Kaze kucheza na muda Yanga SC

Muktasari:

Kaze ataanza kuinoa Yanga mara baada ya kukamilisha vibali vya kufanya kazi nchini.

 

Dar es Salaam. Kocha mpya wa Yanga, Cedric Kaze amebainisha kuwa muda utakuwa mwalimu mzuri japo ataanza na vipindi saba tofauti kuibadili timu yake mpya kabla ya mchezo wa kwanza kuiongoza.

Yanga ilimpokea Kaze juzi usiku kwa ajili ya kuchukua mikoba ya Zlatko Krmpotic, aliyetimuliwa mwezi uliopita kutokana na kile kilichodaiwa timu haina soka la kuvutia.

Na Kaze, ambaye alisaini jana mkataba wa miaka miwili kuwanoa mabingwa hao wa kihistoria, atakuwa na kazi ya ziada kuwafurahisha mashabiki wa timu hiyo iliyokosa ubingwa kwa misimu mitatu mfululizo.

Lakini raia huyo wa Burundi hana wasiwasi na kikosi alichonacho akisisitiza kuwa Yanga inahitaji ubingwa na ndiyo matarajio ya uongozi na mashabiki wa miamba hiyo ya mitaa ya Twiga na Jangwani.

“Nina muda mfupi wa kufanya mazoezi na timu an kuingiza vitu vipya kabla ya mchezo wangu wa kwanza wa Ligi Kuu kama kocha wa Yanga, lakini kuna mambo ya msingi zaidi ya kuanzanayo.

“Tutacheza na Polisi Tanzania mchezo ujao, ambao nitakuwa na muda mfupi na timu, kwangu utakuwa mchezo mgumu zaidi kutokana na ugeni, lakini kila kitu kitakuwa sawa.

Kutokana na muda, nitaanza na nitakuwa na vipindi saba (sessions) vya mazoezi, itakuwa ngumu kubadilika sana dhidi ya Polisi, lakini kuanzia hapo nitakuwa na wakati mzuri,” alisema nyota huyo wa zamani wa Prince Louis Rwagasore FC.

Akizungumizia aina ya kikosi alichonacho, alisema wachezaji wote aliwaona na alihusika katika kutoa ushauri wa kununuliwa kwao (isipokuwa kwa Carlinhos), hivyo anaanmini wanakosa mambo kadhaa ya msingi.

“Karibu wote nilihusika katika kununuliwa kwao na ni vijana ambao wanahitaji tu vitu vichache ikiwamo utimamu wa miili yao kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu na zozote za kimashindano.

“Kama nilivyotangulia kusema, itakuwa ngumu kwa muda mfupi kuona kila kitu dhidi ya Polisi, lakini kadri muda unavyozidi kwenda naamini kutakuwa na mabadiliko ya kuonekana,” alisema kocha huyo bora wa Burundi wa msimu wa 2010/11.

Akizungumzia matarajio yake kwa sasa, kocha huyo wa zamani wa Mukura Victory Sports ya Rwanda, alisema kwa timu kubwa kama Yanga sioku zote matarajio ni ubingwa, hivyo atafanya kila liwekanalo kutimiza hilo.

“Yanga ni timu kubwa, hatuko mbali na Azam, ambayo jana (juzi) iliongeza pointi kufikisha 18, lakini sisi tuna mchezo mmoja mkononi, hivyo naamini tutafanya vizuri msimu huu,” aliongeza.

Yanga itacheza na Polisi Tanzania Oktoba 22, kabla ya kwenda Mwanza kucheza na KMC waliobadili uwanja.

Italazimika kutoka Mwanza kuifuata Biashara United ya Mara kabla ya kucheza na Gwambina katika mchezo unaofuata.

Macho na mashabiki wengi wa soka ni kuona jinsi Yanga itakapoivaa Simba ikiwa chini ya Kaze, ambaye kwake itakuwa nafasi nzuri kucheza mechi nyingine kabla ya kukutana na watani.

Mechi na Simba si miongoni mwa mechi zinazompa presha kocha huyo wa Burundi mwenye miaka 40 kwa sasa.

“Nafahamu kuwa mechi dhidi ya Simba ndiyo mechi kubwa zaidi kwa Tanzania, lakini kwasasa nikisema nafikiria hiyo nitakuwa sisemi ukweli, bado kuna mechi za kucheza na kila mechi kwasasa ni kama fainali kwetu,” aliongeza Kaze.