Minziro, Mzirai wana jambo lao Mwanza

Muktasari:

Michezo 10 itachezwa leo na kazi kubwa itakuwa kwa timu sita kujua hatma yao ya kubaki au kushuka daraja.

LIGI Kuu Tanzania Bara inamalizika leo Jumapili, Julai 26, 2020 ikiwa tayari taa ya msimu ujao kukaribia kuanza.

Michezo 10 itachezwa leo na kazi kubwa itakuwa kwa timu sita kujua hatma yao ya kubaki au kushuka daraja.

Kocha wa Allince FC, Kessy Mzirai ambaye timu yake itacheza na Namungo FC inayoshika nafasi ya nne amesema ni mchezo wa kuamua hatma yao kwenye Uwanja wa Nyamagana.

"Alama tatu ndio kitu cha pekee kitakachotufanya tuone mwanga kwa namna moja maana nafasi tuliyonayo ni ngumu na mbaya.

"Tunacheza na timu ngumu ambayo inahitaji kumaliza kwa ushindi ili kulinda heshima yake, lakini tunaamini lolote linaweza kutokea," amesema Mzirai.

Mzirai anakutana na timu inayoshika nafasi ya nne yenye pointi 64 huku wao wakishika nafasi ya 18 na pointi zao 42 pointi ambazo ni sawa na timu za Mbao, Mbeya City na Mtibwa Sugar.

Mbao FC yenyewe baada ya matokeo mazuri kwenye michezo yake saba, ikishinda michezo mitano na sare mbili mbele ya Tanzania Prisons ikitoa suluhu na sare ya bao 1-1 na JKT Tanzania nayo ina kibarua kigumu itajiuliza mbele ya Ndanda uwanja wa CCM Kirumba.

Kocha Fred Felix 'Minziro' amesema kikubwa ni kuendelea kupambana hadi hatua ya mwisho na kuona kitu gani watakachokivuna mbele ya Ndanda.

Amesema wanakutana na timu ambayo nayo inahitaji ushindi ili kukwepa kushuka daraja katika mchezo huo.

Mbao ambao wanashika nafasi ya 17 kwenye msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi 42 wanacheza na Ndanda wenye pointi 41 na kushika nafasi ya 19.