Mangalo: Simba, Yanga zilishindwa tu zenyewe kunibeba

ABDULMAJID Mangolo jina lake limekuwa maarufu zaidi baada ya mabingwa watetezi, Simba kuanza kuifukuzia saini yake akiwa bado ni mali ya Biashara United.

Mangalo ambaye ni beki wa kushoto msimu uliopita alionyesha uwezo mkubwa na kuisaidia timu yake kumaliza nafasi ya tatu na ni moja ya timu zilizoruhusu mabao machache.

Jina lake lilitajwa sana kujiunga na Simba mwishoni mwa msimu, kabla ya Wekundu wa Msimbazi kuibukia Coastal Union na kumnasa Ame Ally.

Mwanaspoti lilifanya mahojiano na beki huyo kufahamu kilichokwamisha safari yake hiyo Simba na mengi husu maisha yake ya soka na nje ya soka.

MKATABA KIKWAZO KUJIUNGA SIMBA

Sio Simba pekee iliyokuwa ikiwania saini yake. Anasema klabu nyingi za Ligi Kuu zimekuwa zikimhitaji na kufunguka kilichomkwamiosha,

“Ni kweli Simba ilinifuata ili niwe nao msimu huu, hata hivyo, kuna baadhi ya mambo klabu yangu haikufikia mwafaka na hasa suala la kuvunja mkataba,” anasema na kuongeza kwa sasa ana mkataba wa mwaka mmoja na Biashara na hajaongeza, hivyo, ukimalizika atajua wapi anakwenda kupata changamoto mpya.

“Timu nyingine zilizonifuata ni Yanga, Polisi Tanzania, Mtibwa Sugar na Dodoma na zote zimeshindwa kuvunja mkataba, ndio maana nimebaki hapa,” anasema.

 

SOKA LAKE ARSENAL INAHUSIKA

Anasema hakuwa na ndoto ya kucheza soka lakini mazingira aliyokulia na hasa baba yake yalimshawishi.

“Baba alikuwa ni shabiki wa Arsenal. Alikuwa akininunulia begi la shule na waleti (pochi) ya kuhifadhia pesa zenye nembo ya Arsenal, hivyo nilijikuta naanza kuifuatilia timu hiyo kuwajua wachezaji na kuanza kutamani kucheza kwani nilikuwa naiga mengi kutoka kwao.”

Anasema kipindi anafanya yote hayo alikuwa darasa la tatu na alikuwa akitafuta mpira apatapo nafasi na kufanya walichofanya wachezaji wa Arsenal timu anayoishabikia.

“Nilikuwa nacheza kwa kujificha, hivyo wazazi wangu haikuwa rahisi kunielewa naweza kuja kuwa mchezaji mzuri kwa kuwa hawakuwahi kuniona nikicheza,” anasema.

UMISETA ILIMUUMBUA

Kipaji hakifichiki. Beki huyu anafichua pamoja na kucheza kwa siri wazazi wake wasijue, hata hivyo zawadi alizokuwa kipokea kwenye mashindano ya shule zilifichua kila kitu.

“Nilikuwa nafanya vizuri kwenye mashindano hayo, hivyo zawadi mbalimbali nilizozipata nilishindwa kuficha na walishaanza kusikia taarifa zangu.

“Hata hivyo, niliendelea kujituma mazoezini huku nikijua nyumbani wanataka nisome. Namshukuru Mungu kwa sasa wananisapoti kwani niliweka nia kuhakikisha familia inajua nafanya nini ili iweze kunipa ushirikiano kwenye soka na hadi sasa napata,” anasema.

LAKI NA NUSU YAONGEZA JUHUDI

Anasema alipata Sh100, 000 baada ya kufanya vizuri kwenye michuano iliyofanyika Pemba akiwa na timu yake ya Black Wizard.

“Nakumbuka nilifanikiwa kujipatia laki na nusu baada ya timu yetu kufanya vizuri kwenye mashindano tuliyokuwa tunashiriki, hiyo ndiyo fedha yangu ya kwanza kubwa kuishika nikiwa mchezaji kijana,” anasema Mangalo aliyelelewa na kituo cha kukuza vipaji cha Sniper Academy

“Fedha hiyo niliitumia kwa kuinunulia familia yangu zawadi kwa kuwa nilikuwa mbali na nyumbani. Niliwanunulia mama na wadogo zangu vitenge, kanga na baba nilimpelekea jezi kama sehemu ya shukrani kwa kuwa wananisapoti,” anasema.

SURE BOY NJE FEI TOTO NDANI

Anawataja Abubakari Salum ‘Sure Boy’ wa Azam FC na Feisal Salum anayekipiga Yanga ndio viungo bora kwake, hata hivyo kwenye kuamua nani aanze ni kazi lakini kama ni kuchagua ataanza na Fei Toto.

“Kila mmoja ana staili yake ya kucheza ingawa wote wana ubora. Nikiambiwa nani aanze kwenye kikosi basi karata yangu nampa Fei Toto,” anasema na kumwelezea ni kiungo anayeweza kufanya majukumu mawili kwa wakati mmoja, kusaidia mashambulizi na kuzuia.

MWANYENTO FRESH KWA YONDANI

Kwa sasa beki kisiki nchini, Kelvin Yondani hayupo Yanga na nafasi yake imechukuliwa na Bakari Mwamnyeto.

Yondani alipewa mkono wa kwaheri Jangwani baada ya kuichezea kwa mafanikio kwa misimu mingi.

Hata hivyo, kutokana na usajili wa Mwamnyeto kama mbadala wake, Mangolo anasema kwake anaona ni usajili bomba na Yanga walicheza karata zao vizuri.

“Wote nawakubali. Yondani ni beki bora asiyekubali kupitwa kirahisi na ni mfano wa kuigwa,” anasema na kuongeza “Mwamnyeto ni kijana mwenzangu. Nampongeza kwa kupata nafasi ya kuaminiwa na timu yake na  timu ya Taifa. Ameonyesha  thamani sana. Nampongeza sana kwani ananifanya nijieke kwenye katika ushindani zaidi,” anasema na kuongeza wangekuwa kwenye kikosi chake, angeanza na Mwamnyeto kwani ni kijana na ana nafasi ya kuonyesha uwezo zaidi wa kusaka mafanikio.

ANAMKUBALI ALIKIBA

Mbali na soka, Mangalo anafichua ni shabiki mkubwa wa muziki na awapo nyumbani muda wake wa mapumziko hupenda kusikiliza na msanii anayemvutia ni Alikiba.

“Huwa nafuatilia wasanii wote, lakini kwangu Alikiba ndiye kiboko kwani anajua sana kuimba,” anasema na kuongeza ni King wa muziki nchini na anamshinda hata Diamond.

“Alikiba ni King wa muziki kama mwenyewe anavyojiita anajua sana kuimba, anaburudisha na kuelimisha lakini Diamond anafanya muziki kama biashara na ndio maana amefanikiwa haraka,” anasema.

THIAGO SILVA AMPA JEZI NO MBILI

“Napenda sana kuvaa jezi namba mbili na nimeanza kuitumia muda mrefu kwa sababu ni namba mojawapo ambayo ipo kwenye tarehe ya kuzaliwa,” anasema na kuongeza,

“Mbali na hilo, pia ni namba ambayo inavaliwa na mchezaji ambaye nampenda na nimekuwa nikimfuatilia kutokana na namna anavyocheza Thiago Silva,” anasema.

YANGA YAMPA HISTORIA

Wachezaji huwa wanakumbana na changamoto kwenye upambanaji wao, pia wamekuwa wakikutana na matukio mazuri yenye kuwapa furaha, hilo limethibitishwa na beki huyo ambaye ameweka wazi tukio lake la furaha ni siku alipoifunga Yanga.

“Kwangu mechi ya Yanga ambayo niliweza kufunga bao la kwanza na la uongozi msimu wa mwaka juzi 2018, nilifurahi sana na ni tukio ambalo sitokaa nikasahau kwa sababu kabla ya mchezo niliweka nia ni lazima nifunge na kweli nilitimiza hilo,” anasema.

LIGI ISIPOONYESHWA CHANGAMOTO

Misimu ya nyuma baadhi ya mechi zilikuwa hazirushi moja kwa moja kwenye runinga na hivyo baadhi ya mashabiki kukosa kuziona. Jambo hilo lilimuumiza sana Mangalo na kufunguka wamekuwa wakionewa sana.

“Mechi inapokuwa haionyeshwi kunakuwa na changamito nyingi ambazo zinadidimiza soka letu kwani maamuzi kwa asilimia kubwa hayawi sawa, hivyo inatufanya tuwe wapambanaji ili kuweza kufikia lengo tulilokusudia sio rahisi sana kufanikiwa,” anasema huku akiweka wazi hataki kuwa mzungumzaji zaidi kwenye hilo.