Kamisheni ya ngumi, Chama cha waamuzi watofautiana

Tuesday March 24 2020

Kamisheni ya ngumi, Chama cha waamuzi watofautiana,Chama cha waamuzi wa ngumi , ngumi za kulipwa ,mwanasport,

 

By Imani Makongoro

Dar es Salaam.Wakati Chama cha waamuzi wa ngumi za kulipwa Tanzania kimerudi kwa kishindo na kutaka kufanya majukumu yake kwenye ngumi, Kamisheni ya ngumi za kulipwa (TPBRC) imetoa muongozo wa namna watakavyoshirikiana na chama hicho kiutendaji.

Tayari Chama cha Waamuzi kimesajiliwa na mpaka sasa kina wanachama 24 huku, Ally Bakari (Champion) akiteuliwa kuwa mwenyekiti wa Chama hicho.

Licha ya usajili huo, TPBRC imesema itafanya kazi na waamuzi watakaokuwa na leseni za TPBRC bila kujali wako kwenye Chama cha waamuzi au la, ili mradi awe na leseni ya Kamisheni wao watamtambua.

Katibu Mkuu wa TPBRC, Yahya Pori ameiambia MCL Digital kuwa watakutana na chama hicho katika masuala ya kujadili maendeleo ya ngumi na suala la kupanga waamuzi watakaochezesha mapambano litabaki TPBRC chini ya kamati yao ya ufundi.

Msimamo huo umepingwa na Mwenyekiti wa Chama cha waamuzi, Ally Bakari (Champion) ambaye amesema, Chama cha waamuzi ndicho kitaipelekea TPBRC orodha ya waamuzi wa ngumi za kulipwa.

"Ndivyo katiba yetu na hata ile ya TPBRC inabainisha na hata ilipoundwa kamati ya ufundi kwa mujibu wa katiba inapaswa kuundwa kutoka ndani ya Chama cha waamuzi, lakini kinachofanyika sasa ni uvunjifu wa utaratibu na katiba," alisema Champion.

Advertisement

Pori amesema watafanya semina kwa chama cha waamuzi na itawaeleza majukumu yao ni yapi kwa mujibu wa katiba na utendaji kati ya Chama cha waamuzi na Kamisheni utakuwa kama ule ambao unatumiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

 

Advertisement