Hivi viwanja vione tu, ni majina ya watu na mitaa

Muktasari:

Kuanza Nangwanda Sijaona, Mtwara hadi CCM Kirumba, Mwanza Mwanaspoti leo linakupa maana za majina ya viwanja hivi.

MTU anayetisha kwenye viwanja vya soka nchini kwa sasa ni straika Meddie Kagere wa Simba.Unaambiwa jamaa anafunga vile anavyotaka. Wewe mshushe uwanjani tu utaona shughuli yake. Hachagui uwanja, jamaa anatupia tu.

Lakini je, umeshawahi kujiuliza majina ya viwanja hivi maarufu nchini yametokana na nini?

Kuanza Nangwanda Sijaona, Mtwara hadi CCM Kirumba, Mwanza Mwanaspoti leo linakupa maana za majina ya viwanja hivi.

SHEIKH AMRI ABEID -ARUSHA

Unaweza usishangae ukionawengi wanadhani Sheikh Amri Abeid Kaluta ambaye jina lake limebeba uwanua wa Arusha na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume ambaye mwanaye alikuwa Rais wa sita wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, ni ndugu.

Sheikh Kaluta Amri Abeid alizaliwa Ujiji, Kigoma mwaka 1924, Baba yake Kaluta Amri Abeid aliitwa Abeid bin Kaluta.

Kaluta Amri Abeid alikuwa ni mtoto wa pili wa kiume katika familia ya watoto kumi.

Baada ya kumaliza elimu ya awali mwaka 1937 alijiunga na Shule ya Sekondari Tabora. Baada ya masomo yake ya sekondari alikwenda kusomea ukarani wa posta Dar es Salaam 1942 -1943. Kaluta Amri Abeid alikwenda kusoma elimu ya dini Rabwah Pakistani ambako alifaulu vizuri na kutunukiwa shahada ya elimu ya dini.

Sheikh Kaluta Amri Abeid alikuwa na kipaji cha usanii. Kipaji hiki cha usanii kilianza kuonekana alipofika umri wa miaka 13, aliweza kutunga na kuimba mashairi kwa sauti nzuri na pia alidhibiti kanuni za mizani katika ushairi. Aliweza kusoma mashairi ya lugha ya Kiingereza, Kiurdu, Kiarabu na Kiajemi.

JINA LA UWANJA

Tuanze na historia fupi ya Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid unaopatikana Jijini Arusha. Ni uwanja ulioanza kutumika tangu miaka ya 1970 ambapo unakadiriwa kuchukua idadi ya watu takribani 20,000 na kwa sasa unatumika na timu mbalimbali za mkoa huo pamoja na shughuli za kijamii.

Jina la Sheikh Amri Abeid limetokana na kiongozi huyo ambaye alikuwa Waziri wa Kwanza wa Sheria katika serikali ya Tanganyika ya mwaka 1960. Alikuwa ‘Member of the Legislative Council’ (kama Bunge la Tanganyika lilivyokuwa likiitwa wakati huo).

Uwanja huo ulijengwa na Lt. Col. Middleton, mzungu aliyekuwa akijishughulisha na kilimo Jijini Arusha.

Alikuwa mpenda mpira na mara nyingi alikuwa mwamuzi katika michezo iliyokuwa ikichezwa hapo. Alitoa uwanja huo kama zawadi yake kwa watu wa Arusha. Uwanja huo ulikuwa uwanja wa kwanza Tanganyika kuwa na taa za usiku ukiacha ule Uwanja wa Taifa (Uhuru).

Col. Middleton aliendelea kuishi Arusha mpaka miaka ya 1970. Alipofariki, Halmashauri ya Mji wa Arusha ikaamua uwanja huo uitwe Sheikh Amri Abeid kutokana na kiongozi huyo kuwa na uhusiano wa karibu na baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Arusha.

NANGWANDA SIJAONA - MTWARA

Lawi Nang’wanda Sijaona ni mmoja wa wapigania Uhuru wa Tanganyika, akifanya kazi kubwa ya kuasisi vyama vya siasa vya ukombozi, tangu TAA, TANU na hatimaye CCM. Alikuwa kiongozi na mzalendo wa mfano wa aina yake, akifanya mambo mengi makubwa na ya kukumbukwa nchini.

Januari 28 kila mwaka hutimia mwaka mwingine mpya tangu taifa letu likumbwe na msiba mzito wa kumpoteza shujaa wetu, mzalendo wa kupigiwa mfano, mwananchi mwadilifu na mwenye kujali utu, kindakindaki wa Tanzania aliyeipenda nchi yake kwa dhati, mchapakazi na mtumishi asiyechoka, Komredi, Sijaona aliyetutoka Januari 28, 2005.

Lawi Nangwanda Sijaona, aliyezaliwa Novemba 24, 1928, Chiyanga katika eneo la Kijiji cha Mnyambe kilichopo Tarafa ya Chilangala, Wilaya ya Newala mkoani Mtwara na kufariki akiwa na umri wa miaka 77.

Nangwanda alipata elimu ya Msingi Utende kuanzia mwaka 1937 na kumaliza darasa la nne mwaka 1942. Alijiunga na Chuo cha Mtakatifu Joseph Chidya, kilichopo wilayani Masasi mwaka 1943.

Mwaka 1948 alijiunga na Chuo cha Mtakatifu Andrea, Minaki alikopata elimu ya kidato cha tatu hadi cha sita na kuhitimu mwaka 1951.

Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere, nchini Uganda kwa masomo ya juu.

Kutokana na harakati zake, haikuwa ajabu kwa Nangwanda kuanza kazi ya uandishi wa habari mwaka 1952 katika Ofisi ya Sekretari Mkuu, Idara ya Mahusiano kwa Umma na akawa mhariri wa gazeti la kila wiki lililojulikana kama “Habari za Leo”.

Alifanya kazi hiyo kwa miaka miwili hadi mwaka 1954 alipoacha na kisha akaombwa na Halmashauri ya Wilaya ya Newala kuwa mtendaji mkuu wa kwanza katika halmashauri.

Desemba 1961, wakati wa Uhuru wa Tanganyika, Nangwanda aliteuliwa kuwa Waziri Mdogo wa Serikali za Mitaa na Tawala za Majimbo na baadaye alihamishiwa Wizara ya Fedha.

Desemba 1962, aliteuliwa kuwa Waziri wa Mila za Taifa na Uongozi wa Vijana.

Aprili 1964, wakati wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais.

Utendaji wake bora ulimwezesha kuhamishwa katika wizara mbalimbali zikiwamo za Ardhi, Maji na Makazi, Mambo ya Ndani ya Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais na Afya na Ustawi wa Jamii. Mwaka 1972, Wakati wa Madaraka Mikoani, Nangwanda aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ziwa Magharibi na baada ya miezi sita, akahamishiwa Mkoa wa Mwanza.

Mwaka 1976 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na mwaka 1980-1983 alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara. Hivyo uwanja huo umepewa jina lake katika kumuenzi.

NAMFUA - SINGIDA

Jacob Namfua, alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro. Alikuwa ni mchapakazi na miongoni mwa Wakuu wa Mikoa waliokuwa kipenzi cha Baba wa Taifa miaka hiyo. Katika uongozi wake, alipandisha hadhi ya wakulima wa zao la kahawa mkoani Kilimanjaro. Alipendwa na kukubalika sana na wana Kilimanjaro.

Mkuu huyu wa mkoa alifariki kwenye ajali ya gari na huo ndio ukawa mwisho wa maisha yake ya duniani.

Katika kumuenzi, CCM iliamua kuupa uwanja wake wa michezo uliopo Singida jina la kiongozi huyo. Uwanja huo unatambulika kama Uwanja wa Namfua ambao unatumiwa na Singida United kwenye michezo ya Ligi Kuu.

CCM MKWAKWANI - TANGA

Wengi tumezoea kukatisha kwa kuuita ‘Mkwakwani’ hata hivyo, Mwanaspoti liliongea na baadhi ya wazee ambao walisaidia kujua hili na chimbuko la neno hilo ‘Mkwakwani’ kwamba kuna miti aina ya Mkwakwa ambayo ilikuwa ikipatikana sana eneo lililojengwa Uwanja wa Mkwakwani ndio maana ikawa rahisi kuuita uwanja huo jina hilo.

“Wengi tunaujua kwa jina la Mkwakwani lakini awali kabla ya jina hilo ulikuwa ukitambulika kwa jina la Uwanja wa St George, ila kumbukumbu za lini ulibadilishwa jina sina, maana hata mzee niliyemuuliza historia hiyo naye amesahau kutokana na hali yake maana ni mtu mzima kwa sasa,” alisema Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Tanga (TARFA), Beatrice Mgaya wakati akilonga na Mwanaspoti.

Uwanja huo upo Kata ya Central. Kuwepo kwa shule inayoitwa ‘Mkwakwani’ kunasisitiza eneo hilo kuitwa jina hilo. Ni kama ilivyo kwa Mkoa wa Dar es Salaam, kuna eneo linaitwa Mikoroshini ambalo lilitokana na kuwepo kwa mikorosho mingi huko nyuma na hata pale Mnazi Mmoja kunaaminika kulikuwapo na mnazi, kama ilivyo eneo la Mkwajuni.

SAMORA - IRINGA

Samora Moises Machel alizaliwa Septemba 29, 1933 katika kijiji cha Madragoa (kwa sasa Chilembene), mkoa wa Gaza nchini Msumbiji. Alikuwa Kamanda wa Jeshi la Msumbiji, Mwanamapinduzi, mjamaa na mwenye msimamo mkali wa Kimarx na Kilenin aliyeiongoza nchi ya Msumbiji tangu uhuru wake mwaka 1975 hadi kifo chake kilichotokea usiku wa tarehe 19 Oktoba 1986 katika eneo la milima la Mbuzini, mpakani mwa Msumbiji, Swaziland na Afrika Kusini.

Katika harakati za kupigania Uhuru wa Msumbiji kutoka kwa wakoloni wa Kireno, Samora Machel alihudhuria mafunzo ya kijeshi ya kujitolea mjini Dar es Salaam na baadaye alikuwa ni miongoni mwa wapiganaji wa chama cha Frelimo waliopelekwa nchini Algeria kwa ajili ya mafunzo zaidi.

Aliporejea Tanzania kutoka Algeria, Samora Machel aliteuliwa kuongoza kambi ya mafunzo ya wapigania uhuru wa Frelimo iliyokuwa Kongwa mkoani Dodoma.

Baada ya Frelimo kuanzisha vita vya kudai Uhuru wa Msumbiji Septemba 25, 1964, Samora Machel alitokea kuwa kamanda mahiri na muhimu sana katika mapambano hayo ambaye jina lake lilivuma kwa kasi mno miongoni mwa makamanda na wapigania uhuru wa Frelimo kutokana na umahiri wake katika medani.

Na kutokana na umahiri huo, alipanda vyeo kwa haraka ndani ya jeshi la wapigania uhuru wa msituni lililokuwa likijulikana kama FPLM hadi kufikia cheo cha Kamanda wa Jeshi baada ya Kamanda wa Kwanza wa Jeshi hilo, Filipe Samuel Magaia, kufariki mwaka 1966. Na katika uchaguzi wa mwaka 1970, Samora Machel alichaguliwa kuwa Rais wa Frelimo.

Kamanda mpya wa Jeshi la Kireno la Msumbiji, Jenerali Kaulza de Arriaga, alitamba kuwa angewasambaratisha na kuwaangamiza kabisa wapiganaji wa Frelimo kwa muda wa miezi michache tu lakini hakufua dafu licha ya kuanzisha mashambulizi makali katika mpango wake wa Operation Gordian Knot mwaka 1970 akielekeza mashambulizi zaidi katika ngome za Frelimo zilizokuwa Cabo Delgado kaskazini ya mbali ya Msumbiji.

Frelimo chini ya Samora Machel ilijibu mapigo na kuhimili vishindo hivyo ambapo ilianza mashambulizi kutoka kila upande na kuelekeza nguvu upande wa magharibi mwa nchi katika mkoa wa Tete. Mpaka kufikia mwaka 1974, Wareno walikuwa hoi bin taaban katika uwanja wa mapambano.

Baada ya kupigwa vya kutosha, Wareno walikubali kutia saini makubaliano tarehe 7 Septemba, 1974 mjini Lusaka kwa ajili ya kukipa mamlaka kamili chama cha Frelimo na tarehe rasmi ya Uhuru wa Msumbiji ikapangwa iwe Juni 25, 1975.

Serikali ya mpito iliundwa ikiwa na Baraza la Mawaziri lililojumuisha Frelimo na Wareno ikiongozwa na Waziri Mkuu Joachim Chissano.

Samora Machel aliendelea kuongoza akiwa Tanzania hadi aliporejea nyumbani Msumbiji kishujaa katika safari iliyoitwa “Kutoka Ruvuma Mpaka Maputo”.

Siku ya tarehe 19 Oktoba, 1986, Rais Samora Machel alikwenda kuhudhuria mkutano mjini Mbala, Zambia, ulioitishwa kumshinikiza Dikteta Mobutu Sese Seko wa Zaire juu ya uungaji wake mkono kwa chama cha upinzani cha Angola cha Unita.

Mkakati wa nchi zilizokuwa mstari wa mbele ulikuwa ni kupingana na Mobutu Sese Seko na Kamuzu Banda katika nia ya kumaliza kabisa uungaji wao mkono kwa Unita na Renamo, vyama au makundi ambayo nchi hizo ziliyaona kama wasaidizi au vibaraka wa Afrika Kusini.

Japokuwa mamlaka za Zambia zilikuwa zimemwalika Samora Machel kukaa mjini Mbala usiku mzima, yeye alisisitiza kurejea Maputo usiku uleule kwa kuwa asubuhi yake, alikuwa amepanga kuwa na kikao chenye lengo la kufanya mabadiliko katika uongozi jeshini. Kutokana na umuhimu wa kikao hicho kilichokuwa kimepangwa kifanyike asubuhi yake, Samora Machel alikiuka hata maelekezo ya Wizara ya Usalama kwamba Rais hakupaswa kusafiri usiku. Na kweli Samora Machel aliondoka usiku wa tarehe 19 Oktoba, 1986 kwa ndege kurejea Maputo, lakini kwa bahati mbaya hakuweza kuiona tena Maputo kama alivyokuwa amepanga.

Ndege yake ilianguka eneo la milima la Mbuzini mpakani mwa Msumbiji, Swaziland na Afrika Kusini, tena upande wa ndani ya Afrika Kusini; yeye Kamanda Samora Machel na watu wengine 33 walipoteza maisha huku watu 9 waliokuwa wamekaa viti vya nyuma ya ndege wakinusurika.

Samora aliishi sehemu mbalimbali hapa nchini, ikiwamo Mkoa wa Iringa, ambapo katika harakati za kupigania Uhuru nchi yake, alikuwa akifanya kampeni katika Uwanja wa Agakhan (Samora kwa sasa) eneo la Frelimo jina lililobeba chama chake.

KAITABA - BUKOBA

Uwanja wa Kaitaba upo katika Mkoa wa Kagera kando ya Ziwa Victoria ni mali ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Ulijengwa mwaka 1976 unakadiriwa kuchukua watazamaji 25,000.

Jina la uwanja huo limetokana na jina la Chifu Omukama Kaitaba aliyetawala kuanzia mwaka 1860 hadi 1888, lakini kabla ya hapo alikuwa Chifu Kitekere ambaye ni mzazi wa baba wa Kaitaba aliyetawala mwaka 1820 hadi 1860. Baada ya Chifu Kaitaba alikuja Chifu Mukotani mwaka 1888 hadi 1895. Hivyo jina la uwanja huo ni moja ya njia ya kumkumbuka Chifu Kaitaba.

VINGINE

Kuna viwanja vingine ambavyo vimebeba majina ya viongozi kama kile cha Shinyanga, Kambarage ambao n kumbukumbu la jina la Baba wa Taifa Julius Kambarage Nyerere. Uwanja wa Sokoine kule Mbeya awali ulikua ukitambulika kwa jina la Uwanja wa Mapinduzi, ukabadilishwa jina kwa heshima ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Moringe Sokoine. Karume wa Dar es Salaam (Abeid Amani Karume), Uwanja wa Mandela (Nelson Mandela) na Ali Hassan Mwinyi (Tabora),

Baada ya kuangalia viwanja ambavyo vimebeba majina ya viongozi wetu pamoja na mitaa, sasa tunageukia viwanja vilivyobeba matukio makubwa ya kitaifa ambayo bado matukio hayo yanatumika mpaka sasa.

UWANJA WA UHURU

Hapo awali ulikuwa ukitambulika kama Uwanja wa Taifa, lakini baada ya Serikali kujenga uwanja mwingine mpya na mkubwa wenye uwezo wa kuchukua watazamaji waliokaa 60,000 ukabadilishwa jina na kuitwa Uwanja wa Uhuru mwaka 2007 wakati uwanja mpya ulipofunguliwa rasmi, uwanja huu ulijengwa mwaka 1961 kwa madhumuni ya sherehe za Uhuru wa Tanganyika. Ndio maana sherehe nyingi za siku hiyo hufanyika uwanjani hapo.

Wakati unajengwa ulikuwa na uwezo wa kuchukua watazamaji 10,000 na ulipofanyiwa ukarabati wa kwanza ulioongeza idadi ya watu na kufikia 15,000 na sasa unakadiriwa kuchukua watazamaji 30,000. Uwanja wa Uhuru ulijengwa mwaka 1961 kwa madhumuni ya sherehe za Uhuru wa Tanganyika.

UWANJA WA MAJIMAJI

Uwanja wa Majimaji upo katikati ya Mji wa Songea Mkoa wa Ruvuma, una uwezo wa kuchukua watazamaji 30,000. Ulijengwa mwaka 1979.

Vita ya Maji Maji vilikuwa ni upingaji mkali wa Waafrika dhidi ya utawala wa kikoloni wa Ujerumani katika koloni la Afrika Mashariki ya Kijerumani.

Vita hivyo vilishirikisha baadhi ya makabila ya kusini mwa Tanzania ya leo dhidi ya sera ya Kijerumani iliyoundwa kwa nguvu kuwalazimisha watu wa Tanganyika kulima zao la pamba. Vita hivyo vilidumu kuanzia mwaka 1905 hadi 1907.

Kinjeketile Ngwale ndiye aliyeongoza vita hivi akiwaaminisha wenzake kuwa risasi zingegeuka kuwa maji katika mapambano yao ya kujaribu kuwang’oa wakoloni. Uwanja wa Majimaji umetumika kama kumbukumbu ya tukio hilo.