Lionel Messi alivyosambaa kila kona duniani

Saturday June 22 2019

 

MANCHESTER, ENGLAND. LIONEL Messi ni kama hewa ya oksijeni unaambiwa. Anapatikana karibu kila mahali.

Ni hivi, kuna mastaa wengi sana wamepachikwa majina ya ‘Messi Mpya’ kutoka sehemu nyingi tofauti katika dunia hii. Lakini, kitu cha kushangaza, hakuna hata mmoja aliyekaribia makali ya Lionel Messi mwenyewe, staa wa Barcelona na Argentina anavyofanya anapokuwa ndani ya uwanja.

Kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, Manchester United imehusishwa na mchezaji, ambaye anatajwa kuwa Messi Mpya, kinda wa Trabzonspor huyu, Abdulkadir Omur.

Kinda huyo wa miaka 19, amefunga mabao manne na kuasisti saba katika Ligi Kuu Uturuki msimu uliopita na kiwango chake cha uwanjani amekuwa akifananishwa na Messi na kuitwa ‘Messi wa Uturuki’ kutokana na kiwango chake alichokionyesha msimu uliopita.

Hata hivyo, huyo si mchezaji wa kwanza aliyeibukia na kuitwa Messi Mpya, kuna mastaa wengi sana kutoka pande tofauti za dunia hii, wakati walipokuwa wakiibukia walipachikwa majina ya Messi Mpya, kisa tu wanatumia miguu ya kushoto, lakini ubora wao hawamwezi kabisa Muargentina huyo.

Messi wapo kila kona katika dunia hii, huku England ikiwa nao wawili. Inachekesha.

Advertisement

Messi wa England - Patrick Roberts

Wakati anaibukia kwenye kikosi cha Fulham akicheza soka matata, Patrick Robert alipachikwa jina la Messi Mpya. Manchester City walimwelewa na kuamua kutoa Pauni 12 milioni kunasa saini yake. Lakini, baada ya kunaswa tu na Man City, mambo yamekuwa tofauti na amejikuta akitolewa kwa mkopo kwenye Celtic. Licha ya kwamba amebeba mataji ya kutosha huko Celtic akiwa chini ya Brendan Rodgers, Roberts aliandamwa na majeruhi na kushindwa kung’ara na matokeo yake kutolewa tena kwa mkopo huko Girona, ambako alicheza mechi 14 tu kutokana na kuwa majeruhi. Messi mwingine wa England ni mchezaji wa timu ya taifa ya wanawake, Fran Kirby.

Messi wa Scotland - Ryan Gauld

Gauld alikuwa na umri wa miaka 17 wakati anacheza mechi yake ya kwanza kwenye kikosi cha Dundee United na kuanza kutamba huko Scotland, ambapo aliisaidia timu hiyo kufika fainali ya Kombe la Scotland mwaka 2014. Baada ya kuwekwa kwenye orodha ya Kinda Bora wa Mwaka, , Gauld alinaswa na Sporting Lisbon. Lakini, baada ya kwenda kujiunga na Wareno hao, Gauld alicheza mechi tano tu kwenye kikosi cha Sporting kwa mwaka wote wa 2014 hadi mwanzoni mwa 2015 na baada ya hapo amekuwa akitolewa tu kwa mkopo na ameshindwa kutamba.

Messi wa Uswisi

- Xherdan Shaqiri

Kufananishwa na Messi ni jambo la mbali sana, licha ya kwamba Shaqiri amekuwa mwenye kipaji imara kinachomfanya awe na uwezo wa kucheza timu yoyote ile duniani. Amecheza kwenye klabu kubwa na amefunga kwenye fainali mbili za Kombe la Dunia na kwenye michuano ya Ulaya. Lakini, ukweli ni kwamba Shaqiri hajaweza kufikia maajabu ya Messi na kwamba ataendelea tu kufananishwa licha ya kwamba hajafikia uwezo wa Muargentina huyo ambaye siku zote amekuwa tishio kwa wapinzani anapokuwa na mpira ndani ya uwanja.

Messi wa Misri

- Mohamed Salah

Staa mwingine mkubwa anayefananishwa na Messi. Lakini, ukweli Mo Salah hajafikia kwenye kiwango bora kabisa cha Messi, licha ya kwamba amekuwa na uchezaji mzuri ndani ya uwanja. Jina hilo Mo Salah alipachikwa wakati alipokuwa akikipiga kwenye kikosi cha FC Basel. Lakini, baada ya hapo, Salah amecheza kwa kiwango kikubwa, lakini hakufikia kwenye kiwango kile cha Messi na kubaki kwenye ubora wake tu, ambao pengine kutakuwa na mchezaji mwingine atayeibuka huko na kufahamika kuwa Salah Mpya.

Messi wa Catalan

- Gerard Deulofeu

Jambo moja muhimu ni kwamba unapaswa kuwa na kipaji kikubwa sana cha soka ili uweze kulinganishwa na Messi. Huko Catalan, anakotamba Messi mwenyewe mwenyewe katika chama la Barcelona na wao walimpata Messi wao, Deulofeu. Wakati anakua staa huyo alionekana kuwa angefuata nyayo za Muargentina huyo, lakini Deulofeu kwa sasa yupo Watford ameshindwa hata kutunza kiwango chake tu cha soka ndani ya wiki moja. Deulofeu naye alicheza Barcelona katika awali mbili, lakini ameshindwa kutoboa na hivyo kwenda kuichezea Watford, ambapo msimu uliopita walifika fainali ya Kombe la FA.

Messi wa Ujerumani

- Marko Marin

Alitua Chelsea mwaka 2012 akiwa na matumaini makubwa, lakini ni kama kwa makinda wengi wa Chelsea, baada ya kufika tu Stamford Bridge wameshindwa kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza. Alitolewa kwa mkopo mara nne katika misimu mitatu na kufanikiwa kucheza mechi sita tu kwenye Ligi Kuu England akiwa na kikosi cha The Blues. Baada ya hapo, Marin alikwenda sana huko Ugiriki na kutamba pia Hispania na Serbia alikobeba mataji tofauti kunogesha soka lake, lakini hajafikia kiwango cha Messi wa Argentina.

Messi wa Croatia

- Alen Halilovic

Staa mwingine wa kutokea kwenye akademia ya Barcelona, ambapo staa huyo wa kimataifa wa Croatia na ufundi mkubwa mpira unapokuwa kwenye miguu yake, lakini shida ni kwamba hana ubavu wa kutosha wa kupambana kwenye soka la kibabe. Mkopo wake huko Sporting Gijon haukuleta matunda sana. Kwa sasa anakipiga kwenye kikosi cha AC Milan, lakini ametolewa kwa mkopo Standard Liege, ambako alishindwa kabisa kupata nafasi katika kikosi cha kwanza na hivyo kushindwa kuliishi jina la Messi alilopachikwa.

Messi wa Norway

- Martin Odegaard

Mmoja wa makinda waliopambwa sana kwenye soka la Ulaya baada ya kuhama kutoka Stromsgodset kwenda kujiunga na Real Madrid mwaka 2015. Mwanzoni alishindwa kumudu kuishi kwenye sifa anazopewa wakati alipokuwa kwa mkopo kwa miaka miwili huko, Heerenveen ambako alikuwa akiingia na kutoka katika kikosi cha kwanza. Msimu uliomalizika alikuwa kwa mkopo Vitesse. Odegaard anaweza kupata nafasi ya kupata nafasi katika kikosi cha Real Madrid kwa msimu ujao.

Messi wa Ireland

- Alan Judge

Winga huyo alipachikwa jina hilo wakati alipokuwa akicheza huko Brentford, ambako alitamba kwa miaka mitano. Judge aliisaidia timu hiyo kucheza kwenye Championship, akitamba huko na kutajwa kwenye timu bora ya msimu katika ligi hiyo kwa mwaka 2013 na 2016. Kwa sasa yupo katika kikosi cha Ipswich, ambako ameshindwa kuwafanya wababe hao kubaki kwenye ligi hiyo na hivyo kushindwa kuliishi jina la staa ambaye amekuwa akilinganishwa naye. Judge hajawahi kuwa kugusa japo chembe tu ya kiwango cha Messi.

Messi wa Peru

- Raul Ruidiaz

Amepachikwa jina la ‘Messi Mtoto’. Ruidiaz, amefunga mabao mengi sana huko Peru na Mexico kabla hajatimkia kwenye Ligi Kuu Marekani mwaka 2018. Straika huyo amekuwa kwenye kiwango bora kabisa akiwa na kikosi cha Seattle Sounders, ambapo amefunga mabao 16 katika mechi 21. Lakini, licha ya kucheza kwa kiwango bora hivyo, Ruidiaz ameshindwa kupita kwenye nyayo zile matata kabisa za staa anayelinganishwa naye katika dunia ya soka, kwamba ni Messi mtoto. Messi orijino si mchezaji wa mchezomchezo.

Messi wa Kosovo

- Edon Zhergova

Edon Zhegrova alikuwa staa mkubwa kwenye YouTube mwaka 2014 baada ya kuwekwa kwa video yake ya mabao ya hatari kipindi hicho akiwa na umri wa miaka 15 tu na kupata watazamaji wengi, maelfu kwa maelfu. Baada ya hapo akasakwa na timu nyingi ikiwamo Arsenal, PSG na Barcelona, lakini alishindwa kujiunga na timu hiyo hiyo na kuamua kutimkia zake Standard Liege na baadaye akajiunga na Genk, ambako alicheza kukuza soka lake kabla ya kuchukuwa kwa mkopo na Basel, ambako ameonyesha kiwango bora licha si kwa daraja la Messi mwenyewe mwenyewe.

Messi wa India

- Lallianzuala Chhangte

Winga wa Delhi Dynamos amekuwa kinda matata wa timu ya soka ya India ambapo alianza kuichezea mwaka 2015. Kwa sasa umri wake ni miaka 21 na asikwambie mtu mambo yake ya uwanjani yalikuwa si ya kitoto. Lakini, Chhangte ameshindwa kutamba kwenye soka kama ilivyokuwa mwanzoni na hivyo kuonekana kama vile jina la Messi Mpya lilimzidi uwezo na kumpoteza kabisa katika mchakamchaka huo wa mchezo wa soka duniani. Kuwa Messi kunahitaji kuwa na kiwango bora sana ndani ya uwanja.

Messi wa Japan

- Takefusa Kubo

Ndio kwanza ana miaka 18, Kubo ana nafasi kubwa sana ya kwenda kuwa mchezaji mkubwa zaidi na kuishi maisha ya soka analotabiriwa. Fowadi huyo wa FC Tokyo aliibukia kwenye akademia ya Barcelona, ambako alikuwa staa mkubwa sana wa timu ya vijana kabla ya kurudi kwao Japan. Angeweza kubaki La Masia, lakini baada ya Barcelona kukumbana na adhabu ya kusajili, jambo hilo lilimfanya awe na wakati mgumu wa kucheza mechi za kimashindano na hvyo aliamua kurudi zake kwao Japan. Msimu ujao atakuwa kwenye kikosi cha Real Madrid.

Messi wa Iran

- Sardar Asmoun

Klabu kibao za Ulaya zilionyesha dhamira ya dhati ya kuhitaji huduma ya Asmoun miaka michache iliyopita, ikiwamo Arsenal, ambao waliweka mezani ofa ya Pauni 2 milioni kwa ajili ya kumnasa mshambuliaji huyo mwenye kasi ya hatari uwanjani. Kwa sasa umri wake ni miaka 24 na Asmoun ni staa huko Russia, ambako amefunga mabao 11 katika mechi 13 alizocheza na kuisaidia Zenit St Petersburg kushinda ubingwa baada ya uhamisho wake katika dirisha la majira ya baridi. Hata hivyo, Asmoun ameshindwa kufikia viwango vile vya soka la Messi mwenyewe mwenyewe.

Messi wa Ugiriki

- Giannis Fetfatzidis

Winga huyo mwenye umbo dogo ameshindwa kabisa kuishi kwenye ustaa wa jina analolinganishwa nalo baada ya kuibukia kwenye kikjosi cha Olympiacos. Baada ya hapo alikwenda kukipiga huko Italia na Saudi Arabia, lakini kwa sasa amerudi zake Ugiriki kuichezea Aris. Messi huyo wa Ugiriki ameshindwa kutoboa na kucheza soka ambalo wengi waliamini kwamba angekuwa moto zaidi wakati anaibukia kiasi cha kuwafanya watu kumpachika jina la mchezaji anayejua mpira pengine kuliko wote duniani katika kizazi hiki cha kisasa.

Messi wa Uturuki

- Abdulkadir Omur

Kama ilivyojieleza, Omur amekuwa kwenye kiwango bora kabisa katika kikosi cha Trabzonspor kwa kipindi cha karibuni na jambo hilo limemfanya awindwe na timu nyingi za Ulaya. Manchester United ni miongoni mwa timu zilizokuwa zikimsaka staa huyo mwenye umri wa miaka 19 tu, ambaye huku Uturuki wanamwona kuwa ni Lionel Messi wao kutokana na mambo yake makali anayofanya ndani ya uwanja huku akicheza soka la kiwango cha juu san. Hata hivyo, Omur bado ana safari ndefu ya kuifikia katika kulifikia soka analocheza mtu anayelinganishwa nao.

Messi wa Indonesia

- Egy Maulana Vikri

Umri wake ni miaka 18, lakini Egy tayari ameshaanza kuichezea timu ya taifa ya nchi hiyo na kuonyesha soka la kiwango bora kwelikweli. Amefunga mabao 15 katika mechi 16 alizochezea timu ya taifa ya Indonesia kwa umri wa miaka chini ya 19, huku huduma yake ikizivutia klabu nyingi za Ulaya zinazotaka kwenda kumsajili. Lakini, Maulana aliamua kujiunga na Lechia Gdansk mahali ambako amekuwa moto zaidi kwenye kikosi cha akiba, akifunga mabao 12 katika mechi 14 alizocheza katika kikosi hicho cha Ligi Daraja la Nne huko Poland. Timu ya taifa ya wakubwa alianza kuichezea Desemba mwaka jana.

Messi wa Mexico - Diego Lainez

Miaka 18 kwenye umri wake na Lainez ana nafasi kubwa ya kwenda kuwa staa mkubwa kwenye soka na kitu kizuri kuhusu kinda huyo ni kwamba ameweza kutunza kiwango chake cha pesa akicheza kwa daraja la juu kabisa na kuzifanya timu nyingi kuanza kumtolea macho. Kinda huyo tayari ameshaanza kuitumikia timu ya taifa ya Mexico na Januari mwaka huu alinaswa na Real Betis kwa ada ya Pauni 9 milioni. Lakini, sasa amekuwa akitokea benchi kwenye kikosi hicho na kushindwa kufikia kwenye kile anachofananishwa nacho kwamba Messi Mpya.

Messi wa Korea Kusini

- Lee Seung-woo

Lee aliwahi kupewa sifa kubwa kwamba mmoja wa wanasoka matata kabisa waliowahi kutokea Korea Kusini huku akiwa ameibukia kutoka kwenye akademia ya Barcelona, La Masi. Alihamia Catalonia mwaka 2011, lakini alicheza mechi moja tu kwenye kikosi cha Barcelona B, kabla ya kuhamia Hellas Verona mwaka 2017. kwa sasa umri wake ni miaka 21 na winga huyo amekuwa na msimu mzuri huko kwenye Serie B na amekuwa shujaa wa taifa lake kwenye Kombe la Asia. Lee alitoa asisti kwa Son Heung-min wa Tottenham na kufunga bao la ushindi katika michuano hiyo.

Messi wa Malaysia

- Faiz Nasir

Messi wa Malaysia ni mmoja wa wachezaji wadogo zaidi kwenye dunia ya soka. Nasir anaposimama kimo chake ni futi 5 tu. Lakini, amekuwa na kipaji kikubwa sana, kwamba miguu yake ina ufundi mkubwa anapokuwa na mpira. Amekuwa mchezaji muhimu akifunga pia kwenye mechi yake ya kwanza ya soka la kimataifa aliyocheza mapema mwaka huu na kuwa mmoja wa makinda wenye viwango vya juu sana. Hata hivyo, Nasir ana safari ndefu sana ya kwenda kufikia viwango vya mtu anayefananishwa naye kwenye soka la dunia.

Messi wa Nigeria

- Stanley Okoro

Amepachikwa jina la ‘Messi Mtoto’, Okoro ametumikia muda wake mwingi huko Hispania akiichezea Almeria, lakini ameshindwa kupenya na kupata namba katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo. Lakini, mwenyewe anaonekana kulipenda jina analoitwa kwamba ni Messi, akisema: “Sijali watu wanaponiita Messi Mtoto. Ni kitu kizuri kulinganishwa na mwanasoka bora duniani, mimi sina tatizo na jambo hilo.” Hata hivyo, kitendo cha kushindwa tu kupata nafasi kwenye timu yake huko linamfanya Okoro kuwa na safari ndefu ya kwenda kuwa Messi kutokana na ubora wake.

Messi wa Thailand

- Chanathip Songkrasin

Songkrasin anafahamika kama ‘Messi Jay’ au ‘Jay’, lakini kubwa ni kwamba amekuwa akicheza soka lake kwa kumuiga staa huyo wa Kiargentina. Baba yake amekuwa akimnoa kwa kumtaka aige vitu vya Muargenntina mwingine, Diego Maradona. Amekuwa kipenzi cha mashabiki wengi huko Thailand kutokana na uhodari wake wa kukokota mipira, huku akiwa ameshacheza mechi 52 za timu ya taifa hadi sasa na soka lake la ngazi ya klabu anacheza huko Japan kwa sasa. Pamoja na kupendwa huko Thailand, lakini Songkrasin bado hawezi kucheza soka lake kwa kiwango cha mchezaji anayelinganishwa naye.

Messi wa Afrika Kusini

- Tebogo Tlolane

Winga huyo Tlolane amepachikwa jina la Messi tangu akiwa mdogo kutokana na uwezo wake wa kukokota mipira. Aliwahi kwenda kufanya majaribio kwa wiki mbili huko Barcelona, lakini alifeli. Kwa sasa Tlolane amerudi zake Afrika Kusini akikipita kwenye kikosi cha Chippa United, ambako amebadilishwa na kucheza kwenye beki ya kushoto. Ndiyo hivyo, kutoka kuwa Messi hadi kwenda kucheza beki ya kushoto baada ya mambo kwenda kombo, akifeli majaribio yake huko Nou Camp.

Advertisement