANGWEA

“Nilibahatika kupata watoto 6 na marehemu Albert Mangwea alikuwa wa mwisho kwenye familia yetu na watoto hawa walipatikana jijini Mbeya ambako tulikuwa tukiishi kwa wakati huo na katika watoto hao sita, watoto wa kiume walikuwa wawili na wa kike wanne.”


MRABAHA WA SERIKALI KWA KAZI ZA MANGWEA

“Tangu huu utaratibu uanze huwa ninapata kulingana na mgao unaotolewa kwa wakati huo. Huwa ninapigiwa simu, ninasafiri hadi jijini Dar es salaam kuchukua. Kwa hilo namshukuru Mungu.”


KUMBUKUMBU YA MANGWEA KWA MAMA

“Kumbukumbu ambayo aliniachia hadi leo najivunia nao ni watu ambao wamekuwa wakija hapa kuniona tangu kufariki kwake. Siwezi kukumbuka ni watu wangapi wameshakuja kuniona ila ni watu wengi na kama mwanangu asingekuwa na upendo na kutengeneza marafiki, sijui ingekuwaje maana siku ya msiba wake uwanja wa Jamhuri watu walivaa Tisheti zilizoandikwa mtu wa watu, ile ilikuwa na maana kubwa kwangu.”


WASANII HAWAJAMTUPA

“Marafiki wa Ngwea kiukweli wanafika kunijulia hali na wengi wao wako karibu, wanafika kuniona akiwemo Jay Mo, Q chifu, TID na wengine ambao siwakumbuki. Kiukweli nashukuru lakini kwa kuwa P Funk Majani alikuwa kama mzazi wake, huwa anapiga simu kila wakati, hilo linanitia moyo na kupitia hao najiona niko karibu na mwanangu.”


UMATI ULIOMZIKA NGWEA

“Nakumbuka siku ya msiba wake, watu walitoka Dar wakatembea kwa miguu hadi hapa Morogoro. Hii ina maana ya upendo ambao alikuwa nao kwa watu, nao walimpenda pia maana yeye hakujali huyu mkubwa au hawa watoto na hilo lilinifanya nione Ngwea sio mwanagu pekeangu bali ni zawadi kwa Watanzania wote, hilo lilinipa faraja na sikuweza kulaumu kwa Mungu kwa nini amemchukua mwanangu,” alisema


WIMBO WA MWANAE ANAOUPENDA

“Mwanangu alitoa nyimbi nyingi kiukweli ila Wimbo ninaoupenda ni ule wa ‘She gotta gwan’ maana una ujumbe mzuri hasa pale aliposema mpenzi wake atamzalia pacha na atamvumilia na ule ujumbe wake wa kuwasihi uvumilivu kwenye ndoa ni jambo kubwa maana maisha ya sasa ndoa nyingi zinavunjika kwa kuwa hakuna kuvumiliana. Hivyo ninaupenda ule wimbo kuliko wimbo wowote ambao amewahi kuimba mwanangu mangwea.”


NGWEA ALIACHA MKE, MJUKUU?

“Mtoto wangu hakuacha mke wala mtoto. Nakumbuka siku ya mazishi kuna mtu alijitokeza akidai amezaa na Mangwea, lakini tulichunguza na kugundua haikuwa kweli. Sisi kama familia na tangu wakati huo hajawahi kurudi, unajua kilichotushtua ni walikuja hapa msibani kuulizia kama aliyekufa ni mwanamke au ni mwanaume hapo tukashtuka lakini hatukuwahi kuwa na taarifa za uwepo wa mke au mjukuu.”


KUNA MRADI ULIACHWA NA NGWEA UNAOKUSAIDIA?

“Kwa kifupi, mradi aliouacha mwanangu ni hizi nyimbo zake alizoziacha ambazo serikali kila mwaka kuna fedha tunapata, lakini pamoja na hayo alifanya mengi ambayo tunamkumbuka nayo, lakini P.Funk anazo nyimbo zote za mwanangu, hivyo ikitokea kuhusu mgao wowote, huwa ananiita maana yule ndiye tuko bega kwa bega wakati wote pamoja na wengine tunaoshirikiana nao na hicho kinanisaidia sana kwenye maisha yangu.”


MABADILIKO YA MISA YA KUMBUKUMBU

“Kila mwaka ikifika tarehe 28, tunaadhimisha kumbukumbu ya kifo chake maana alifariki dunia tarehe kama hiyo mwaka 2013, akiwa nchini Afrika kusini, utaratibu ambao tumekuwa nao, tukifanya sala kanisani, baadae kaburini na kisha kula chakula hapa nyumbani.

Lakini mwaka huu hatutafanya badala yake tutafanya kwa jumla mwezi Desemba na tutakuwa na kumbukumbu ya kifo cha baba yake aliyefariki dunia miaka 15 iliyopita na Mangwea ambaye ana miaka 11 tangu afariki dunia. 

Kwa upande wa tarehe ya Ngwea, kuanzia sasa tutasali kanisani na kwenda kumwombe kaburini na hatutakuwa na shughuli kama ilivyokuwa kila mwaka.”