Mbeya City yaipiga Polisi Tanzania kwa penalti yatinga 16 bora

Muktasari:

Wafungaji wa penalti wa Mbeya City walikuwa Rolland Msonjo, Ibrahimu Nduguli, Rehani Kibingu wakati wenyeji Polisi mfungaji pekee akiwa Sixtus Sabilo.

Arusha.Mbeya City imetangulia hatua ya 16 bora ya Kombe la FA baada ya kuifunga Polisi Tanzania kwa penalti 3-1 baada ya kumaliza kwa sare bao 1-1 katika dakika 90 za mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Ushirika, Moshi.

Wafungaji wa penalti wa Mbeya City walikuwa Rolland Msonjo, Ibrahimu Nduguli, Rehani Kibingu wakati wenyeji Polisi mfungaji pekee alikuwa Sixtus Sabilo.

Huku waliokosa kwa Polisi Tanzania, Marcel Kaheza, Hassan Maulid na Shabani Stambuli na kuzima ndoto ya mafaande hao kusonga mbele katika mchezo huo.

Katika mchezo huo Polisi Tanzania ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia Mohammed Mkopi katika kipindi cha kwanza kabla ya Mbeya City kusawazisha katika dakika 57 kupitia Rehani Kibingu.

Mbeya City inayofundishwa na kocha Amri Saidi ilibadilika kipindi cha pili baada ya kufanya mabadiliko mawili ya haraka haraka dakika ya 47 kwa kumtoa Samson Madekele na kuingia Rolland Msonjo pia kumtoa Abdul Sulemani na kuingia Kibingu.

Kibingu alipokea pasi Peter Manyika katika dakika ya 57, na kupiga shuti kali lililomshinda kipa Polisi Tanzania, Peter Manyika na kujaa wavuni.

Baada ya bao hilo Polisi Tanzania ilifanya mabadiliko ya kuwaingiza Erick Msagati na kumtoa Mohammed Mkopi dakika 78 na dakika ya 88 aliingia Baraka Majogoro kuchukua nafasi ya Pato Ngonyani, lakini haijazaa matunda hadi dakika 90 zinamalizika matokeo yalikuwa 1-1 ndipo penalti zilipotumika kuamua bingwa.