Kenya yajipanga kutuliza machungu kwa Tanzania

Tuesday June 25 2019

 

By Fadhili Athumani

Cairo, Misri. Baada ya kuanza vibaya katika mchezo wake wa kwanza, Timu ya taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’ sasa inajinoa vikali, kwa ajili ya kutuliza machungu katika mchezo wake wa pili, dhidi ya majirani zao Tanzania, utakaopigwa Alhamisi, Juni 27.

Kikosi hicho kinachonolewa na Mfaransa Sebastien Migne kilianza mazoezi jana jioni, ikiwa ni siku moja baada ya kutandikwa 2-0 na Algeria, kwa mabao ya Baghdad Bounedjah, aliyefunga kwa mkwaju wa penalti na Riyad Mahrez.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mazoezi, Kocha Migne alisema wamejifunza mengi hasa uzembe waliofanya katika kipindi cha kwanza na kushuhudia wakipigwa mabao ya haraka, huku akisisitiza kuwa, Stars iko tayari kupambana katika mechi zake mbili zilizosalia.

“Nikiri tu kuwa, tulizidiwa katika kila idara hasa kipindi cha kwanza, hii ni kwa sababu ya vijana wangu kukosa uzoefu, hata hivyo niwahakikishie kwamba, tumeshayarekebisha makosa na tuko tayari kwa mapambano,” alisema Migne.

Aidha, kuhusu uwezekano wa Joash Onyango kupona kabla ya mechi ya Tanzania, Migne alisema uwezekano ni mdogo lakini ana uhakika kuwa, beki huyo wa Gor Mahia, atakuwa tayari kwa ajili ya mchezo wa mwisho, dhidi ya Senegal.

 “Joash hayuko tayari kwa ajili ya Tanzania, juhudi za madaktari hazijazaa matunda, kila mtu anatamani apone haraka, lakini tuna matumaini atakuwa tayari kucheza dhidi ya Senegal,” alisema.

Advertisement

Kenya, inayoshiriki Afcon kwa mara ya kwanza baada ya miaka 15, iko kundi C, pamoja na Algeria, Senegal na Tanzania. Msimamo unaonesha kuwa Stars, wako katika nafasi ya tatu, sawa na Tanzania iliyo katika nafasi ya nne, huku kinara wa kundi akiwa ni Algeria, akifuatiwa na Senegal.

Advertisement