Mpenja : Hivi macho yake yanaona kama mimi

Monday April 15 2019

 

By Charity James na Thobias Sebastian

HIVI macho yake yanaona kama mimi au macho yako yanaona kama mimi?

Ni msemo maarufu mjini hivi sasa ulioanzishwa na mtangazaji wa Azam TV, Baraka Mpenja kufuatia bao tamu la kisigino lililofungwa na kiungo Clatous Chama dhidi ya Nkana Red Devils na kuipeleka Simba katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Ilikuwa ni mechi ya marudiano iliyokuwa na presha kubwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwa sababu Simba ilitokea kupoteza 2-1 katika mchezo wao wa awali mjini Kitwe, Zambia.

Wakati wanaingia uwanjani, Simba walikuwa wakifahamu kwamba ushindi wa 1-0 ungetosha kuwavusha, lakini haraka Wekundu wa Msimbazi walijikuta wakitangulia kufungwa goli la mapema dakika ya 17 kupitia kwa straika wa Nkana, Walter Bwalya. Simba sasa ilikuwa ni lazima ishinde 3-1. Kazi haikuwa nyepesi.

Kiungo Jonas Mkude aliisawazishia Simba kwa shuti la mbali katika dakika ya 29 na Meddie Kagere akatupia la pili kwa kichwa katika dakika ya nyongeza kabla ya mapumziko. Kipindi cha pili kilimaanisha kwamba Simba wanahitaji bao moja ili kwenda kwenye hatua ya makundi.

Presha ikawa inapanda kila muda ulivyosogea. Dakika ya 85… dakika ya 86… dakika ya 87…. mambo yalikuwa bado na zikasalia dakika tatu mchezo kumalizika mechi iingie hatua ya kupigiana penalti. Baadhi ya mashabiki walianza kukata tamaa hasa wakikumbuka historia ya timu za Tanzania kushindwa kila penye tunamaini.

John Bocco alikimbia na mpira kishujaa upande wa kushoto na kupiga krosi. Lakini ndani ya boksi hakuwapo mshambuliaji. Alikuwapo Clatous Chotta Chama. Huku akiwa amebanwa na mabeki na huku akiwa amelipa mgongo goli, ‘Mwamba wa Lusaka’, aliusukumia wavuni mpira huo kwa kisigino na kuamsha shangwe lililokaribia kuinua paa la Uwanja wa Taifa.

Advertisement

Ni wakati huu, Baraka Mpenja wa Azam TV aliyekuwa akitangaza mechi hiyo ‘live’ alipolipuka: “Hivi macho yake yanaona kama mimi? Au macho yako yanaona kama mimi?”

Yaliyobaki ni historia.

HARUSI KICHEKESHO

Ukimsikia anavyotangaza mpira, unaweza kudhani Mpenja ‘ana-trend’ kwenye mambo ya soka tu, lakini sivyo.

Kuna jambo moja la kufurahisha kuhusu maisha ya Mpenja nje ya kazi yake ya utangazaji na lilitokea siku yake ya ndoa. Hiyo harusi yake buana ilikuwa ni funga mwaka. Mwenyewe anasema hakutaka makubwa akihofia akichelewa mke wake anaweza akachukuliwa na jamaa wengine, hivyo akafanya sherehe ya harusi ya hali ya chini kabisa.

Alifunga ndoa hiyo ya Kikristo katika Kanisa la Moravian (Yerico) katika Kijiji cha Itete Kata ya Isuto, Tarafa ya Isangati Wilaya ya Mbeya Vijijni mkoani Mbeya.

Burudani ilikuwa ni aina ya usafiri aliotumia yeye na bi harusi wake mpya mara tu baada kufunga ndoa.

“Yaani usafiri wetu ulikuwa boda boda. Mimi na mke wangu tulipanda mshikaki huku nikiwa nimevaa suti na mke wangu ametinga shela. Hatukutaka mambo mengi ya sherehe.

Baada ya hapo tukajipongeza na soda na maisha yetu yakaendelea. Nilichokuwa nakitaka mimi ni kumuoa siyo kingine.

“Siyo kwamba nilikuwa sina pesa, ningeomba michango Azam wangenichangia lakini mimi nilikuwa na haraka zangu.

“Baada ya harusi picha zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii, ikawa inatumika kwa utani wa mitandao, watu wakawa wanasema ‘Msukuma wa wapi huyo?’ Kwa hakika ilikuwa picha maarufu, kila mtu aliiposti kwa kadri awezavyo huku wakiiwekea kila aina ya utani.

“Iliwafikia watu wengi hadi kwa jamaa yangu mmoja ambaye alinipigia simu na kuniandikia ujumbe wa WhatsApp: ‘Mpenja nakufananisha au ni wewe mwenyewe?’ huku akiambatanisha na picha hiyo.

“Nikamwambia ni mimi mwenyewe hujakosea. Alibaki anashangaa na kuniuliza nimekutwa na nini, nikamjibu ‘kupenda ndugu yangu’.

Mpenja ambaye pamoja na mkewe ni Wanyakyusa, anasema picha hiyo haikumuumiza yeye wala mkewe kwa sababu ni kwa mapenzi yao ndiyo wakaamua kufanya walichofanya. Kadri alivyokuwa anasimulia maisha yake, Mwanaspoti likabaini kwa nini anapenda nyimbo za mapenzi za wasanii Diamond Platnumz, Ali Kiba na Barnaba ambao ujumbe wao unakuwa unagusa maisha yake halisi ya mahusiano.

Usikose sehemu ya pili ya mahojiano haya maalum upate kusoma mikasa ya kimapenzi ya mtangazaji huyu, ambaye maneno yake mengi humsababishia kutafutwa wakati mwingine. Unajua chanzo cha Meddie Kagere na Heritier Makambo kumsaka? Unajua nini kilitokea siku walipomwona? Hakikisha unasoma Mwanaspoti kesho Jumanne.

Advertisement