Nyoni asisitiza ushindi Stars lazima

Muktasari:

Baada ya Taifa Stas kushindwa kupata ushindi nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa, imejipa matumaini kuhakikisha wanakwenda kuwafunga Wakenya kwao.

LICHA  ya Stars kutojitengenezea mazingira mazuri ya ushindi nyumbani dhidi ya Kenya, iliocheza nayo hivi karibuni Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kiraka Erasto Nyoni amesema matokeo hayo hajawakatisha tamaa kupigania ushindi ugenini.
Stars itarudiana na Kenya Agosti 4, jambo ambalo Nyoni anaamini watapata ushindi ugenini kwa madai kwamba tayari wanajua wapinzani wao ni wa aina gani.
Anasema ni nafasi kwao kuonyesha ushindani kwenye michuano ya CHAN, akidai inatoa taswira ya uwezo wao kama wachezaji wa ndani Afrika, hivyo anasisitiza kwamba Watanzania waendelee kuwaunga mkono kwamba bado wana nafasi ya kufanya vyema.
"Michuano hii ina maana kubwa kwetu wachezaji wa ndani Afrika, inapima uwezo wetu hivyo kila mchezaji akitambua hilo atapambana kwa kadri awezavyo ili kuonyesha thamani yake mbele ya nchi yake.
"Pamoja na hilo inaweza ikawapa nafasi chipukizi kuonekana na mataifa mengine ya kufanya nayo kazi kwa timu ambazo tunapambana nazo kwenye michuano hii, kila mchezaji ajitume kwa kadri anavyoweza atafika pale anapopataka.
"Jambo lingine Watanzania wanapenda timu yao, lazima tuendelee kupambana kuhakikisha bendera ya taifa letu inapepea kwa ushindi, tunapokutana na nchini nyingine basi sisi ni askali wa Tanzania kuona inakuwa mfano dhidi yao,"anasema.