Kagere apendekeza nyota watakaosajili Simba
KINARA wa mabao wa Simba na Ligi Kuu Bara, Meddie Kagere ametaja wachezaji ambao wanatakiwa kwenye kikosi chao mara baada dirisha la usajili litakapofunguliwa.
Kagre amesema si rahisi kutaja moja kwa moja majina ya wachezaji ambao wanatakiwa ila endapo angepewa nafasi ya kupendekeza basi angeshauri wasajili nyota wenye uwezo na kuisaidia timu kufikia malengo.
"Mtazamo wangu Simba tunatakiwa kusajili wachezaji ambao wanatakiwa kuja kutoa mchango wao ili kuziba mapungufu ya msimu huu na kufanya vizuri msimu ujao,"
"Natamani kuona wachezaji ambao watakuja hapa ni wale ambao watafanya kazi na hata tusipokuwepo wa zamani kwenye mechi yoyote ya msimu ujao lisionekane pengo lolote.
"Ukiangalia kikosi chetu msimu huu kina wachezaji wengi bora ambao wengine hawajatumika zaidi na hili limetokana na usajili mzuri tulioufanya msimu huu kwa maana hiyo natamani kuona hilo linafanyika kwenye usajili msimu ujao.
"Binafsi sina wasi wasi, naamini tutakuwa na kikosi mahiri tena msimu ujao ndio maana siwezi kutaja majina ya wachezaji ambao wanatakiwa kusajiliwa hapa bali nimetaja sifa ambazo wanatakiwa kuwa nazo ni wale wenye kupambana, kiu ya mafanikio kuona tunafikia malengo ya timu, kutambua majukumu na mengineyo," amesema Kagere
Kagere msimu uliopita alikuwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara akimaliza na mabao 23 na sasa anaongoza mabao 19 .
Mbali ya Kagere kutaja aina ya wachezaji wanaohitajika Simba, wachezaji ambao hadi sasa wanatajwa kuwaniwa na mabingwa hao watetezi ni beki wa Coastal Union Bakari Mwamnyeto na Mpiana Mozizi (FC Lupopo ya DR Congo).