Ben Pol: Sijaishiwa, tulieni!

MSANII wa bongo fleva, Ben Pol amesema hana presha ya kuachia nyimbo mara kwa mara kwa kuhofia ushindani sokoni, kitu anachokiamini ni kazi nzuri na kujua mashabiki wake wanahitaji ujumbe gani na kwa wakati gani.

Ben Pol amesema kwamba muziki anauona ni maisha na unamgusa binadamu wa aina yoyote kulingana na chagua la aina ya nyimbo anazotaka, hilo ndilo linamfanya awe mtulivu wa aandike ujumbe gani.

Amesema aina ya muziki wake anapenda kuimba uhalisia na visa ambavyo vinakuwa vinawagusa moja kwa moja wale anaowapelekea kazi zake na kwamba ndio sababu ya kutokuwa na papara ya kuachia nyimbo kila wakati.

"Muziki ni maisha, kuna wakati binadamu akisikiliza unamburudisha, unamfariji na kumfundisha, ndio maana kabla ya kufanya jambo lolote huwa nakaa chini na kutafakari ni aina gani ya mashairi yanafaa na kwa wakati gani;

Ameongeza kuwa "Ndio maana nimsema kila mtu anaupenda muziki kulingana na staili yake ya maisha na ndio maana ipo ya kidini na kidunia yote ni miziki, kabla sijatoa mashairi naangalia uhalisia wa nyakati tulizopo,"amesema.

Amesema kutokutoa nyimbo hakuna maana kwamba ameishiwa mashairi, amefichua ana nyimbo nyingi zipo stoo ambazo ukifika muda ataziachia kwa wadau wanaopenda muziki wake.
"Ninaposema muziki ni maisha maana yangu nyingine binafsi nina maishairi mapya kila siku yanayotokana na uhalisia wa maisha, mazingira, marafiki na mambo mbalimbali," amesema.