Ronaldo yupo mmoja tu

Sunday September 13 2020

 

TURIN, ITALIA

SUPASTAA Cristiano Ronaldo ni kielelezo hai kwamba umri ni namba tu.

Mshindi huyo mara tano wa Ballon d’Or amefanya mapinduzi ya mitazamo ya wengi juu ya wachezaji wa kulipwa baada ya kuendelea kuonyesha makali ya hali ya juu kwenye soka licha ya umri wake kuwa miaka 35.

Kucheza kwa muda mrefu, kuliwahi kufanywa na Paolo Maldini na Ryan Giggs, lakini hakuna aliyethubutu kuwa kwenye orodha ya mastaa bora kabisa waliopo tatu bora licha ya kuwa na umri mkubwa.

Wakati alipotoka Real Madrid na kwenda kujiunga na Juventus ilionekana kama ndio anakwenda kupotea kwenye soka, lakini Ronaldo amezidi kuonyesha makali ya hali ya juu kwa misimu yote miwili aliyotamba huko Serie A.

Na kama isingekuwa maajabu ya kiwango matata kabisa kutoka kwa straika Robert Lewandowski alichofanya huko Bayern Munich, basi habari zote za kuhusu mshindi wa Ballon d’Or zingekuwa zikimhusu Ronaldo. Hata hivyo, tuzo hiyo imeahirishwa na waandaaji, France Football, hivyo hata Lewandowski hatapata nafasi ya kuibeba kwa mwaka huu. Wakati ikitazamwa mafanikio yake hayo ya ndani ya uwanja kwa soka la ngazi ya klabu, Ronaldo wiki iliyopita aliandika rekodi mpya baada ya kuwa mchezaji wa pili kufikisha na kuvuka mabao 100 kwenye soka la kimataifa. Wakati ukitafakari juu ya mambo ya Ronaldo - hizi hapa rekodi 11 alizoweka tangu msimu wa 2019/20 ulipoanza.

Advertisement

1. Mzungu wa kwanza kufunga mabao 100 soka la kimataifa

Ronaldo alifunga bao lake la 100 kisha la 101 kwenye mchezo wa chama lake la kimataifa Ureno lilipokipiga na Sweden katika mikikimikiki ya UEFA Nations League. Kutokana na hilo, supastaa huyo wa Ureno amekuwa mchezaji wa kwanza wa kutoka Bara la Ulaya kufikisha idadi ya mabao yanayoanzia 100 kwenye soka la kimataifa.

2. Henry, Van Persie wote wamefunikwa

Kwa idadi yake ya mabao Ronaldo kwenye soka la kimataifa, unaweza kuchanganya wafungaji wa muda wote wa mataifa matata kwenye soka, Ufaransa na Uholanzi ukachanganya pamoja nab ado hawamfikii Mreno huyo. Ronaldo hadi sasa amefunga mabao 101 kwenye soka la kimataifa, sawa na kujumlisha mabao ya wakali wawili moto kabisa, kinara wa mabao wa Ufaransa, Thierry Henry na kinara wa Uholanzi, Robin van Persie. Henry amefunga 51 na Van Persie mabao 50.

3. Mabao mengi kuliko wa pili na wa tatu Ureno

Hakuna kitu kinachompa thamani kubwa Ronaldo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Ureno kama mabao yake, ambayo ukichukua wachezaji wawili wanaomfuatia kwa mabao, ukijumlisha mabao yao yote waliyofunga hayamfikii fowadi huyo wa Juventus. Anayeshika namba mbili kwa mabao Ureno ni Pauleta, amefunga 47 na namba tatu Eusebio ni 41, hivyo mabao yao yote ukijumlisha unapata 88, ambayo yapo nyuma kwa mabao 13 kutoka idadi aliyofunga Ronaldo peke yake.

4. Bado mabao manane tu kuweka rekodi duniani

Kwa mabao yake 101 aliyofunga kwenye soka la kimataifa, Ronaldo amezidiwa mabao manane tu kufikia rekodi ya mchezaji mwenye mabao mengi zaidi kwenye soka la kimataifa. Kama atafunga mara tisa, basi atakuwa mchezaji namba moja duniani kufunga mabao mengi kwenye soka la kimataifa. Kwa sasa mchezaji anayeshikilia rekodi ya kuwa kinara wa muda wote wa mabao kwenye soka la kimataifa duniani ni straika wa Iran, Ali Daei, aliyefunga 109.

5. Mabao 49 katika mechi 47 za mwisho Ureno

Katika kitu ambacho Ronaldo amekuwa akikifanya kwa ufasaha zaidi anapokuwa uwanjani basi ni kuhakikisha mipira inatinga kwenye nyavu za wapinzani. Staa huyo alionyesha kuwa yeye ni moto baada ya kufunga mabao 49 katika mechi 47 za mwisho alizoitumikia Ureno, huku akiwa mchezaji pekee aliyepiga mabao mawilimawili katika mechi nyingi kuliko wenzake kwenye kikosi cha Ureno. Ronaldo amepiga mbilimbili mara 24 zaidi.

6. Afikisha mabao 700 kwenye soka

Jina la Ronaldo litakuwa kwenye kumbukumbu matata kabisa katika dunia ya mchezo wa soka. Mabao yake aliyofunga yamemfanya Mreno huyo kuingia kwenye anga za magwiji kama Romario, Gerd Muller, Josef Bican, Ferenc Puskas na wa hivi karibuni Lionel Messi, ambaye aliweka jina lake kwenye historia ya wababe waliofikisha mabao 700 kwenye maisha yao ya soka alipofikisha idadi hiyo Oktoba mwaka jana. Ndani ya msimu wa soka wa 2019/20 – Ronaldo amefanya mambo mengi makubwa yanayomfanya kuzidi kuwa juu milele.

7. Mabao mengi zaidi kwa msimu mmoja Juventus

Ndio hivyo. Licha ya kuwa na umri wa miaka 35, Ronaldo hakuwa na shida kabisa kwenye hilo, akifunga mabao 35 ndani ya msimu mmoja akiwa anaitumikia Juventus na hivyo kufikia rekodi ya Ferenc Hirzer aliyoweka katika msimu wa 1925-26, ambayo imedumu karibu karne moja sasa. Staa Ronaldo amepangua rekodi hiyo kongwe akiwa na umri mkubwa tofauti na wengi ambavyo walidhani kwamba unahitaji kuwa kijana na mwenye uchu wa kufunga kufikia rekodi hiyo.

8. Mchezaji mkubwa kufunga mabao 30 kwa msimu ligi tano za Ulaya

Ile tafsiri ya umri ni namba tu ndo hii. Ronaldo aliweka rekodi ya mabao 30 ndani ya msimu mmoja akiwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi katika Ligi Kuu tano bora za Ulaya ambazo ni La Liga, Ligi Kuu England, Bundesliga, Serie A na Ligue 1. Akiwa na miaka 35 na siku 166, alipangua rekodi iliyodumu iaka mingi iliyowekwa 1947-48 na straika wa zamani wa Arsenal, Ronnie Rooke – alifikisha idadi kubwa ya mabao akiwa na umri huo mkubwa.

9. Mchezaji aliyetumia mechi chache kufunga mabao 50 Serie A

Ronaldo alifikisha idadi hiyo ya mabao 50 kwenye mikikimikiki ya Serie A baada ya kucheza mechi 61. Staa huyo wa Ureno alitua kwenye kikosi cha Juventus na kuwaonyesha mastaa wanaokipiga kwenye Serie A jinsi mabao yanavyofungwa ambapo alihitaji mechi 61 tu kufikisha nusu karne ya mabao. Kwa kitendo hicho amevunja rekodi iliyokuwa imewekwa na straika Andriy Shevchenko, ambapo Ronaldo amefikisha idadi hiyo ya mabao kwa mechi saba nyuma.

10. Wakwanza kufunga mabao 50 ya ligi, England, Hispania na Italia

Hii inajieleza yenyewe kuhusu ubora wa mchezaji huyo kwenye mchezo wa soka na linapokuja suala la kuweka mipira kwenye nyavu za magoli ya wapinzani. Ronaldo amekuwa mchezaji wa kwanza kufunga zaidi ya mabao 50 kwenye Ligi Kuu Tatu kubwa Ulaya, Ligi Kuu England, La Liga na Serie. Staa huyo alifunga mabao 84 kwenye mechi za ligi alizocheza huko England, wakati Hispania kwenye mikikimikiki ya La Liga alifunga mabao 311 na alipotua Italia, alifunga mabao 52 kwenye Serie A.

11. Tarakimu mbili ya mabao kwa misimu 15 mfululizo

Asikwambie mtu, Ronaldo ameonyesha ni balaa kubwa anapokuwa ndani ya uwanja na hilo linakuonyesha kwamba unakuwa na uhakika wa timu kufunga mabao ya kutosha tu anapokuwa uwanjani. Kwa kuanzia msimu wa 2004/05, ambapo ulikuwa msimu wa pili kwake Man United, ambapo ndio ilikuwa mara ya mwisho kwa Mreno huyo kushindwa kufikisha walau mabao 10 kwa msimu mmoja. Zaidi ya hapo, Ronaldo amefunga idadi ya mabao yanayoanzia 10 na kuendelea kwa misimu 15 mfululizo.

Advertisement