Ebitoke ajitosa kuwania taji la Miss Tanzania

Friday February 28 2020

Ebitoke ajitosa kuwania taji la Miss Tanzania,MSANII wa filamu na mchekeshaji nchini Tanzania,Anastazia Exavery , taji la Miss Tanzania 2020,

 

By Nasra Abdallah

MSANII wa filamu na mchekeshaji nchini Tanzania, Anastazia Exavery maarufu Ebitoke amejitosa kuwania taji la Miss Tanzania 2020.
Msanii huyo amejizolea umaarufu kutokana na vichekesho vyake ambapo hutumia rafudhi ya Kihaya na pia amekuwa akijipaka masizi kwenye nyusi  na mafuta mengi usoni.
Ebitoke amesema zipo sababu tatu kubwa zilizomsukuma kushiriki mashindano hayo mojawapo kujiamini kuwa yeye ni mrembo.
“Mimi ni mrembo na nisingependa kutumia urembo huu kwa mambo mengine yasiyokuwa na tija, ndio maana nimeamua kutumia nafasi hii ya mashindano na  kushiriki kwa kuwa kuna fursa nyingi,”amesema msanii huyo.
Jambo lingine amesema ni kutokana na kuwa mfano kwa vijana wengi ambao wamekuwa wanamfuatilia, hivyo ametaka kuwaonyesha kuwa hakuna kinachoshindikana kukifanya kama unajiamini na itasaidia kushawishi wengine kushiriki mashindano hayo.
Wakati jambo la tatu amesema yeye kama msanii anapaswa kubadilika, hivyo kuingia kwake kwenye urembo ni moja  ya njia kuonyesha kipaji chake kingine mbali ya kuigiza filamu na vichekesho.
Mwandaaji wa mashindano hayo, Basila Mwanukuzi amethibitisha ushiriki wa msanii huyo ambaye ameeleza kuwa amerudisha fomu jana Alhamisi.
Ebitoke ambaye amedai kuwa ana umri wa miaka 22 ana elimu ya msingi ambapo kwa taratibu ya mashindano hayo mshiriki anapaswa kuwa na elimu ya sekondari kuanzia kidato cha nne na kuendelea.
Ebitoke yeye ana elimu ya msingi aliyopita katika Shule ya Msingi Kalema iliyoko Chato kuanzia mwaka 2006 hadi 2013. Kwa upande wa umri kwenye mashindano hayo mshiriki anatakiwa awe na umri kuanzia miaka 18 hadi 24.

Advertisement