Rais Magufuli ampa shavu Beka Flavour Moro

Muktasari:

  • Beka Flavour ni msanii pekee aliyepata nafasi ya kutumbuiza jana katika shughuli maalum ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.John Magufuli ya ukaguzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge) Kilosa Mkoani Morogoro

MSANII wa muziki wa kizazi kipya Beka Flavour ameshukuru kupata nafasi ya kipekee katika shughuli kubwa ya ukaguzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge) iliyoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John  Magufuli jana huko Kilosa,Morogoro.

Beka Flavour mmoja wa wasanii wanaofanya vizuri katika muziki huo akitamba na nyimbo kama Kibenten na Siachani Naye akiibukia katika kundi la Yamoto Band lililokuwa linaongozwa na Said Fella.

 Akizungumza na Mwanaspoti , Beka amesema kupata fursa hiyo ni jambo kubwa na la kihistoria katika maisha yake ya kimuziki, kwani fursa hiyo ameipata yeye licha ya uwepo wa kundi kubwa la wasanii nchini

Anasema walikuwepo wasanii watatu katika tukio hilo yeye na wengine wawili ambao ni chipukizi lakini kutokana na muda wa Rais ikatakiwa apande msanii mmoja na ndipo nafasi hiyo akaipata yeye.

"Kwangu mimi ni jambo kubwa sana, kuimba mbele ya Rais kwani wasanii tuko wengi ambao tumetunga nyimbo za kumpongeza mheshimiwa Rais lakini nafasi nikaipata mimi ni jambo kubwa na la kumshukuru Mungu,"

Aidha Beka anasema hiyo  inamfanya azidi kuumiza kichwa kufanya vitu vikubwa zaidi ambavyo vitamfanya azidi kuaminika na kukubalika kwa rika zote.

Anasema ni furaha kwa msanii kuimba alafu watu wakubwa na mashuhuri kama Rais, Waziri Mkuu na wengineo wakafurahia kinachoimbwa huku akikiri kwake ni deni kubwa ili azidi kuwafurahisha atakapopata nafasi tena kama hiyo.

Rais jana alikagua reli ya kisasa katika maeneo ya Kilosa Morogoro shughuli iliyoudhuliwa na watu, mbalimbali.