Amitabh, Shah Rukh Khan wamlilia Dharmendra
Muktasari:
- Staa huyo Sholay na Loha, amefariki wiki chache kabla ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa ya miaka 90 ambayo ingeadhimishwa Desemba 8.
SAA chache baada ya mwigizaji mkongwe wa filamu, Dharmendra, kufariki dunia nyumbani kwake leo Jumatatu, Novemba 24, ikithibitishwa na Shirika la Habari la IANS, rafiki yake wa muda mrefu na mshirika wa mara kwa mara katika kazi, Amitabh Bachchan pamoja na mwanawe Abhishek wamefika nyumbani kwa marehemu kutoa heshima za mwisho.
Staa huyo Sholay na Loha, amefariki wiki chache kabla ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa ya miaka 90 ambayo ingeadhimishwa Desemba 8. Gwiji huyo alizaliwa tarehe hiyo 1935 na kuanza kuigiza miaka ya 1960 hadi mauti yalipomkuta akiwa anajiandaa kushuhudia uzinduzi wa kazi yake ya mwisho iitwayo Ikkis iliyopangwa kutolewa Desemba 25.
Mbali na Amitabh na mwanawe Abhishek, pia mkongwe na swahiba huyo wa Dharmendra alikambatana na mjukuu wake Agastya wakati wakiwasili. Aamir Khan pia alifika kutoa heshima za mwisho sambamba na Rajkumar Santoshi, rafiki wa familia ya kina Deol.
Mastaa wengine ni pamoja na Sanjay Dutt na Salim Khan pia walikuwamo miongoni mwa waliofika kutoa heshima zao, huku Shah Rukh Khan na Salman Khan, ambao hapo awali walimtembelea Dharmendra alipokuwa amelazwa katika Hospitali ya Breach Candy mjini Mumbai, pia waliwasili.
Akshay Kumar, Anil Kapoor, Gauri Khan, mkongwe Saira Banu pamoja na Deepika Padukone na Ranveer Singh nao waliwasili kutoa heshima za mwisho.
Duru za habari kutoka India zinasema tangu asubuhi baada ya taarifa ya kifo cha gwiji huyo, hali ya taharuki iliongezeka, huku ulinzi ukiongezwa nje ya nyumba ya Dharmendra. Ambulansi ilionekana ikiingia katika eneo hilo.
Esha Deol, binti wa Dharmendra na Hema Malini, alionekana akiwasili nyumbani hapo. Hema Malimi ni mke wa pili wa Dharmendra aliyebahatika kuzaa naye Eshe Deol, huku Sunny na Bobby Deol wakizaliwa na aliyekuwa mke wa kwanza wa mkongwe huyo aliyecheza zaidi ya filamu 200 enzi za uhai wake.
Hata hivyo, taarifa rasmi kutoka kwa familia bado inasubiriwa kuelezea taratibu za mazishi ya mwigizaji huyo. Dharmendra aliruhusiwa kutoka Hospitali ya Breach Candy Novemba 12. Alikuwa akipatiwa matibabu tangu Oktoba 31 baada ya kulalamika kushindwa kupumua vizuri.
Dharmendra, mmoja wa waigizaji mashuhuri zaidi wa filamu za India, alijulikana kupitia filamu kama Sholay, Dharam Veer, Chupke Chupke, Mera Gaon Mera Desh na Dream Girl.
Mara ya mwisho alionekana katika filamu ya Teri Baaton Mein Aisa Uljha Jiya, iliyochezeshwa na Shahid Kapoor na Kriti Sanon.