Wasanii wa AliKiba waibukia kwa Harmonize

Tuesday September 8 2020

 

By Nasra Abdallah

Hatimaye wasanii wa AliKiba wajiunga na lebo ya Kondeboy inayomilikiwa na msanii Harmonize.
Wasanii hao Cheed na Killy waliokuwa chini ya lebo Kings Music inayomilikiwa na Alikiba, waliachana na lebo hiyo Aprili mwaka huu kwa kile walichoeleza wanataka kwenda kujitegemea.
Hata hivyo jana mmoja wa viongozi wa lebo Kondegang anayejulikana kwa jina la Chopa,  katika ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram, aliweka bayana kuwa wasanii hao tayari wamejiunga na lebo hiyo kwa kuweka picha ya Cheed akiwa na Harmonize na Ibra msanii wa kwanza kusajiliwa kwenye lebo hiyo.
Picha hiyo ilisindikizwa na maneno chini yaliyosomeka "karibuni kwenye familia ya Konde Gang, naamini katika kipaji mlichonacho, haya ni muda sasa wa kuwaonyesha watanzania”
Utambulisho huo pia umeandikwa kwenye ukurasa rasmi wa Instagram wa lebo hiyo.
Kwa upande wake Cheed, alishukuru kujiunga na lebo hiyo na kueleza kutosahau mchango wa AliKiba katika safari yake hiyo ya muziki.
Kujiunga kwa wasanii hao,kutaifanya lebo ya  Kondegang worldwide kuwa na wasanii wanne kwa sasa akiwemo Harmonize na Ibra aliyesajiliwa Aprili mwaka huu.

Advertisement