Koeman anataka kuibomoa Liverpool

Monday September 14 2020

 

BARCELONA, HISPANIA. BARCELONA ina jambo lao kwa Liverpool, ilianza kwa kiungo Georginio Wijnaldum sasa imehamia kwa staa Mohamed Salah ambaye ni mmoja kati ya wachezaji tegemeo katika kikosi hicho.
Ripoti zinadai kuwa Barca imemuweka Salah kama mchezaji kinara kwenye orodha ya wachezaji ambao inatarajia kuwasajili katika dirisha hili. Hiyo ikiwa ni moja ya harakati za kocha Ronald Koeman wa Barca ambaye ametamba kuwa anatasainisha wachezaji ambao watalitikisa soko hili la usajili.
Taarifa yakuwa Koeman yupo kwenye harakati za kuiwania saini ya Salah na sio Sadio Mane kama ilivyoelezwa hapo awali ni rafiki yake wa karibu mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa ya Uholanzi na Ajax, Sjaak Swart ambaye anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji aliyecheza mechi nyingi zaidi katika Klabu ya Ajax.
“Najua Koeman anamuhitaji huyu na nina uhakika Salah hawezi kukataa, Siwezi kukwambia zaidi ya hapo, lakini ninachojua ni kuwa muda wowote anaweza kumsajili”
Huyo anakuwa mchezaji wapili wa Liverpool baada ya Georginio Wijnaldum kuhusishwa na tetesi za kutaka kutua Barcelona katika dirisha hili la usajili. Lakini uwepo wa Messi ndani ya kikosi unatajwa kuwa kikwazo kimoja wapo kinachowafanya mabosi wa Barca kusita kutoa kiasi kikubwa cha pesa ili kufanikisha mchakato wa kuipata saini ya Salah. Hiyo ni baada ya Messi kutaka kuondoka na uongozi ukamwambia atoe Pauni 630 ili kuvunja mkataba wake.
Salah ni miongoni mwa wachezaji tegemeo ndani ya kikosi cha Liverpool kwa misimu kadhaa na msimu uliopita aliisaidia kuchukua ubingwa wa kwanza toka mwaka 1990.
Katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu dhidi ya Leeds, fundi huyo kutoka Misri aliiwezesha Liver kutoka kifua mbele baada ya kupiga hat-trick. Katika mchezo ambao ilifanikiwa kushinda mabao 4-3, licha ya madhaifu makubwa yaliyo oneshwa na safu ya ulinzi.
Inaelezwa Koeman anataka kuwachezesha Philippe Coutinho, Messi na Salah katika eneo la ushambuliaji baada ya kumruhusu Suarez kutafuta timu ya kucheza.
Utatu huo unatajwa kuwa utasumbua zaidi kutokana aina ya wachezaji wanaokwenda kukutana, Coutinho ambaye ametoka kuisaidia Bayern Munich kuchukua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa, Bundesliga na DFB-Pokal na Salah ambaye ametoka kushinda taji la Ligi Kuu,England wanatazamiwa kuwa miongoni mwa wachezaji watakaoonesha viwango bora katika muunganyiko wao na Messi kwa kuangalia walichokifanya katika msimu uliopita.
Salah ambaye ana umri wa miaka 28, Juni mwakani atakuwa anafikisha umri wa miaka 29 na mkataba wake unaotarajiwa kumalizika mwaka 2023 utakuwa umebakisha miaka miwili.
Ripoti zinadai kuwa Liver inaweza ikakubali kumuuza kutokana na umri wake na muda uliobakia kwenye mkataba wake, kwani ikifika dirisha lijalo la majira ya kiangazi thamani yake itazidi kushuka na kwa sasa haonekani kutaka kuongeza mkataba mpya.

Advertisement