Mkomola kicheko Ukraine

Thursday October 1 2020

 

By THOMAS NG’ITU

STRAIKA Yohana Mkomola anayeichezea klabu ya Inhulets, ameandika historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu ya nchini Ukraine kwa mara ya kwanza.

Mkomola anayecheza kwa mkopo katika kikosi hicho akitokea Vorskla Poltava, ameichezea Inhulets kwa dakika 180 baada ya kucheza dakika 60 katika michezo mitatu hadi sasa.

Akizungumza na Mwanaspoti kuhusu kucheza Ligi Kuu, alisema amejikuta akikomaa zaidi kutokana na aina tofauti ya wachezaji wa Ligi Daraja la Kwanza kuwa tofauti na Ligi Kuu.

“Changamoto kubwa ninayokutana nayo ni kukutana na wachezaji wenye uwezo wanaocheza Ligi Kuu muda mrefu, hiyo ni changamoto ambayo kwangu ni kubwa mno ukiangalia mimi ni mara yangu ya kwanza kucheza Ligi lakini nashukuru Mungu nimeanza vyema,” alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga.

Akizungumzia utofauti wa Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Kuu nchini humo, alisema “Tofauti sio kubwa sana, ila Ligi Kuu ina ugumu wake kutokana na ukubwa wake.”

Mkomola akiwa na kikosi hicho kinachoshika nafasi ya 10 kikiwa na pointi tatu katika mechi nne, amecheza mechi tatu Inhulets 1-1 Desna, Kolos 0-0 Inhulets na Inhulets 1-1 Dnipro.

Advertisement

Mkomola aliibukia katika timu ya taifa ya Vijana U17 iliyoshiriki fainali za Afcon (U-17) 2017 Gabon.

Advertisement