Kiwango cha Taifa Stars chazua gumzo

Muktasari:

Taifa Stars itajiandaa tena kukutana na Tunisia Novemba 13 katika mchezo wa kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2021.

Dar es Salaam. Juzi, Taifa Stars ilipoteza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Burundi kwa bao 1-0 jijini Dar es Salaam, lakini jana baadhi ya makocha nchini na wachezaji wastaafu walitofautiana kimtazamo juu ya mchezo huo.

Licha ya kutawala mchezo kwa kmuda mwingi ikiwa na asilimia 52 kwa ujumla, Taifa Stars ilishindwa kumaliza vizuri dakika 15 za mwisho.

Kupoteza kwa mchezo huo kumeibua maneno mengi kwa mashabiki wa soka, ambao walikuwa na mtazamo tofauti, wengine wakienda mbali zaidi kwa kupata mashaka na upangaji wa kikosi.

Katika mchezo huo, Taifa Stars ilitengeneza nafasi zaidi ya nne za kufunga, ambazo walikutana nazo Saimon Msuva, Shomary Kapombe na Mbwana Samatta mara mbili lakini hazikuwa mabao.

Mashuti 11 waliyopiga Taifa Stars, ni moja tu ambalo lililenga lango, jambo ambalo halikuleta picha nzuri katika umakini wa washambuliaji wanapofika langoni. Suala la uwezo binafsi nalo lilionekana kwa baadhi ya wachezaji kuonekana kutaka kufanya makubwa katika maeneo ambayo wangeweza kugongeana na kupata faida.

Udhaifu wa mwamuzi, Martine Saanya ulikuwa sehemu ya mchezo huo, wakati licha ya kuwanyima Burundi penalti kwa rafu ya Bakari Mwamnyeto, aloionekana kupishana kauli tangu Samatta alipolalamika kunyimwa penalti kwa kuangushwa kwenye eneo la hatari.

Tukio jingine la Saanya lililotoa picha tofauti ni lile la kumsukuma nahodha huyo wa Stars anayecheza nchini Uturuki, wakati akitaka kumwelewesha jambo.

Kadi nyekundu ya Mkude ilitoa nafasi kwa Burundi kuwa na uwanja mpana wa kucheza katika eneo la kiungo na kufanikiwa kupata bao.

Makocha na wachezaji wa zamani wa Stars walikuwa na mawazo tofauti katika mchezo huo, huku wengi wakionekana kulia na eneo la ushambuliaji.

Kocha wa zamani wa Simba, Abdallah Kibaden alisema Stars ilikuwa vizuri kuanzia nyuma hadi eneo la kiungo, lakini upungufu ulikuwa katika safu ya ushambuliaji. “Kila mmoja alitaka kuonyesha uwezo wake binafsi, jambo ambalo liliwafanya kushindwa kutumia nafasi ambazo tulipata,” alisema Kibaden.

Kocha wa KMC, Habibu Kondo alisema kwa ambavyo ameiangalia Taifa Stars, amegundua kuna baadhi ya wachezaji hawakuwa katika hali nzuri kupata nafasi ya kucheza.

Kondo alisema kutokuwa vizuri kwa wachezaji hao ndiyo lililosababisha kutengeneza nafasi za kufunga na ikashindikana kufanya hivyo.

“Kama tungetumia nafasi za kufunga ambazo hazikuwa chini ya tatu Burundi wangeshuka morali, lakini tulishindwa na mwisho wenzetu wakapata nafasi moja wakatumia,” alisema Kondo.

“Kutokana na kiwango cha chini kilichoonyeshwa na Taifa Stars tunatakiwa kuita wachezaji waliokuwa na viwango vizuri kwenye mechi inayofuata dhidi ya Tunisia, ndiyo silaha pekee.”

Kocha wa Mwadui FC, Khalid Adam alisema timu ilikuwa inakosa muunganiko, kuna wakati ilikuwa inacheza vizuri kutoka nyuma.

“Kutokana na tulivyocheza mechi hiyo kushinda labda mchezaji kama Samatta au mwingine angeonyesha uwezo binafsi ili kufunga, lakini kitimu hatukuwa bora,” alisema Adam.

Mchezaji wa zamani wa Taifa Stars, Mussa Mgosi alisema wakati Burundi walipokuwa wanapoteza mara kwa mara dhidi ya Taifa Stars, kwao ilikuwa kama somo.

“Ukiwaangalia Burundi waliocheza na Taifa Stars wamebadilika na kuimarika katika maeneo mengi tofauti na tulivyowahi kucheza katika awamu zote zilizopita,” alisema.