Rekodi za maisha ndani ya EPL

BAADA ya Ligi Kuu England kumalizika juzi Jumapili Julai 26, habari kubwa iliyoibuka ni kwenye rekodi ambazo zimewekwa na wachezaji, timu  na hata makocha, Mwanaspoti Online inakuletea baadhi ya rekodi muhimu zilizowekwa.

David Luiz

Beki wa Arsenal, David Luiz ameweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyefanya makosa mengi yaliyosababisha penalti, kwa kufanya hivyo mara tano. Hakuna mchezaji ambaye amefanya mara nyingi zaidi yake.

Kevin De Bruyne

Kiungo wa Manchester City, Kevin De Bruyne ameweka rekodi ya kuhusika katika mabao 100 ya Ligi Kuu katika mechi 155 alizocheza, akifunga mabao 35 na kutoa asisti 65.

Pia msimu huu ameweka rekodi ya kutoa asisti 20, ambazo zinamfanya kufikia rekodi ya Thierry Henry aliyefanya hivyo msimu wa 2002/03. 

Kwa msimu huu ameweka rekodi ya kuhusika kwenye mabao 33 ya City akiwa ametoa asisti 20 na kufunga mabao 13, anakuwa kiungo wa pili wa kati kuhusika kwenye mabao mengi ndani ya EPL nyuma ya Lampard ambaye alihusika kwenye mabao 36, akiwa amefunga mabao 22, na kutoa asisti 14 msimu wa 2009/10.

Tokea msimu wa 2012/13, Kevin De Bruyne amekuwa mchezaji wa pili kwenye ligi tano bora barani Ulaya kutoa asisti nyingi zaidi nyuma ya Lionel Messi, yeye akiwa ametoa asisti 100 na Messi 112.

Mount kama Lampard 

Mason Mount amekuwa mchezaji wa kwanza raia wa England kuifungia Chelsea bao la faulo, tokea afanye hivyo kocha wa sasa wa timu hiyo Frank Lampard.

Giroud kikongwe tishio

Akiwa na umri wa miaka 33, Olivier Giroud anakuwa mchezaji wa kwanza mzee zaidi kufunga mabao katika mechi tano mfululizo, akimpita Jemie

Vardy ambaye ana umri wa miaka 32. Hakuna mchezaji mwenye miaka hiyo aliyewahi kufunga katika mechi tano mfululizo.

 

Manchester United

Katika mchezo wa mwisho dhidi ya Leicester, Manchester United imeweka rekodi ya kupata penalti 14 ndani ya EPL kwa msimu huu, hiyo inakuwa ni  mara ya kwanza ndani ya ligi hiyo timu kupata penalti nyingi zaidi kwa msimu mmoja.

Raheem Sterling

Fundi wa Manchester City Raheem Sterling amefunga mabao 20 msimu huu kwenye mashindano yote jambo lililomfanya kuwa mchezaji wa pili raia mwenye uraia wa England kuifungia City idadi hiyo ya mabao nyuma ya Brian Kidd ambaye alifunga mabao 21, katika msimu wa  1976/77.

Jemie Vardy

Amekuwa mchezaji wa kwanza mwenye umri mkubwa kuwahi kushinda kiatu cha dhahabu ndani ya EPL akiwa na umri wa miaka 33, akivunja rekodi ya Didier Drogba ambaye alifunga mabao 29, msimu wa 2009/10 huku akiwa na umri wa miaka 32

Watford na Bournemouth

Imeshuka kwa mara ya tatu ndani ya EPL kwenda Championship, mara ya kwanza kushuka ikiwa ni msimu wa 1990/20 na msimu wa 2006/07.

Bournemouth imetolewa Ligi Kuu kwa mara ya kwanza baada ya kucheza kwa msimu tano mfululizo.