Tamasha la Muziki laishtua Serikali

Muktasari:

  • Makundi 30 ya ngoma za asili yaliyoshiriki tamasha hilo linalofanyika kila mwaka nchini.

Dar es Salaam. Tamasha la muziki wa Cigogo limeishtua Serikali ikilitaja kuwa na taswira ya muendelezo wa heshima ya Tanzania katika sanaa Afrika Mashariki na Kati.
Tamasha hilo la 11 msimu huu limefanyika kwenye viwanja vya Chamwino Ikulu mjini Dodoma.
Kaimu mkurugenzi wa Idara ya Sanaa, Joyce Fisoo alisema tamasha la Cigogo limezidi kuwa kivutio na kuitambulisha sanaa ya Tanzania kimataifa.
Alisema waudhuriaji kutoka mataifa ya Marekani, Uganda, Hispania, Thailand, Zambia, Ujerumani, Bulgaria, Ethiopia na Argentina ni taswira kuwa sanaa ya Tanzania inapendwa na kuvutia.
Fisoo aliyewahi pia kuwa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Filamu Tanzania, amesema kutokana na utendaji uliotukuka kwa waandaaji wa tamasha la Cigogo na Kituo cha sanaa Chamwino (CAC) atatoa cheti maalum kwa ajili ya kutambua na kuthamini mchango wa taasisi hiyo.
Alisema kwa sababu ya ukubwa wa tamasha hilo, ataishawishi serikali kuliongezea nguvu zaidi kwa sababu ya maudhui yake.
Mwenyekiti wa tamasha hilo, Dk Kedmon Mapana alisema tamasha hilo limekuwa fursa kwa wasanii kujitangaza na kuitangaza nchini.
Wadau mbalimbali akiwemo Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Godfrey Mngereza, Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi, Adrian Nyangamale na wadau wengineo walitembelea mabanda ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaa (UDSM), Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Basata, Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA) na Bodi ya Filamu.