Kwako Kashasha: Usajili wa Bongo ni ‘Try And Error’

Saturday January 18 2020

Mwanaspoti-Tanzania-Usajili-Bongo-Try And Error-Kichuya-Niyonzima-Mwanasport-Yanga-Simba SC-Azam

 

By Mwalimu Kashasha

IKIWA dirisha dogo la usajili likiwa limefungwa Januari 15, klabu za Simba, Yanga na Azam zimeshika ukubwa wa usajili kutokana na majina ya wachezaji wao waliowasajili.
Usajili huu unakuwa ni mahususi kwa ajili ya kuziba mashimo ambayo yameonekana katika baadhi ya michezo hivyo benchi la ufundi huwa wanaangalia sehemu chache ili kupata wachezaji wengine.
Kwa upande wa Ulaya huko wakati timu zao zikicheza huwa kuna mtu anaangalia namna timu inavyocheza kwa kila mchezaji (Perfomance Circle) huyu anakuwa anafanya uchambuzi wa kila mchezaji lakini pia anaweka data ili kujua namna ambavyo dakika alizocheza na vitu vingine.
Kwa yule ambaye anaonekana ana shida kidogo basi anapewa mazoezi maalumu ili kufikia pale wanapopataka, pia kuna mwingine ambaye anakuwa anafatilia wachezaji wanaokuja (wanaotakiwa) ili kujua sehemu gani ya kuanzia.
Nyumbani hapa imekuwa ni kama Try and Error (Kujallibu na kukosa) kwasababu hatuna watu maalum ambao wanakusanya data za wachezaji ambao tunawatafuta na wanapokuja hapa wanashindwa kuonyesha mwishowe wanaondoka.
Simba waliwaleta Wabrazil lakini tumeona hawapati nafasi katika kikosi cha kwanza, huku yule Wilker Da Silva akiachwa. Sidhani kama ufatiliaji ulikuwa mzuri kwake na hayo ndiyo makosa yenyewe.
Usajili unaofanyika ni mbwembwe tu. Kwa mfano huyu mchezaji Luis wa UD Songo tayari alikuwa anakuja Tanzania kwa ajili ya Yanga lakini ghafla kisa pesa akaenda Simba, sio kwamba ni mchezaji mbaya, kwa sababu uwezo wake ni mzuri na akizoea mazingira anaweza akawa bora, lakini mahitaji yalikuwepo kwa kocha mwenyewe?
Hata usajili wa Shiza Kichuya una mambo matatu ndani yake kwani sio jambo dogo yeye kurejea Tanzania wakati tayari alishaanza kufungua njia za kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.
Jambo la kwanza kujiuliza kwa Kichuya huko alipokuwepo alichokwa? Jambo la pili sasa hivi yupo katika hali gani, kama alikuwa hachezi ni tatizo kubwa, sielewi kwa kiwango gani atamshawishi mwalimu.
Jambo la tatu Kichuya anaweza akawa amerejeshwa Simba na kusaini mkataba kwa sababu tu ni mtoto wa nyumbani, amecheza kwa kiwango kikubwa mpaka anaondoka lakini sasahivi atakuwa na changamoto kwa sababu wanaocheza namba ile Hassan Dilunga na Deo Kanda wote wapo katika kiwango kizuri.
Ukija kwa upande wa Azam kwenye dirisha hili dogo unaona kabisa wamefanya usajili kwa kufuata mapendekezo ya kocha, wamesajili wachezaji wawili tu katika eneo ambalo wao wenyewe wameona wanahitaji nguvu.
Pia kwa usajili huu ni rahisi kukopi na wenzao tofauti kama wangekuwa wamesajili wachezaji wengi kwani ingewasumbua hata benchi la ufundi kuhakikisha wachezaji wanaingia haraka katika mfumo.
Mapacha wa Simba hapa nawazungumzia Yanga, wao wana kazi kubwa ya kufanya kwa  kumalizia raundi zinazokuja kwa sababu wamebadili kocha wakati ambao nasema unaweza ukawa sio sahihi.
Kocha huyu mpaka aje kuzoea mazingira, presha za mashabiki inaweza ikamchukua muda kidogo lakini pia hata wachezaji wao ambao wamewachukua nao ni tatizo hasa katika eneo la ushambuliaji wana wachezaji takribani watano ambao wote ni wapya.
Vilevile pia tatizo lingine ni katika utafutaji wa wachezaji, inashangaza mtu kama Yikpe Gnamien haaminiwi katika kikosi hiko, kama haaminiwi kwa kucheza dakika 90 inamaanisha kuna jambo.
Haruna Niyonzima amerejea na moja kwa moja ameingia katika kikosi cha kwanza inatokana na uzoefu wake wa soka la Bongo, Mkwasa amemzoea kwahiyo ni jambo la kawaida kwake.
Uwezo wake haujapungua sana kwani anajua namna ya kuchanganya miguu yake na kuwafanya mashabiki wa Bongo kulitaja jina lake wanapokuwa wapo majukwaani.
Naweza kusema usajili wa Bongo ni Try and Error kwa sababu wachezaji wetu wanasajiliwa kwa mbwembwe lakini baada ya muda mfupi wanaondoka.

Advertisement