Gigy ajiachia na bendera ya Tanzania nchini Kenya

Licha ya kufungiwa kutojishughulisha na kazi za Sanaa, msanii Gift Stanford, maarufu Gigy ameonekana akijiachia nchini Kenya akiwa na bendera ya Tanzania.
Gigy ambaye ni msanii wa Bongofleva na filamu, Januari 5, 2021, Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), lilitangaza kumfungia miezi sita kutojihusisha na kazi za sanaa ndani na nje ya nchi.
Maamuzi hayo ambayo yalitangazwa na Kaimu Katibu Mtendaji wa barza hilo, Matiko Mniko, yalieeleza kuwa wamefikia hatua hiyo baada ya Gigy akiwa katika tamasha la ‘Tumewasha Tour’ ,jijini Dodoma alivua nguo na kubaki na vazi lilionyesha maungo yake ya mwili.
Baraza hilo lilieleza kuwa kitendo hicho kilidhalilisha utu wa msanii huyo na kubughudhi hadhira ya wapenda sanaa ndani na nje ya nchi.
Pamoja na kutumikia adhabu hiyo ambayo ndio kwanza ana miezi nayo miwili, msanii huyo ameonekana katika mitandao ya kijamii nchini Kenya akiwa anapokelewa na wenyeji wake kwa ngoma na nyimbo, huku akiwa amejifunika bendera ya Tanzania.
Gigy ambaye alikuwa amevalia suruali nyeusi na blauzi nyeusi inayoishia juu ya kitovu, kuna wakati pia alifunga bendera hiyo kiunoni na kuanza kukatika.
Mwananchi iliwatafuta Basata kujua kama wamempa kibali hicho, ambapo kupitia msemaji wake Agnes Kimwaga, alisema hawana taarifa nayo na hata hiyo bendera hawajui kaipata wapi.
“Gigy bado yupo kwenye adhabu mpaka ninavyozungumza na wewe hapa, hatujamfungulia, na hiyo bendera huenda kajishonea, lakini tunafuatilia tujue ilikuwaje mpaka akafanya hivyo,”alisema msemaji huyo.
Pia tulimtafuta Gigy kupitia simu yake ya kiganjani, ili kujua ni shughuli gani haswa ilimpeleka huko, lakini simu yake haikuwa ikipatikana hewani.