Wenger haishiwi visa

Muktasari:
Mahasimu hao, Arsenal na Spurs kesho Jumapili watakutana kwenye ligi mchezo utakaofanyika huko White Hart-Lane.
London, England. Kocha Arsene Wenger amesisitiza kwamba dhamira ya Arsenal ipo palepale kuhakikisha inamaliza Ligi Kuu England msimu huu ikiwa juu ya mahasimu wao Tottenham Hotspur.
Kwa kauli hiyo ya Wenger ina maana ana uhakika kwamba Arsenal itamaliza ligi ndani ya Top Four baada ya sasa kuwa wamezidiwa pointi 14 na Spurs, lakini wababe hao wa White Hart-Lane wakiwa wamecheza mechi moja zaidi ya wapinzani wao. Mahasimu hao, Arsenal na Spurs kesho Jumapili watakutana kwenye ligi mchezo utakaofanyika huko White Hart-Lane.
Mechi hiyo itatoa matumaini Wenger kama kweli ataweza kumaliza ligi juu ya Spurs au la, kwani akishinda atakuwa amepunguza pointi na kufikia 11, huku wao watakuwa wamebakiza mechi tano na Spurs mechi nne.
Kocha wa Spurs, Mauricio Pochettino amesema kikosi chake kinawaza mambo makubwa zaidi msimu huu kuliko kumaliza ligi juu ya Arsenal. Spurs kwa sasa wapo nyuma kwa pointi nne tu dhidi ya vinara Chelsea, hivyo wanahitaji kushinda mechi zao ili kukimbizia taji hilo. Chelsea nao kesho watakuwa na shughuli pevu ugenini kwa Everton, huku vita ya Top Four ikiwa kali pia kwa Man United wao kucheza na Swansea City nyumbani na Man City watakuwa ugenini kwa Middlesbrough.
“Lengo letu ni kumaliza ndani ya Top Four, hapo tutakuwa tumeendeleza heshima yetu na hasa kile tunachokitaka kumaliza juu ya Spurs," alisema Wenger.