Mwanamuziki Aurlus Mabele afariki dunia kwa ugonjwa wa corona

Friday March 20 2020

 

 

Dar es Salaam. Mwanamuziki wa miondoko ya Soukous Aurlus Mabele amefariki dunia nchini Ufaransa akiwa na miaka 67.

Kwa mujibu wa rafiki yake wa karibu Nyboma Mwandido amethibitisha Aurlus Mabele kufariki dunia, huku taarifa zikieleza kuwa nguli huyo wa miondoko ya Soukous alifariki usiku wa kuamkia Ijumaa Machi 20, 2020 baada ya kuugua ugonjwa wa kiharusi kwa muda mrefu na hivi karibunia alipata maambukizi ya virusi vya corona.

Taarifa zaidi zimeeleza kuwa mwanamuziki huyo pia alikuwa akisumbuliwa kwa ugonjwa wa saratani ya koo, kwa miaka mingi, kabla ya kupata maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa corona.

Ugonjwa huo ambao ulianzia Wuhan nchini China na kusambaa katika nchi mbalimbali duniani, umeua zaidi ya watu 371 nchini Ufaransa.

Aurlus Mabele Alizaliwa mnamo mwaka wa 1953 huko Kongo-Brazzaville katika wilaya ya Poto-Poto nchini Jamhuri ya Kongo alifariki tarehe 20 March 2020.

Advertisement

Jina lake halisi ni Aurélien Miatsonama. Alianzisha kundi liitwalo "Ndimbola Lokole".

Mabele alikuwa mmoja ya waanzilishi na lijendi aliyewahi kuanzisha kundi la Loketo akiwa na wanamuziki wenzake nguli kama Mav Cacharel na Diblo Dibala miaka ya 1980 japo baadae kundi lao lilivunjika.

Mabele akiwa na Mav Cacharel na Diblo Dibala walitengeneza muziki maarufu wa soukous ambapo baadaye akatajwa kama mfalme, na kupelekea msemo wa kuwa "Aurlus Mabele ndiye mfalme wa soukous".

Mabele alikuwa ni msanii pekee aliyeweka makazi yake jijini Paris Ufaransa na kutamba katika miaka ya 1980 akitumia santuri.

Mabele pia aliwahi kutamba na nyimbo zake maarufu kama Embargo, Liste Rouge.

Katika miaka 25 ya kazi zake ameuza zaidi ya nakala milioni 10 za albamu dunia nzima na alisaidia kwa kiasi kikubwa katika kuitambulisha na kuisukuma vilivyo muziki wa soukous nje ya mipaka ya bara la Afrika.

Alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa kupooza kwa miaka mitano, lakini aliweza kujipanga ili kufanya matamasha na kundi zima la Loketo huko Ulaya kati ya mwezi Mei na Juni, 2009.

Kwa kushirikiana na wapiga magitaa maarufu na wenye vipaji, alitengeneza dansi ya Kiafrika yenye ladha yake ya kipekee ya soukous kwa kutunga nyimbo kama vile Mousso Africa, Ivorian woman, Embargo, Betty De Asta, Evelyne, Loketo na kadhalika.

Advertisement