Klopp anavyoongoza makocha wengine kwa kutoa vichapo

Tuesday January 14 2020

Mwanaspoti-Klopp-Liverpool-Mwanasport-Michezo-Michezo blog-anavyoongoza-makocha wengine-kutoa-vichapo

 

LIVERPOOL, ENGLAND. JOSE Mourinho na Tottenham Hotspur yake chali, kuna mwingine? Liverpool imeamua kila anayekuja mbele yake ni kichapo tu.
Kila wakiingia uwanjani, Jurgen Klopp na jeshi lake wanazidi kuandika rekodi, inaonekana wazi kuwa Liverpool wana jambo lao na hakuna wa kuwazuia.
Awali, watu waliamini ilikuwa nguvu ya soda, lakini sasa kila anayepewa dhamana ya kuizuia Liverpool anakutana na kipigo, huku ubingwa wa Ligi Kuu England ukizidi kunukia Anfield.
Kadiri wanavyozidi kutoa dozi ndivyo rekodi mpya zinaandikwa kwenye soka la England na Ulaya kwa ujumla.
Ushindi wa juzi wa bao 1-0 dhidi ya Spurs umewapa rekodi nyingine, safari hii wameingia kwenye vitabu vya historia kama timu iliyokuwa na mwanzo mzuri zaidi katika ligi tano bora baada ya mechi 21.
Awali timu ambayo ilikuwa na mwanzo mzuri zaidi baada ya mechi 21, ilifanikiwa kuvuna pointi 59, lakini Liverpool imevuna pointi 61, kitu ambacho hakijawahi kutokea katika Ligi tano bora za Ulaya.

Chelsea – Mechi 21, Pointi 58
Baada ya kuipa Porto ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2004, Jose Mourinho alitua Chelsea na kutengeneza timu moja ya rekodi ya kibabe sana, huku akifanikiwa kubeba taji katika msimu wa 2004-05 ambao ndio ulikuwa wa kwanza kwake Stamford Bridge.
Aliendeleza ubabe wake katika msimu wake wa pili Chelsea, baada ya kufanikiwa kuvuna pointi 58 katika mechi 21, akishinda mechi 19, kutoka sare moja dhidi ya Everton na kufungwa moja na Manchester United.
Baada ya kuanza vizuri msimu wa 2005-06, Mourinho alifanikiwa kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu England akiwa na kikosi kilichokuwa na staa kama Frank Lampard na Didier Drogba.

Barcelona – Mechi 21, Pointi 58
Barcelona haikuanza vizuri sana msimu wa 2010-11, kwa sababu ilipoteza mechi ya pili tu ya msimu baada ya kupigwa mabao 2-0 nyumbani na Hercules, lakini baada ya mechi hiyo iliwasha moto wa kutisha.
Ikiwa chini ya Kocha Pep Guardiola, Barca ilifanikiwa kushinda 19 kati ya 21, huku ikifungwa mechi moja na kutoka sare mechi moja huku ikifanikiwa kutwaa taji la La Liga mwisho wa msimu.
Katika msimu huo utatu wa Xavi Hernandez, Andres Iniesta na Lionel Messi ulizitesa timu ambazo zilipita mbele ya Barcelona na kutawala soka la Hispania.

Barcelona - Mechi 21, Pointi 58
Msimu wa 2012-13, Barcelona ikiwa chini ya Hayati Tito Valenova aliyerithi mikoba ya Pep Guardiola, ilianza msimu ikiwa kwenye kiwango cha hali ya juu na kutoa dozi kwa kila timu iliyokuja mbele yao.
Hadi inacheza mechi ya 21 ya La Liga, timu hiyo ilikuwa imekusanya jumla ya pointi 58, baada ya kushinda mechi 19, kutoka sare moja dhidi ya Real Madrid na kufungwa moja na Real Sociedad, hivyo kupoteza pointi tano tu kati ya 63 ambazo wangekuwa nazo kama wangeshinda mechi zao zote.
Barcelona ilifanikiwa kutwaa taji mwisho wa msimu baada ya kushinda mechi 32, kutoka sare nne na kufungwa mbili, kati ya mechi 38 za msimu huo.

Bayern Munich,
Mechi 21, Pointi 59
Baada ya kupumzika kufundisha soka kwa kipindi cha mwaka mmoja, 2013, Guardiola alirudi tena kwenye soka, lakini safari hii akatua Bayern Munich na kuendelea alipoishia wakati akiwa na Barcelona.
Guardiola alifanikiwa kuitawala Bundesliga katika msimu wake wa kwanza tu na ilikuwa katika msimu huu wa 2013-14 ambao aliiongoza Bayern Munich kushinda mechi 19 kati ya 21 za kwanza za ligi hiyo.
Katika msimu huo Bayern Munich ilipata sare mbili tu kati ya mechi 21 ya kwanza na kuvuna pointi 59 kati ya 63 ambazo walitakiwa kuzipata na ndiyo maana haikuwa ajabu kwao kuchukua ubingwa mwisho wa msimu.

Manchester City –
Mechi 21, Pointi 59
Hii ni kawaida ya Guardiola pale anapofanikiwa kusuka timu anayoitaka, ndiyo maana baada ya kuwa na msimu mbovu wa 2016-17, Pep aliingia msimu wake wa pili England akiwa amejipanga.
Katika msimu wa 2017-18, Guardiola alifanikiwa kutengeneza kikosi bora cha Man City na kufanikiwa kutwaa taji lake la kwanza la Ligi Kuu England baada ya kuuanza kwa kasi kubwa sana msimu huo.
Guardiola alitoa sare mechi mbili tu kati ya 21 za kwanza akishinda 19 na kuvuna jumla ya pointi 59 na huku akifanikiwa kuondoka na taji la England msimu huo.

Juventus – Mechi 21,
Pointi 59
Hii ilikuwa Juventus yenye Massimiliano Allegri kwenye benchi lake la ufundi huku Cristiano Ronaldo akiongoza mashambulizi, huu ulikuwa msimu wa 2018-19 ambapo timu hiyo ilifanikiwa kuvuna pointi 59 katika mechi 21.
Katika mechi 21 za kwanza Juventus ilitoa sare mbili tu, ikiwemo ile ya 1-1 nyumbani dhidi ya Genoa na ile ya 2-2 dhidi ya Atalanta ugenini, lakini mechi nyingine zote walitoa dozi. Ulikuwa katika msimu huu ambapo Ronaldo alitwaa taji lake la kwanza Serie A baada ya kutua Juventus akitokea Real Madrid.

Liverpool – Mechi 21, Pointi 61
Hakuna timu imewahi kuuanza msimu kwa kiwango hiki cha Liverpool miongoni mwa ligi tano bora za Ulaya na sasa Klopp na jeshi lake linaonekana limepania kupeleka taji la Ligi Kuu England Anfield msimu huu.
Manchester United pekee ndiyo imefanikiwa kuizuia Liverpool kubeba pointi tatu kwenye mechi ya Ligi Kuu Msimu huu ambapo katika mechi 21, Liver imeshinda 20 na kutoka sare moja tu msimu huu wa 2019-2020.
Ushindi wa juzi dhidi ya Spurs ndiyo imeifanya timu hiyo kuandika historia hii ya kipekee katika ligi tano bora za Ulaya na kuna kila dalili Liver itaendelea kuandika historia kila kukicha.

Advertisement