Molinga, Balinya wawapa mzuka Yanga ikijianda kwa Zesco

Wednesday September 11 2019

 

By Saddam Sadick

Mwanza. Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema kiwango walichoonyesha nyota wake, Juma Balinya na David Molinga kimempa nguvu wakati wakijiandaa na mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco.

Yanga iliweka kambi jijini Mwanza kujiandaa na mchezo wa kimataifa dhidi ya Zesco, ilicheza mechi mbili za kirafiki, ambapo awali ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Pamba kisha kuitandika Toto Africans mabao 3-0.

Katika michezo hiyo, Straika David Molinga ‘Falcao’ alionyesha kiwango cha hali ya juu na kuisadia timu yake kufunga mabao matatu, huku kiungo Abdulazizi Makame akifunga moja.

Zahera alisema kiwango cha nyota hao kimeimarika tofauti na siku za nyuma, kwani mapungufu yalikuwa mengi, lakini kwa sasa anaona mambo yamenyooka.

Alisema ikiwa wanajiandaa na mechi ya kimataifa dhidi ya Zesco, anaamini iwapo wataendeleza moto huo Yanga itapata ushindi mzuri kwani malengo yao ni kuipeleka timu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Nimeona kiwango cha Balinya na Molinga nimefurahi wamebadilika sana, kama wataendelea hivi ninaamini mchezo wa Jumamosi tutapata matokeo mazuri,”alisema Zahera.

Advertisement

Alisema wanaobeza kiwango cha nyota hao, lazima wafahamu kazi waliyoifanya ikiwa ni kufunga mabao mengi katika Ligi za kwao, ambapo Balinya amefunga mabao 21 Ligi ya Uganda huku Molinga akitupia 15 kwenye Ligi ya Congo.

Alisema anaamini wachezaji hao watabadilika na kufanya vizuri zaidi, hivyo mashabiki na wadau wa timu hiyo waendelee kuwapa sapoti kwani matunda yao yataonekana.

“Wapo baadhi ya mashabiki wanatukana eti ni wazito, lakini lazima wajue, Balinya alifunga mabao 21 Uganda na Molinga akafunga 15 Ligi ya Congo lazima tuwape hamasa watafanya vizuri hata hapa Yanga,”alisema Kocha huyo.

Kocha huyo aliongeza kuwa katika mchezo wao na Zesco hatarajii kutumia mbinu alizotumia kwenye mechi zake za kirafiki walizocheza jijini hapa,ispokuwa ataingia na vitu vipya.

Alisema kutokana na ugumu wa mchezo huo,hata kikosi kitakuwa na mabadiliko kwani Benchi la Ufundi ndilo litajua ni mchezaji gani aanze na nani asubiri.

“Ni mchezo mgumu kwahiyo tutakuwa na mbinu tofauti kusaka ushindi, lakini lazima tuwe na mabadiliko kujua nani aanze ili kufikia malengo yetu”alisema kocha huyo.

Zahera hakusita kusifia kambi yao ya jijini Mwanza, huku akiweka wazi kuwa walichokifanya katika kambi hiyo kitawasaidia kubaki na ushindi katika mchezo wa Jumamosi.

Advertisement