Simba yaanza kutafuta mchawi

Muktasari:

Tayari Patrick Rweyemamu na Mohamed Mwalami wameonyeshwa mlango wa kutokea Simba.

 

Dar es Salaam. Hali bado si shwari katika klabu ya Simba, baada ya juzi kumwondoa meneja wake, Patrick Rweyemamu katika nafasi yake pamoja na kocha wa makipa, Mohamed Mwalami ‘Shilton’.

Habari za kuondolewa kwa Shilton na Rweyemamu zilianza kusambaa juzi jioni, kabla ya jana kuthibitishwa na Rweyemamu mwenyewe juu ya kuenguliwa kwake.

Akizungumza jana, meneja huyo wa Simba alisema alipewa taarifa hizo kwa mdomo kuwa hatakuwa katika nafasi hiyo kutokana na sababu za kutomudu majukumu yake.

Rweyemamu alisema: “Ni kweli nimeambiwa kwamba sifai kuwa meneja ni taarifa kamili kwa kuwa imetoka kwa viongozi wangu ingawa hawajanipa barua kwahiyo tusubiri,”alithibitisha Rweyemamu kwa kifupi ambaye anasifika kwa misimamo mikali.

Wakati Rweyemamu akithibitisha hilo karibu mabosi wote wa klabu hiyo kuanzia juzi na jana walishindwa kuthibitisha kwa kuzungumza moja kwa moja zaidi ya habari za ndani zilizolifikia gazeti hili jana.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya sekretarieti ya klabu hiyo, zinadai kuwa wafanyakazi wawili katika idara ya habari, Ally Shatry ‘Bab Chico’ na Jacob Gamaly nao wamewekwa kando.

Kamati ya Uongozi ya Simba iliamua kukutana kutokana na mwenendo mbovu wa timu hiyo baada ya kufungwa mfululizo katika mechi mbili zilizopita.

Suala hilo linadaiwa huenda likawahusisha viongozi wengine was benchi la ufundi, ambao hatma yao imebaki katika kikao cha bodi ya wakurugenzi wa klabu hiyo.

Anayeonekana kuwa katika hatari zaidi ni kocha Sven Vandebroeck, ambaye ndiye hasa mwenye majibu ya kiwango kibovu cha soka la Simba kwasasa.

Kocha huyo amedaiwa kuwa katika migogoro ya mara kwa mara na wachezaji wake, akidaiwa pia kuamua kumpa Jonas Mkude kuvaa beji ya unahodha katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting badala ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na John Bocco aliyeingia kipindi cha pili

Hata hivyo, juhudi za gazeti hili kuwatafuta viongozi wa Simba wakiwemo makamu mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi, Salim Abdallah, Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez na mwenyekiti wa klabu hiyo, Mwina Kaduguda, ziligonga mwamba kutokana na vigogo hao kutokupokea simu wala kujibu meseji na wengine simu zao kutopatikana.

Kocha mzoefu, Mrage Kabange alisema kama sababu kubwa ya kusafisha benchi la ufundi ni vipigo katika mechi mbili mfululizo basi Simba wanakosea na wanaweza kupoteana zaidi.

“Nimesikia wamemtimua meneja na kocha wa makipa na wanajiandaa kumuondoa kocha mkuu. Sijajua sababu zilizosababisha kuwaondoa ila kama ni sababu zao za ndani na za msingi basi hatuwezi kuingilia,” alisema.

Kocha wa Pamba na winga wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe alisema haoni sababu ya Simba kutupiana lawama wakati huu baada ya kupoteza mechi mbili, kwani hata timu kubwa Ulaya zinapoteza mechi na maisha yanaendelea.

“Kinachotakiwa ni benchi la ufundi kukaa na kuangalia wapi wanakosea na wachezaji kujiongeza ili mechi zijazo wafanye vizuri. Lakini sifikirii kama ni wakati sasa wa uongozi kumfukuza kocha kwa sababu yeye anafundisha mazoezini na baada ya hapo hawezi kuingia uwanjani kuwaelekeza wachezaji namna ya kufunga”, alisema Ulimboka.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel ’Batgoal’ alisema Simba watakuwa wamemchoka kocha Sven Vandebroeck, ndiyo maana wanamtafutia sababu ya kumtimua.

“Sioni kosa la kocha kwani ni kocha mzuri na huwa anatimiza majukumu yake, lakini wachezaji ndiyo wanamuangusha kwani wanashindwa kujiongeza uwanjani kulingana na ugumu wa mechi wanazokutana nazo. Waseme tu kama wanamtafutia sababu ya kumuondoa, si vinginevyo,” alisema Gabriel.