Diamond ang’ara vipengele saba, Rosa Ree aking’ara vinne tuzo za Afrima

Thursday September 23 2021
diamond pic
By Nasra Abdallah

Wasanii wa Tanzania, Diamond Platnumz na Rosa Ree wameonekana kung’ara kwenye vipengele vingi kwenye tuzo za Afrima zinazorajiwa kufanyika Novemba mwaka huu nchini Nigeria.

Orodha ya wateule wa tuzo hizo imeanikwa jana Jumatano Septemba 22, 2021 ambapo wasanii wengi kutoka Tanzania wakiingia katika vipengele 13, huku Diamond na Rosa Ree wakijitokeza kwenye vingi zaidi ya wengine.

Kwa upande wa Diamond wimbo wa Waah! Ndio umembeba, kwani licha ya kumuingiza katika vipengele vine pia wimbo huu umetajwa katika vipengele saba ikiwemo Wimbo wa mwaka, video ya mwaka, Wimbo unachezeka,  wimbo bora wa kushirikiana.

Aidha Waah!  umemuingiza msanii huyo katika vipengele vya msanii bora wa mwaka na  msanii bora wa kiume Afrika Mashariki.

Wimbo huo uliotoka miezi tisa iliyopita na mpaka sasa umeshatazamwa mara milioni 85.

Ukiacha Diamond mwingine aliyejitokeza kwenye vipengele vingi katika tuzo hizo, ni msanii wa muziki wa kufokafoka, Rosa Ree,ambaye ameingia katika vipengele vinne.

Advertisement

Vipengele alivyotajwa Rosa Ree na wimbo wake  kwenye mabano ni Msanii bora wa kike,Msanii bora wa Hiphop, msanii wa muziki wa Raggae Dancehall(That Girl) na msanii bora wa kike Afrika Mashariki.

Msanii mwingine ni Zuchu ambaye anayewania vipengele vitatu ikiwemo cha wimbo wa mwaka kupitia wimbo wa Number One alioshirikishwa na Rayvanny.

Kipengele kingine ni Msanii anayechipukia na Msanii bora wa kike Afrika Mashariki ambapo anachuna na akina Nandy, Spice Diana na Rosaree.

Yupo Alikiba ambaye yeye anawania kipengele cha Chaguo la Watazamaji kupitia wimbo wake wa Jelous na msanii bora wa kiume Afrika Mashariki akichuana na wakina Diamond, Harmonize,Darasa na  Rayavanny.

Aidha yupo Dj Sinyorita akiwania kipengele cha DJ bora, Mwandaaji wa Muziki Laizer anayewania kipengele cha mwandaaji muziki bora wa mwaka na Derecror Kenny anayewania kipengele cha Muongozaji bora wa Video wa mwaka kupitia wimbo wa Waah.

Tuzo zote za Muziki Afrika hufanyika kila mwaka na zilianzishwa na Kamati ya Kimataifa ya AFRIMA, kwa kushirikiana na Jumuiya ya Afrika kwa lengo la kutuza na kusherehekea kazi za muziki, talanta na ubunifu kote bara la Afrika huku ikitangaza urithi wa kitamaduni wa Kiafrika

Advertisement