Yanga, Biashara milango migumu dakika 45

Muktasari:

Katika kipindi hiko cha kwanza wenyeji Biashara United walionekana kutengeneza mashambulizi matatu ya wazi ambayo kama wangekuwa makini huenda wangepata bao la kuongoza.

KIPINDI cha kwanza kimemalizika kwa wenyeji Biashara United, kutoka suluhu dhidi ya wapinzani wao Yanga katika mechi ya Ligi Kuu Bara ambayo ilianza saa 10:00 jioni katika uwanja wa CCM Karume mkoani Mara.

Katika kipindi hiko cha kwanza wenyeji Biashara United walionekana kutengeneza mashambulizi matatu ya wazi ambayo kama wangekuwa makini huenda wangepata bao la kuongoza.

Mashambulizi hayo matatu ya Biashara United, ambayo yalikuwa hatari kwa Yanga lilikuwa faulo moja ambayo ilikwenda kuokolewa na kipa, Farouk Shikhalo, la pili mshambuliaji Atupele Green alionekana kukosa umakini wakati lile lingine walinzi wa Yanga waliokoa.

Biashara mbali ya kufanya mashambulizi matatu ya maana walionekana kutawala mpira muda mwingi kuliko Yanga kwani waliweza kupiga pasi ndefu na fupi zisisopungua tano na baada ya hapo ndio hupoteza mpira.

Kwa upande wa Yanga wao walionekana kufanya mashambulizi machache na mengi yalikuwa ya kawaida si yale ya kuwashtukiza wapinzani wao Biashara ambao walionekana kuwa imara katika ngome yao ya ulinzi.

Yanga katika kipindi cha kwanza walikuwa wakipoteza mipira mingi na hata pasi zao zilikosa macho kwa maana ya kudakwa na wachezaji wa timu pinzani wakati huo huo mastraika wao wawili David Molinga na Ditram Nchimbi walionekana kukabika vyema na safu ya ulinzi ya Biashara United.