Mastaa hawa swaumu imepanda buana!

WAISLAM wote duniani wapo kwenye Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, wakitekeleza Nguzo ya Nne kati ya tano za dini yao kwa kujizuia kula na kunywa wakati wa mchana sambamba na kujikithirisha kufanya ibada ili kuomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu.
Kama ilivyo kwa waumini wengine wa dini hiyo, baadhi ya mastaa nchini ambao wameupokea na kuingia kwenye swaumu wamezungumza jinsi mfungo wa safari hii ulivyowabamba, hasa kukiwa na janga la virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa covid-19.

Seleman Jabir ‘Msaga Sumu’,
Huyu jamaa ni mkali wa muziki wa singeli, ngoma zake kadhaa ikiwamo Shemeji, Mwanaume Mashine na nyingine zikiendelea kukimbiza amesema kama muumini huwa hakwepi mfungo na hata safari hii ameuanza tangu mwezi ulivyoandama, huku akiwatakia mashabiki wake kuwa makini na corona ambayo imewatibulia mfumo wa maisha waliouzoea kitambo.
"Nashukuru nimeupokea salama kabisa na ninafunga kwani ni wajibu wangu ikiwa moja ya nguzo ya Kiislamu, pia nawatakia kila la kheri Waislamu wote na wasio Waislamu katika kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhan. Nawakumbusha tu kufunga na ibada ni muhimu sana.”

Kalala Junior
Mkali wa muziki wa dansi nchini yeye kwa upande wake amesema;
"Nimeupokea vizuri huu mwezi na nimejaaliwa kufunga, hivyo nawakumbusha tu Waislamu wenzangu huu mwezi ni lazima kufunga endapo Mwenyezi Mungu ametupa uzima na afya njema. Tunafanya mambo mengi ndani ya miezi 11, tunashindwaje kufunga mwezi mmoja?”

Haji Salum 'Mboto'
Msanii wa vichekesho hapa nchini amesema haya; "Mwezi huu wa Ramadhan nimeupokea vizuri sana na nafunga kama kawaida yangu kila mwaka, ila nawashauri wasanii wenzangu na hata wasio wasanii tujaribu kujiheshimu kimavazi ili kuweza kulinda swaumu zetu. Pia isiwe kwa mwezi huu tu bali hata miezi mingine tufanye hivyo.”

Khadija Yusuf
Mwimbaji huyu wa miondoko muziki wa taarabu amesema haya "Mwezi huu nimeupokea vizuri kabisa na huwa naupenda sana kutokana na asilimia kubwa ya watu kubadilika kimavazi na hata kuzidisha ibada. Napenda huu ungekuwa kwa miezi yote 12, ingependeza kabisa.”

Khadija Kopa
Mkali mwingine wa taarabu nchi amesema haya'; "Mwezi huu nimeupokea vizuri kabisa na huwa naupenda sana kutokana na asilimia kubwa ya watu kubadilika kimavazi na hata kuzidisha ibada.”
"Pia niwakumbushe kuwa kuna corona, hivyo wawe makini na kuepuka mikusanyiko na kujilinda kwa kuvaa barakoa kokote waendako, bila kusahau kunawa kwa maji na sabuni na vitakasaji vingine na kubwa ni kuzingatia maelekezo ya serikali na wahudumu wa afya kwa usalama zaidi."
Mfungo wa Ramadhani ni moja ya nguzo tano za Kiislam ambapo muumini hujizuia kula na kunywa mchana sambamba na kuepuka madhambi na kujikithirisha kuomba msamaha kwa Mungu na masiku yake huwa kati ya 29 au 30 kabla ya kufuatiwa na Sikukuu ya Eid El Fitry.