Kocha Nigeria awapa neno nyota wake Afcon

Muktasari:

  • Kocha huyu aliirejesha Nigeria kwa mara ya kwanza katika Fainali za Afcon tangu walivyochukua ubingwa mwaka 2013.

Achana na kipigo cha 2-1 walichokipata dhidi ya Algeria katika mchezo wa nusu fainali (AFCON), kocha mkuu wa Nigeria, Gernot Rohr amechukulia matokeo hayo katika upande wa usawa kwa vijana wake kujifunza.

Katika mchezo huo mshambuliaji Riyad Mahrez aliibuka shujaa baada ya kupiga faulo iliyoenda moja kwa moja wavuni na kufanya mchezo huo ukimalizika Algeria wakitoka kifua mbele 2-1 na kwenda katika fainali.

Gernot ambaye alisema timu yake ina vijana wengi na bila shaka wamejifunza kupitia matokeo hayo na ana uhakika watafanya vizuri katika michuano ijayo inayokuja.

“Nadhani hii timu imetokana na matokeo mazuri ya Kombe la Dunia, tunajivunia kwa kiwango tulichokionyesha, lakini katika upande wa mbinu wenzetu walionekana kutuzidi katika upande wa uzoefu,” alisema.

Aliongeza wanabidi wafanye kazi na kuwasoma wachezaji wake vijana kwa sababu anaamini uzoefu ulichangia wao kupoteza katika mchezo wa dhidi ya Algeria.

“Viungo wetu Etebo (Paul) na Ndindi (Wilfred) ni vijana wanahitaji kujifunza katika mawasiliano na jinsi ya kuutuliza mchezo, lakini hilo tumeshalichukua na naamini tutakuwa bora zaidi baadae,” alisema.

Alifunguka zaidi na kusema “Nilianza hii safari baada ya kuchaguliwa kutengeneza upya vijana wa Nigeria, kiukweli tulitokea mbali mpaka kufika hapa tulipo,” alisema.