Simba kuvaa jezi za kijivu, hali ya hewa, umbali kikwazo kambi Marekani

Muktasari:

Simba itaiwakilisha nchi katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara nyingine msimu ujao utakaoanza Agosti, baada ya msimu uliopita kutolewa katika robo fainali, watani zao Yanga pia watashiriki Ligi ya Mabingwa.

Dar es Salaam. Kama ulizoea kuwaona Simba katika jezi za rangi nyekundu na nyeupe basi msimu ujao wamekuja kivingine na jezi za rangi ya kijivu.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori alisema rangi hiyo mpya ya jezi za Simba imetokana na mabadiliko ya sheria za Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).

Alisema, CAF imetaka timu ambazo zinashiriki mashindano yao kuwa na aina tatu za jezi ambazo ni ile ya nyumbani, ugenini na nyingine ya ziada.

"Tumekuwa tukivaa jezi nyekundu na nyeupe katika mechi zetu za nyumbani na ugenini hivyo katika kanuni hiyo ya CAF, tumeongeza jezi nyingine ambayo iatakuwa ya kijivu," alisema Magori.

Simba yaanika kilichowakimbiza Marekani

Katika hatua nyingine Magori amesema hali ya hewa na umbali ndivyo vimechangia klabu hiyo kuachana na mipango ya kuweka kambi nchini Marekani au Ureno.

Awali mwekezaji wa timu hiyo, Mohamed Dewji (Mo) alieleza mipango ya kuipeleka kambini timu hiyo kwenye moja wapo ya nchi kati ya Marekani au Ureno kujiandaa na msimu mpya wa Ligi.

"Ni kweli Mo alipendekeza timu iweke kambi katika mojawapo ya nchi hizo, lakini wakati ule hatukujua kama Ligi ya Mabingwa itaanza Agosti.

"Hivyo hatukuwa na namna kwani kuipeleka timu Marekani kwa siku 17 pekee, tuliona si jambo la kiufundi bora ingekuwa kwa wiki sita.

Alisema kingine kilichowakwamisha ni hali ya hewa ya Marekani ambayo alisema haikuwa rafiki kwa wachezaji wao kwa kipindi hiki kuweka kambi huko.

"Hivyo tukalazimika kuhamishia kambi yetu Afrika Kusini," alisema Magori huku akitamba katika hoteli ambayo Simba imeweka kambi ndipo timu ya Uingereza ilipofikia wakati ikijiandaa na Kombe la Dunia 2010.

"Ni kambi nzuri na ina vifaa vya kisasa vya mazoezi, hakuna shaka vijana watu wamepata kambi bora," alisema Magori.

Alisema ikiwa Afrika Kusini, Simba itacheza mechi kadhaa za kirafiki ambazo kwa programu ya kocha wao, zitaanza Julai 23 bila kueleza watacheza na timu gani.