Mwakinyo afuata nyayo za Cheka

Muktasari:

Akizungumzia mazoezi hayo, Mwakinyo alisema amekuwa akijifua mara tatu kila siku ikiwamo ya kunyanyua vitu vizito, mazoezi ya kasi ya mikono, kupiga begi na padi, na kukimbia akiwa anaendesha tairi la trekta katika maeneo ya milima.

Dar es Salaam. Bondia Hassan Mwakinyo ameanza kutumia mbinu kama alizowahi kutumia bingwa wa zamani wa dunia wa WBF, Francis Cheka mazoezini ili kujiweka fiti kuelekea pambano lake la Oktoba 26.

Mwakinyo atacheza kwa mara ya kwanza kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikiwa ni miezi 10 tangu alipoweka rekodi ya kumchapa kwa Technical Knock Out (TKO) aliyekuwa bondia namba nane wa dunia kwenye uzani wa super welter, Samm Eggington pambano lililoacha mshtuko nchini Uingereza.

Tayari bondia huyo ameanza mazoezi makali ikiwamo ya gym, kuzichapa ana kwa ana (sparring) na ya kukimbia akiwa anaendesha tairi la trekta, zoezi maarufu lililokuwa likifanywa na Cheka wakati akijiandaa kuzichapa na Phil Williams kuwania ubingwa wa dunia wa WBF.

Akizungumzia mazoezi hayo, Mwakinyo alisema amekuwa akijifua mara tatu kila siku ikiwamo ya kunyanyua vitu vizito, mazoezi ya kasi ya mikono, kupiga begi na padi, na kukimbia akiwa anaendesha tairi la trekta katika maeneo ya milima.

“Nafanya mazoezi ya kunijenga pumzi, ya mbinu na ufundi, najua ugumu wa pambano linalonikabili, najipanga kuhakikisha naweza rekodi nyumbani ili kuwapa furaha ya ubingwa Watanzania Oktoba 26,” alisema.

Hamis Mwakinyo, kocha wa bondia huyo, alisema Mwakinyo amekuwa akiimarika kila siku katika mazoezi yake jambo ambalo linaonyesha atafanya vizuri zaidi ya alivyofanya Uingereza mwishoni mwa mwaka jana.

“Yuko vizuri, sina wasiwasi na bondia atakayecheza naye, japo naamini litakuwa pambano gumu, ila namuamini Mwakinyo na naamini ataweka rekodi mpya,” alisema Hamis.

Mwakinyo ambaye ni bondia wa 19 wa ubora duniani na namba moja Afrika katika uzani wa welter amewaomba Watanzania na wadau wa ngumi kujitokeza kusapoti pambano hilo ambalo limepewa jina la ‘Pambano la Dunia Tanzania’.

“Mashabiki wengi wa ngumi nchini walitamani kuniona nacheza kwenye Uwanja wa Taifa, kiu ya kuniona nazichapa Dar es Salaam itakoma Oktoba 26, nimejipanga, kikubwa ni wadau kujitokeza kutusapoti,” alisema.

Mabondia Arnel Tinampay wa Ufilipino na Stefano Castellucci wa Italia ni miongoni mwa mabondia wanne ambao mmoja wao ndiye atazichapa na Mwakinyo Oktoba 26, wengine ni kutoka Marekani na Urusi ambao watatajwa Jumamosi ijayo.