MTU WA PWANI : Hivi ni kocha gani duniani anaifaa Tanzania?

Muktasari:

Baada ya Amunike kutimuliwa, swali la msingi ni je matatizo yanayolikabili soka letu hadi timu zetu za taifa zinashindwa kufanya vizuri yatakwisha?

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), lipo kwenye mchakato wa kutafuta makocha wa muda mfupi na mrefu wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’.

Hatu hii ni baada ya kumtimua aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Emmanuel Amunike baada ya Stars kufanya vibaya kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zinazoendelea huko Misri.

Baada ya kelele za muda mrefu na ushawishi wa kundi kubwa la wadau wa soka nchini, TFF ni kama imewatimizia kiu yao kwa kumtimua kocha.

Kiuhalisia uamuzi wa kumtimua Amunike umetokana zaidi na shinikizo la baadhi ya watu kwa sababu kufanya vibaya kwa Stars kwenye Afcon ni jambo ambalo lilikuwa wazi.

Aina ya timu tulizocheza nazo zilikuwa zimetuacha mbali kwa maana ya ubora wa mchezaji mmoja mmoja, maandalizi, uwekezaji ambao zimeufanya na uzoefu wa mashindano.

Watu walimhukumu Amunike kwa kushindwa kuvuna kitu ambacho hakikupandwa. Ni sawa na bosi anayemlaumu kibarua kwa kutovuna matikiti wakati alimpa mbegu za karoti.

Baada ya Amunike kutimuliwa, swali la msingi ni je matatizo yanayolikabili soka letu hadi timu zetu za taifa zinashindwa kufanya vizuri yatakwisha?

Inavyoonekana Watanzania tumesahau matatizo ya msingi yanayolikabili soka letu na kuamua kugeukia kuwabebesha zigo la lawama makocha pindi timu zetu za taifa zinapofanya vibaya.

Tunajiaminisha kuwa makocha ndio sababu ya kufanya vibaya kwetu badala ya kujikita kutazama changamoto nyingine ambazo zinatufelisha. Ni sawa na mtu anayetumia nguvu kubwa kunyoosha kivuli wakati uliopinda ni mti.

Hadi leo tumeshindwa kujiuliza kwa nini tumekuwa tukibadilisha makocha lakini bado timu zetu hazifanyi vizuri. Kwa bahati nzuri, makocha wengi ambao tunajiaminisha kuwa ndio wanatuangusha hugeuka lulu mahali pengine baada ya kufanya vizuri. Je tumejitazama na kujitafakari kuwa pengine sisi ndio wenye matatizo?

Simba iliwahi kuwa na kocha Pierre Lechantre lakini ikamtimua kwa madai kuwa anacheza soka la kujilinda. Matokeo yake kwa sasa ni miongoni mwa wataalamu wa jopo la ufundi la Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA).

Kocha Mart Nooij aliwahi kuonekana hafai kwenye timu ya taifa na akatimuliwa, lakini mwisho wa siku akaenda kutwaa mataji Ethiopia akiwa na St. George. Kuna Milutin Sredojevic ‘Micho’, alipata nafasi ya kuinoa Yanga lakini alijikuta akiondolewa kwa madai kuwa uwezo wake ulikuwa ni mdogo.

Lakini ni huyo Micho ambaye baadaye alielekea Uganda kufundisha timu ya taifa na kuipa mafanikio makubwa huku akiwatengenezea msingi imara wa soka ambao unaibeba nchi hiyo hadi leo.

Alikuja hapa kocha Mathias Lule kuifundisha Stand United ikamuona hafai lakini leo ni kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Uganda, huku timu hiyo ya Shinyanga ikijikuta imeshuka daraja.

Kuna kocha anaitwa Dylan Kerr. Huyu naye aliondoka kimaajabu pale Simba kwa kutimuliwa akiwa anaongoza ligi na kudaidwa kuwa timu ilikuwa haichezi vizuri.

Matokeo yake alienda kuinoa Gor Mahia ya Kenya na kugeuka shujaa kwa kuipa mataji mawili mfululizo ya Ligi ya Kenya, Kombe la SportPesa lakini pia aliiongoza kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kuna mifano mingi ya makocha ambao walikuja nchini na wakaonekana hawafai lakini wakaenda kwingine wakafanya vizuri. Wengi wanaondolewa kutokana na presha na misukumo ya mashabiki na wadau wa soka ambao wengi wao hawana hata taaluma ya ukocha.

Na mara kwa mara, chuki dhidi ya makocha hawa zinatokana na misimamo yao ya kutotaka kuingiliwa katika utimizaji wa majukumu yao. Ni hulka ya kundi kubwa la Watanzania kujifanya wajuaji wa soka na kupenda kuwalazimisha makocha kufanya kile wakipendacho badala ya kuwapa uhuru wa kutimiza majukumu yao.

Uamuzi wa kumtimua Amunike unapaswa uwe mwanzo wa Watanzania kujitafakari, kubadilika na kuachana na tabia ya ujuaji na kuwapangia makocha nini cha kufanya kwani mwisho wa siku ndio imekuwa ikichangia kutuangusha.

Vinginevyo tutaendelea kutimua makocha kila siku lakini soka letu halipigi hatua.

Unapoondoa kocha maana yake yeye ndio alikuwa chanzo cha tatizo hivyo kama mafanikio hayapatikani kwa kocha mwingine mpya, maana yake tatizo halipo kwa makocha hao.

Kama tusipobadili tabia, maana yake tutakuwa tunafanya kazi bure ya kubadilisha pori wakati nyani ni walewale.