Kocha Gor atii,Ingwe wameanza kushika nare

Muktasari:

Matokeo hayo yalimwezesha Polack kuhakikisha kasajili ushindi wa asilimia 100% kwenye mechi zote za Mashemeji Derby alizoweza kusimamia zikiwa ni mbili sasa.

Nairobi, Kenya.MKUFUNZI wa Gor Mahia, Mwingereza Steve Polack katii AFC Leopards chini ya Kocha kijana Antony ‘Modo’ Kimani wameimarika sana.

Hii ni kutokana na utathmini wake baada ya dakika 90 za Mashemeji Derby iliyopigwa juzi Jumapili uwanjani Nyayo na timu yake Gor ikafanikiwa kuponyoka na ushindi mwembamba wa bao 1-0.

Matokeo hayo yalimwezesha Polack kuhakikisha kasajili ushindi wa asilimia 100% kwenye mechi zote za Mashemeji Derby alizoweza kusimamia zikiwa ni mbili sasa.

Lakini tofauti na Mashemeji, Derby yake ya kwanza Novemba mwaka jana, vijana wake waliwalima Ingwe mabao 4-1, safari hii mambo yalikuwa tofauti kabisa.

Mechi ilikuwa ngumu sana na hata bao la Gor lilikuwa la kuangukia tu likitokana na uzembe wa mabeki kushindwa kudhibiti mpitra wa kona na kumruhusu wing’a Boniface Omondi kuusukuma wavuni mpira ulipomwangukia.

Ingwe nao walipata fursa zao lakini wakashindwa kuzitumia, kubwa zaidi ikiwa kunako dakika ya 65, straika Elvis Rupia alimmwaga kipa wa Gor Boniface Olouch kulia na kisha kuusukuma mpira kushoto lakini ukaishia kulikosa lango kwa nchi kadhaa.

Kiwango cha mchezo kilikuwa cha kasi ya juu na timu zote zilionyesha ubora wa kutandaza mpira hasa Ingwe.

Kutokana na alichokiona, Polack hakuna na mengi ila kutii kuwa hakika Ingwe wameanza kushika nare na kama wakiendelea hivyo basi watasumbua.

“Mwanzo nafurahia ushindi wetu wa alama tatu hizo muhimu ukizingatia hii ilikuwa derby. Pia ningependa kuwapongeza AFC kwa mchezo waliotuletea, walikuwa juu sana, huwezi ukalinganisha mchezo waliounyesha juzi na tulipochuana nao hapo awali (Novemba 2019). Anachokifanya pale kocha wao ni kikubwa na ni vizuri kuwapongeza kwa juhudi zao,” Pollack akasema.

Kwa upande wake Modo, hana tatizo na kipigo hicho japo alitamani sana kumalizana na swara la kutowafunga Gor kwa miaka minne sasa. Ingawaje straika wake tegemeo Rupia alipoteza nafasi murwa ya kusawazisha, Modo anasema hana lawama na yeyote.

“Ndio hali ya mpira mzee kuna wakati mnacheza vizuri mkakosa matokeo ya kuridhisha, kuna wakati macheza vibaya mkapata matokeo mazuri. Leo vijana wangu wamecheza vizuri na ningelipenda waendelee hivyo sina lawama na yeyote waliniridhisha licha ya kipigo,” Kimani alituambia.