Juma Kakere: King Kikii, Mafumu walinipunguza kasi
Muktasari:
- Tangu wimbo huo ulipotoka na kuishika nchi kutokana na ujumbe ulioko katika mashairi yake, kumbukumbu hazifutiki kwa mashabiki na ni wazi hata wewe, ukisikia tu wimbo huo haraka litakujia jina la mwanamuziki huyu.
‘POLE kwa Safari’ ndio ngoma iliyomtambulisha nguli huyu wa muziki wa dansi, Juma Kakere.
Tangu wimbo huo ulipotoka na kuishika nchi kutokana na ujumbe ulioko katika mashairi yake, kumbukumbu hazifutiki kwa mashabiki na ni wazi hata wewe, ukisikia tu wimbo huo haraka litakujia jina la mwanamuziki huyu.
Hata hivyo, safari yake ya muziki haijawa rahisi na anakiri amepitia mambo mengi kwa zaidi ya miaka 40 kwenye gemu, ikiwamo aliyoyapanga pamoja na wasanii wengine akiwamo King Kikii na kushindwa kufikia malengo.
Pia anazungumzia shoo zake na kuhusu kazi zake za muziki ambazo anakiri bado yumo.
SAFARI YA ZAIDI YA MIAKA 40
Kakere ni miongoni mwa wasanii waliodumu kwa muda mrefu kwenye muziki wa dansi Tanzania.
Safari yake ilianza miaka ya 1970 akiwa bado mwanafunzi na ameshuhudia mabadiliko makubwa ya tasnia kutoka zama za bendi za dansi hadi enzi za muziki wa kidijitali.
Anasema siri ya kudumu kwenye muziki ni kufanya kazi zenye ujumbe na kugusa maisha ya watu na ukiangalia kizazi cha sasa kina nafasi kubwa ya kujifunza kutoka kwa muziki wa zamani ulioweka mkazo kwenye mashairi, maadili na hadithi za maisha ya kila siku.
BADO HAJAFUNGA UKURASA
Pamoja na kupunguza idadi ya maonyesho, Kakere anasema hajastaafu muziki na bado anaendelea kuandika pamoja na kurekodi nyimbo mpya.
“Muziki bado upo ndani yangu. Nina kazi kadhaa tayari na muda si mrefu mashabiki wataanza kuzisikia. Bado nina mengi ya kutoa,” anasema.
Kwa msanii huyo ambaye ameshuhudia vipindi tofauti vya muziki wa dansi nchini, anaamini nyimbo nzuri haziishi. Labda ndiyo sababu hadi leo, zaidi ya miaka 20 tangu itoke, Pole Kwa Safari bado inaendelea kuishi kwenye masikio ya mashabiki wengi wa muziki wa dansi Tanzania.
AUMIZWA NA KING KIKII, MAFUMU
Kakere anasema kuwapoteza wanamuziki wakubwa kama King Kikii na Mafumu Bilali kumemfanya apunguze kasi ya kuachia kazi zake mpya licha ya kuendelea kutunga nyimbo hadi sasa.
MRADI WAO UMEKUFA
Anasema kuwapoteza wasanii hao kumeua mradi wao mkubwa waliopanga kuufanya kwani kuna kazi amefanya nao na aliamini ungekuwa kwa kiwango kikubwa.
“Baada ya kuwapoteza King Kikii na Mafumu Bilali, pamoja na changamoto nyingine zilizoukabili mradi huo, nilinyong’onyea kuusukuma wimbo wa Utu Si Pesa kama nilivyokuwa nimepanga,” anasema Kakere.
UTU SI PESA ILIBEBA NDOTO KUBWA
Anasema wimbo wa Utu Si Pesa aliourekodi mwaka 2019 chini ya mtayarishaji Erasto Mashine ni moja ya kazi anazozithamini zaidi kutokana na ujumbe wake pamoja na mkusanyiko wa majina makubwa ya muziki wa dansi yaliyoshiriki.
Anasema baada ya vifo vya King Kikii na baade Mafumu hamasa ya kuusukuma wimbo huo ilipungua na hatimaye kazi hiyo kubaki mikononi mwa mashabiki wachache walioweza kuisikia.
“Ulikuwa mradi wa watu ambao nilikuwa nawathamini sana. Hadi leo nikikumbuka namna tulivyopanga mambo mengi kuhusu kazi hiyo napata huzuni,” anasema.
POLE KWA SAFARI BADO NI NEMBO YAKE
Licha ya changamoto hizo, anaendelea kufurahia mafanikio ya wimbo ‘Pole Kwa Safari’ ambao hadi leo bado unapendwa na mashabiki wa dansi nchini.
Msanii huyo anasema kabla ya wimbo huo tayari alikuwa ameshatengeneza jina kupitia kibao cha Betty mwaka 2001, lakini Pole Kwa Safari ndiyo kilichompa mafanikio makubwa zaidi.
“Betty ulinipa mwanga, lakini ‘Pole Kwa Safari’ ilinifungulia milango mingi zaidi. Nilipata maonyesho mengi na watu wakaanza kunitambua kwa kiwango kikubwa,” anasema.
Kwa mujibu wa Kakere, mafanikio ya wimbo huo yaliongezwa na video yake iliyomshirikisha mwigizaji maarufu wa Kaole Sanaa, Christina Manongi maarufu Sintah.
Anasema wazo la kumshirikisha Sintah lilitokana na mashauriano kati yake na msanii wa bendi ya Msondo ngoma, Karama Regesu, huku wakiamini staa huyo alikuwa akipanda kwa kasi katika tasnia ya filamu na angeongeza mvuto wa kazi hiyo.
Video hiyo ilipata nafasi kubwa kwenye vituo vya televisheni na kuwafanya mashabiki wengi kuikumbuka hadi leo.
KWA NINI HAPIGI SHOO KILA WIKI?
Tofauti na baadhi ya wanamuziki wa dansi wanaopanda jukwaani karibu kila wiki, Kakere anasema kwa sasa amefikia hatua ambayo anachagua zaidi maonyesho ya kushiriki kutokana na umri wake na mahitaji ya mwili kupumzika.
Anasema bado anaupenda muziki, lakini haoni sababu ya kujilazimisha kufanya maonyesho ya mara kwa mara bila kupata muda wa kupumzika.
“Umri umeenda. Siwezi tena kufanya shoo kila wiki kama zamani au kama wanavyofanya baadhi ya wanamuziki wengine. Mwili unahitaji mapumziko pia,” anasema.
Anasema kwa sasa anaimba zaidi katika harusi, send-off, sherehe za kitaifa, kampeni, matukio maalumu na maonyesho anayopata kwa mialiko rasmi.
“Napiga muziki kwa mialiko maalumu. Ukifanya shoo kila wiki mwanamuziki unachoka na wakati mwingine hukosi hata muda wa kupumzika. Mimi kwa sasa nafanya muziki kwa utaratibu unaonipa nafasi ya kuendelea kuwa na afya njema na kufanya kazi zangu nyingine,” anasema.
Pamoja na kupunguza idadi ya maonyesho, amesisitiza bado hajastaafu muziki na anaendelea kuandika pamoja na kurekodi nyimbo mpya ambazo anatarajia kuzitoa siku zijazo.
Kwa msanii huyo mkongwe, anaamini bado ana mengi ya kutoa licha ya kupunguza kasi ya maonyesho, akisisitiza kuwa muziki bado upo moyoni mwake.
USHAURI KWA WANAMUZIKI WA SASA
Kakere anawataka wanamuziki wa sasa wa dansi kutambua muziki si mashindano ya kasi ya kutoa nyimbo, bali ni ubora na uvumilivu unaojenga historia ya kudumu.
“Wanamuziki wa sasa wajifunze kuwa si kila kitu ni kukimbizana kutoa kazi kila wakati. Muziki unataka ubora, nidhamu na uvumilivu. Maana kazi nzuri haifi,” anasema.
Anasema pia wasanii wanapaswa kujifunza kuheshimu historia ya muziki wa zamani na kujenga kazi zenye ujumbe unaogusa maisha ya watu.