Alikiba anavyopeta na Baby Mama wa Diamond

NI wazi mwimbaji wa Kings Music, Alikiba anajipigia mapande ya nguvu kutoka kwa wazazi wenziye (Baby Mama) na mshindani wake upande wa muziki, Diamond Platnumz.

Hamisa Mobetto na Tanasha Donna ambao tayari wamebwagana na Diamond, wana himaya yao katika ulimwengu wa Alikiba, huku warembo hao wanaupiga mwingi tu.

Hilo limezidi kujionyesha mara baada ya hivi karibuni Alikiba kuachia albamu yake ya tatu ‘Only One King’ yenye nyimbo 16. Je, ni lini na wapi na kwa namna gani Alikiba anapeta na hao Baby Mama wa Diamond kimuziki?


HAMISA MOBETO

Katika video ya wimbo wake ‘Dodo’ iliyotoka Aprili 2020, Alikiba ameupiga mwingi ndani yake kwa kuachia na Hamisa Mobetto ambaye ametokea kama video vixen licha ya kuachana na kazi hiyo kitambo ila Kiba akamrejesha tena.

Utakumbuka Septemba 2016 Hamisa aliipendezesha vilivyo video ya Diamond ‘Salome’ na kujizolewa umaarufu zaidi, baada ya hapo ndipo penzi lao la siri likachipuka hadi kupata mtoto mmoja.

Kitendo cha Hamisa kwenda kufanya video ya Alikiba, kikachochea mijadala mingi, Diamond akaibuka na kusema yeye ndiye alimruhusu Bibie kwenda kufanya video hiyo, hata hivyo mrembo huyo alikanusha vikali hilo, huku akisisitiza hiyo ni biashara yake binafsi.

Video hiyo ambayo imewekwa Youtube kwenye chaneli ya lebo ya Alikiba, Kings Music tayari imetazamwa zaidi ya mara milioni 15, na kuwa video ilivyovutia watazamaji wengi zaidi kuliko yoyote ile kwenye chaneli hiyo hadi sasa.

Hamisa ambaye naye anafanya muziki, kipindi akiwa na ukaribu na Diamond aliweza kutia sauti yake katika nyimbo za mwimbaj huyo kama ‘Nikifa Kesho’na ‘Jibebe’ ingawa hakutajwa kama amehusika.


TANASHA DONNA

Mara baada ya Dar es Salaam, Alikiba alienda pia kufanya listening party Nairobi, Kenya ambapo aliwaalika wasanii wa huko kama Otile Brown, Khaligraph Jones, Nyashinski Nameless, Wahu, na Tanasha.

Hata hivyo, siku kadhaa nyuma Alikiba alikuwa na Tanasha visiwani Zanzibar ambapo mrembo huyo aliungana na mwimbaji wa Kings Music, Tommy Flavour katika kushuti video ya wimbo wao ambao upo mbioni kutoka.

Katika hafla hiyo Tanasha alimpongeza Alikiba kwa kuachia albamu hiyo kwa kueleza Afrika na dunia nzima watasikiliza kutokana na ubora wake.

Ikumbukwe Tanasha ambaye Desemba 2015 alitokea kwenye video ya Alikiba ‘Nagharamia’, hajashirikishwa kwenye albamu hiyo lakini katika mahojiano na Wanahabari alisema Alikiba ni sehemu ya familia yake.

Tanasha alienda mbali kwa kukiri ni kweli alikataa kutokea kwenye video mpya ya wimbo wa Diamond ‘Naanzaje’ licha ya kuombwa vilivyo na mzazi huyo mwenziye. Wawili hao waliachana Aprili 2020 kwa kile Tanasha alichodai mama yake Diamond, Bi. Sandra (Mama Dangote) alikuwa akiingilia sana mahusiano yao.

Ikumbukwe Tanasha ambaye amejaliwa mtoto mmoja na Diamond, kabla ya kuachana kwao alifanikiwa kurekodi wimbo mmoja na mwimbaji huyo ‘Gere’ unaopatikana kwenye Extended Playlist (EP) yake iitwayo DonnaTella EP iliyotoka Februari 2020 ikiwa na nyimbo nne alizowashirikisha wasanii wengine kama Khaligraph Jones na Mbosso.