Mmachinga aibuka mshindi wa E-gazeti

Muktasari:

Kijana huyu ambaye ni mchuuzi wa biashara ndogondogo bahati ilikuwa upande wake kwani pamoja na kuwa mshindi wa jumla ameshinda pia kwenye bahati nasibu na kujinyakulia Sh100, 000.

AMELALA maskini na kuamka tajiri hilo ndilo lililomtokea Felician Stephen (25) ambaye ameibuka mshindi wa jumla wa wiki ya nne ya promosheni ya Tajirika na  E-gazeti inayoendeshwa na kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL)  na kujishindia Sh200,000.

Kijana huyu ambaye ni mchuuzi wa biashara ndogondogo bahati ilikuwa upande wake kwani pamoja na kuwa mshindi wa jumla ameshinda pia kwenye bahati nasibu na kujinyakulia Sh100, 000.

Akizungumza na Mwananchi mara baada ya kushinda kwenye droo hiyo inayofanyika kila wiki Felician alisema ushindi huo ni ukombozi kwenye maisha yake.

Felician alisema mtaji wa biashara yake ulikuwa Sh30000 hivyo zawadi hiyo ya Sh300, 000 atailekeza kwenye kupanua biashara yake.

“Yani hizi pesa nitazitumia kuongeza kwenye biashara yangu. Nilikuwa natembeza vyombo na wakati mwingine kuchoma mahindi lakini sasa najiona naweza kupata hata kibanda nikaweka bidhaa zangu na ikanipunguzia kutembea.

“Ukweli nilikuwa siamini haya masuala ya promosheni na nilikuwa nanunua gazeti kwasababu napenda habari za Mwananchi sikufahamu inaweza kunitoa kimaisha,” alisema Felician

Katika wiki ya nne washindi saba wamepatikana kupitia promosheni hiyo inayolenga kurudisha shukrani kwa wasomaji wa gazeti hilo.

Pamoja na Felician washindi wengine ni Patrick Ngugi, Jaspery Andrew, Hasphan Njama wote wa Dar es Salaam ambao kila mmoja amejishindia Sh 50,000.

Wengine ni Michael Ndendia wa Njombe aliyeshinda Sh25, 000 na Doto Mwenda wa Dar aliyejishindia Sh10, 000.

Ofisa masoko mtandaoni wa kampuni ya MCL Edson Sosten aliwasisitiza wasomaji wa magazeti kuendelea kununua magazeti kupitia E-gazeti ili waweze kupata zawadi mbalimbali.

Alisema droo kubwa ya mwezi itafanyika Agosti 6 ambapo mshindi atapata zawadi ya Sh5 milioni pamoja na fursa ya kulala katika hoteli ya Serena.