Ratiba yaziweza mkao wa kula, klabu Ligi Kuu

Muktasari:

  •  Jana, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli alitangaza kuruhusu shughuli za michezo kuendelea nchini kuanzia Juni Mosi mwaka huu baada ya kusimamishwa mnamo Machi 17 ikiwa ni hatua za kukabiliana na virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid19.

Muda wowote kuanzia sasa, ratiba ya Ligi Kuu Bara inaweza kutolewa na namna gani ambavyo inaweza kurejea na kuendelea kuchezwa kama ilivyokuwa hapo awali.

Wakizungumza na Mwanaspoti Online kwa nyakati tofauti, makocha na maofisa wa klabu mbalimbali nchini wamesema kuwa kuendelea kwa programu zao za maandalizi, kutategemeana na ratiba na muongozi watakaopata kutoka katika mamlaka zinazosimamia soka na zile za serikali.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema wao bado hawajaanza jambo lolote hadi watakapopata maelekezo hayo kutoka kwa mamlaka husika.

"Kwetu Simba baada ya kupata ratiba na mazingatio ya kiafya tutafanya kama ipasavyo ili kuishi katika mazingira sahihi na tatizo hili ambalo tunaendelea kujikinga nalo," amesema.

"Kwa maana hiyo kuanzia ndani ya timu, kambini, na mahala popote pale ambalo tutakuwa pamoja mbali ya kuwepo na taratibu zetu kama klabu lakini tunaendelea kujikinga na kufuata kauli za mamlaka husika kama ambavyo tulielekezwa," amesema Rweyemamu.

Ofisa habari wa KMC, Anuary Binde umesema wao tayari wameanza mazoezi tena kwa kufata taratibu zote za kujikinga ambazo zinatolewa na mamlaka husika wakati wote.

"Kwetu tumeanza maandalizi lakini kuanzia katika kambi tunaishi kwa nafasi kila mchezaji na chumba chake, hatuna mikusanyiko, hakuna kuruhusu wachezaji kutoka nje na mambo mengine ya msingi," amesema.

"Tumepokea kwa furaha taarifa hii ya kurejea kwa ligi ndio maana tumeanza maandalizi kwa kuzingatia taratibu zote ambazo wataalamu wa kiafya hutuelekeza," amesema Binde.

Kocha wa Coastal Union, Juma Mgunda anasema baada ya kupokea kauli hiyo ya kurejea kwa ligi kwa upande wao hawajaanza kufanya jambo lolote mpaka hapo watakapo fahamu itarudi kwa namna gani.

Mgunda alisema tayari kama kocha yupo na mipango yake ya kiufundi ambayo amepanga kuanza nayo ila hilo halitawezekana hadi hapo ambapo watakapofahamu kila kitu.

"Tunafahamu tumepewa ruhusa ya ligi kurejea lakini bado hatujui itarejea kwa namna gani, ratiba itakuwa vipi na wakati gani tutaanza kucheza," anasema.

"Baada ya kupata hivyo vyote ndio tutaeleza tutafanya mazoezi kwa namna ipi, wapi kwa maana ya uwanjani wenye mazingira yapi, na ambavyo tutaishi kama wachezaji watakuwa kambini au kila mchezaji atatoka nyumbani kwake," anasema Mgunda.