Mwalala apasua mbarika

Wednesday June 5 2019

 

By Thomas Matiko

KOCHA wa Bandari FC, Bernard Mwalala amefunguka kutokana na kutimiza ndoto yake ya kujikatia tiketi ya kushiriki dimba la CAF Confederation Cup msimu ujao.

Baada ya kushindwa kukimbizana na Gor Mahia kwenye ubingwa wa Ligi Kuu ya KPL, Mwalala alikata tamaa zikiwa zimesalia takriban mechi 10 hivi na kuelekeza nguvu zake katika kulitwaa  kombe la GOTV Shield Cup.

Mwalala aliishi kusisitiza lengo lake msimu huu ilikuwa ni kuhakikisha anavuka na kombe hilo baada ya kulemewa kwenye ligi na mabingwa Gor huku vijana wake wakimaliza katika nafasi ya pili.

Alipambana na kufika fainali alikokutana na Kariobangi Sharks na kufanikiwa kuvuna ushindi mnene wa mabao 3-1 kwenye mechi hiyo iliyochezwa kwa siku mbili Jumamosi na Jumapili, wikendi iliyopita.

Mchuano huo uliratibiwa kuchezwa Jumamosi na ulianza saa kumi jioni na hadi kumalizika  kwa kipindi cha kwanza Bandari walikuwa wakiongoza kwa mabao 2-1.

Mechi hiyo haikuendelea kutokana na mvua kali hivyo iliahirishwa hadi Jumapili na kipindi cha pili kilichezwa na Bandari wakafanikiwa kuongeza bao lingine.  Baada ya ushindi huo ambao ulikuwa ni ulipizaji kisasi dhidi ya Sharks waliowalima 1-0 kwenye fainali ya Sportpesa Cup mapema mwaka huu, Mwalala kafunguka.

Advertisement

“Kwa sasa sitazungumzia mipango yetu kuelekea dimba la kitaifa lililo mbele yetu. Kikubwa ni kuwashukuru wachezaji, menejimenti kwa kujitahidi sana hadi tumefikia  levo hizi. Kikweli nimefurahia sababu huu ni ushindi wangu mkubwa kati ya zinginezo,” alisema.

Kando na kuliwakilisha taifa kwenye CAF Confederation msimu ujao, pia Bandari walizawadiwa na Sh2 millioni na kupokea nyongeza nyingine ya Sh1 milioni kutoka kwa wadhamini wao Kenya Ports Authority (KPA).

Mara ya mwisho kwa Bandari kubeba taji hili ni 2015.

Ushindi huu unajiri kipindi meneja Mkuregenzi wa KPA Daniel Manduku alitangaza kuwa wachezaji na benchi wataongezewa mishahara yao na pia kuwasafirisha hadi Afrika Kusini kwa kambi ya mazoezi ya wiki moja kwenye matayarisho ya msimu ujao.

Advertisement