Twanga Pepeta sasa mbele kwa mbele

Wednesday April 29 2020

 

By RHOBI CHACHA

BENDI  ya muziki wa dansi nchini, The African Stars International 'Twanga Pepeta', imevunja ukimya kwa kuachia ngoma mpya iitwayo 'Twanga Mbele' ambayo imeanza kufanya vema hewani.
Wimbo huo mpya umetayarishwa na prodyuza Erasto Mashine katika Studio za iSTUDIO zilizopo Kinondoni, Dar es Salaam ikiwa ni utunzi wa kiongozi wa bendi hiyo, Kalala Junior.
Ndani ya ngoma hiyo, waimbaji Chaz Baba, Msafiri Diouf, Kalala Junior, Luiza Mbutu na Dogo  Piano wamefanya yao, huku kwenye ala zikipigwa na Jojoo Jumanne, Gody Kanuti na Drums Kirikuu
Hiyo ni ngoma ya kwanza kwa bendi hiyo maarufu nchini, tangu walipoachia kazi zao mbili zilizobamba kinoma za Povu na Rekebisha kabla ya kupiga kimya kirefu, japo walikuwa wakiendelea na shoo zao kabla ya marufuku ya kupisha janga la corona kutangazwa na serikali.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kalala Junior amesema kulikuwa na lengo la kuachia ngoma hiyo ya Twanga Mbele ukiwa na audio na video yake, lakini kutokana na corona wamesitisha mpango wa video wakisuburi kwanza janga hilo lipungue.
"Watu wanatuuliza sana kwanini hatujatoa video yake, baada ya kuisikia audio ambayo inafanya vema kwenye mitandao ya kijamiii, lakini ukweli ni kwamba Mungu akijaalia ili janga la corona  likipa fasta tutawashushia video sababu maandalizi yalishaanza kitambo sema basi tu," amesema mtunzi na mwimbajji huyo ambaye ni mtoto wa gwiji wa muziki wa dansi nchini, Komandoo Hamza Kalala 'Mzee wa Madongo' aliyewahi kutamba na bendi mbalimbali nchini ikiwamo Vijana Jazz, Bantu Group, UDA Jazz na Washirika Tanzania Stars.
Aidha Kalala Junior  amewaomba mashabiki wa bendi hiyo kipindi hiki cha kukaa nyumbani kutokana na ugonjwa wa covid-19, watumue muda kusikiliza Twanga Mbele kupitia mtandao wa YouTube ambapo tayari wameshaiweka.

Advertisement