Kisa Nchimbi, Fei Toto Timbwili laibuka Yanga

Friday January 24 2020

Kisa Nchimbi, Fei Toto Timbwili laibuka Yanga-winga mpya wa Yanga- Mghana Bernard Morrison-klabu ya Smouha ya Ligi Kuu ya Misri-

 

By Mwandishi wetu

WAKATI winga mpya wa Yanga, Mghana Bernard Morrison akirejesha shangwe huko Jangwani, kuna timbwili jipya limeanza kuibuka taratibu.

Jana kikosi cha Yanga kilirejea jijini Dar es Salaam kikitokea Singida kumenyana na wenyeji wao, Singida United na kuibuka na ushindi wa mabao 3-1, lakini kuna mastaa wake wawili wakatibua hali ya hewa.

Ishu iliyopo kwa sasa ndani ya klabu hiyo ni kuwapo kwa dili la straika wao mpya Ditram Nchimbi na kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambao wametakiwa kwenda kufanya majaribio nje ya nchi.

Habari za kuaminika zinasema kuwa, wachezaji hao wamepata dili la kwenda kufanya majaribio kwenye klabu ya Smouha ya Ligi Kuu ya Misri.

Awali, ilielezwa kuwa Nchimbi na Fei Toto walitakiwa kuondoka kwenda nchini Misri kwa ajili ya kujaribu bahati yao kabla ya mchezo dhidi ya Azam FC na baadhi ya viongozi kuridhia.

Hata hivyo, Kocha Luc Eymael akashtukia kuwapo kwa mchongo huo na kutibua mambo akiwataka mabosi wake kumalizana kwanza na mechi ngumu dhidi ya Azam ndipo mambo mengine yaendelee.

Advertisement

Dili hilo lilitibuka baada ya Eymael kuwasaka wachezaji hao kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo ndipo akaelezwa kwamba, walikuwa wakijiandaa kwenda nje ya nchi kufanya majaribio.

“Wakati kikosi kikiwa mazoezini kocha aliwauliza walipo hawa wachezaji ndipo, akapewa taarifa kuwa wako katika mchakato wa kutafutiwa vibali kwenda Misri kwa majaribio,” kilisema chanzo chetu ndani ya Yanga.

Imeelezwa kuwa, hatua hiyo ilimshutua Eymael na kumfanya kuwa mkali kutokana Fei Toto, ambaye mbali na kuwa amekuwa akihudhuria mazoezini mara kwa mara, lakini alimuhitaji zaidi Nchimbi katika mchezo huo wa Azam.

Hata hivyo, baada ya mazoezi hayo mabosi wa klabu hiyo walifanya kikao kifupi kisha kumshirikisha Eymael, ambaye alitoa uamuzi wa kumruhusu Feisal huku akitaka Nchimbi abaki.

Lakini, wakati Eymael akifanya uamuzi huo ghafla akajikuta akimkosa Nchimbi katika safari ya kuifuata Singida United. Nchimbi hakuonekana wakati wa safari hiyo.

Kigogo mzito matatani

Ndani Yanga Mwanaspoti linafahamu kwamba, mmoja wa vigogo wa klabu hiyo alikuwa akisimamia mchakato huo hatua ambayo imewatibua wenzake.

Mabosi wengine ambao wameshtushwa na mpango wa mwenzao kushiriki kwenye mchakato wa kutaka kuwapeleka katika majaribio wachezaji, wametaka uamuzi wa kocha kuheshimiwa.

Molinga amtibulia Nchimbi zaidi

Wakati Eymael akitoa msimamo wa kutaka Nchimbi kubaki hadi hapo mambo yatakapokuwa sawa kikosini kwake, straika anayekubalika kwa kocha huyo, David Molinga naye akatibua mambo zaidi.

Iko hivi. Katika mchezo dhidi Singida United Molinga alipata maumivu ya mguu na hatua hiyo imemfanya Eymael kumuhitaji Nchimbi zaidi katika kikosi chake.

Kutokana na kuumia kwa Molinga, kwa sasa Yanga itabaki na mshambuliaji mmoja Yipke Garmien hivyo kama Nchimbi ataondoka basi Eymael atakuwa na shughuli pevu.

Nchimbi na Fei Toto inaelezwa wanatakiwa katika majaribio katika klabu ya Smouha ya ligi nchini Misri dili linalosimamiwa na wakala Mnigeria.

Advertisement