HISIA ZANGU : Mkwassa angewaachia timu yao, akasepa zake

Tuesday January 21 2020

Mkwassa angewaachia timu yao, akasepa zake-Kocha Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ -Kocha Mkuu Mzungu, Luc Eymael -Azam vs Yanga-MwanaspotiSoka-MwanaspotiGazeti-

 

By Edo Kumwembe

NIKASIKIA minong’ono kutoka kwa watu wa Yanga. Kwamba Kocha Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ huenda anamuhujumu Kocha Mkuu Mzungu, Luc Eymael pale Jangwani. Kipigo cha Azam kimemchanganya kila mtu pale Yanga.

Walichapwa 3-0 na Kagera Sugara na sasa wamechapwa 1-0 na Azam. Meli inaonekana kuzama. Kabla ya hapo mambo kama vile yalikuwa yanakwenda sawa baada ya Mkwasa kuchukua nafasi ya Mcongo, Mwinyi Zahera.

Lakini ghafla kila kitu kinakwenda kombo. Mkwasa yupo katika benchi. Majuzi mashabiki wamepitiwa na vipaza sauti vya redio mbao na nyingine wameanza kulalamika kwamba huenda staa huyu wa zamani wa Yanga anawahujumu ili aonekana alikuwa kocha mwafaka kuliko Luc.

Mkwasa anaweza kweli kuihujumu Yanga yake? Mtu ambaye alikuwa kiungo maridadi pale Yanga. Halafu akawa shabiki. Akawa mwanachama. Akawa kocha msaidizi. Na baadaye akawa kocha mkuu. Anawezaje kufanya hivyo?

Mtu ambaye Yanga ikizama huwa wanamuita, anaikoa. Amefanya hivyo majuzi tu na nadhani atarudi kufanya hivyo siku za mbele. Sasa hivi kuna mashabiki na wanachama wanataka kumchafua. Lakini pia hata viongozi nao wamegawanyika kiasi chake.

Kuna viongozi ambao wanataka Mkwasa awe kocha mkuu, na kuna viongozi ambao wanamtaka Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Mexime achukue kiti chake.

Advertisement

Kufikia hali ilipofika nafasi Mkwasa ameruhusu hali hiyo. Kwanza kabisa, Kaka Charles ana asili ya upole lakini wakati mwingine inamponza. Angeamua kufuata miiko ya kazi yake nadhani haya mambo yasingemkuta.

Kocha akishafikia hadhi ya kuwa kocha mkuu hapaswi kurudi chini kuwa kocha msaidizi. Kwa mara ya pili Mkwasa amekuwa kocha msaidizi. Aliwahi kuwa chini ya Mzungu, Hans van de Pluijm, na sasa amekuwa chini ya Mzungu mwingine.

Kwa heshima yake alipaswa kuwa kocha mkuu au kuachana na Yanga. Mkwasa aliwahi kuwa kocha wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars. Leo inakuaje anakuwa kocha msaidizi? Ni tatizo ambalo utaliona Tanzania. Baada ya kuwasili kwa hawa Wazungu, Mkwasa angeweza kuwa mkurugenzi wa ufundi na sio kocha msaidizi.

Wakati mwingine makocha wetu wanajishusha. Wanaonekana wapo kwa ajili ya kutatua matatizo ya muda ya klabu hizi. Hawapewi heshima iliyostahili kwa sababu wanaonekana kama mashabiki zaidi wa klabu hizi kuliko makocha.

Kwa mfano, mara kibao makocha wazawa waliowahi kuchezea klabu hizi wamekuwa wakitumika kuficha matatizo ya uongozi. Viongozi huwa wanatumia kisingizio cha ‘mwenzetu’ katika kuficha matatizo ya timu. Hapa ndio unakuta kocha anakubali kufundisha kwa mazingira magumu tofauti na yale mazingira mazuri ambayo makocha wa kigeni huwa wanawekewa pindi wakiwasili nchini.

Lakini hapo hapo linaingia tatizo jingine. Kama Mkwasa asingepewa ofa ya nafasi yoyote ya juu zaidi ya kocha mkuu basi alipaswa kuondoka zake na benchi lake la ufundi. Yanga ndio ambao walipaswa kuchukua maamuzi haya.

Unapomuondoa kocha unalazimika kumuondoa na watu wake jumla jumla. Kumbakisha katika benchi la ufundi kwa namna yoyote nyingine ndio uleta mambo kama haya. Tuwe na bahati kuwa Mzungu wa Yanga hajasikia kinachosemwa kuhusu Mkwasa. Kama akijua kinachosemwa basi anaweza kuamini kuwa kweli Mkwasa anamuhujumu.

Lakini hapo hapo, kama Yanga wangeshinda ushindi wa kishindo katika mechi mbili mfululizo zilizopita basi ingesemwa kwamba kocha Mzungu hakuna aliyechobadili na bado anaendelea kutumia mbinu za Mkwasa. Waswahili ndicho walivyo.

Wakati mwingine jinamizi hili linatokea hata wakati kocha ameondoka. Kwa mfano, Simba walipotoka sare na Yanga, halafu wakapoteza pambano la fainali Kombe la Mapinduzi dhidi ya Mtibwa kelele zilipigwa kwamba timu ilikuwa inacheza ovyo kwa sababu kocha aliyetimuliwa, Patrick Aussems hakuwepo tena katika benchi.

Kama Simba ingekuwa inashinda bado kuna mashabiki wangeamini anayepelekea timu kushinda ni kocha aliyepita na si kocha wa sasa. Hizi ndio busara za mashabiki wa soka wanaokuja na matokeo yao uwanjani.

Maamuzi ya busara kwa sasa ni Mkwasa kukaa kando na kusubiri nafasi yake nyingine. Itakuja. Simba na Yanga huwa hazina ujanja dhidi ya makocha ambao zamani walikuwa wachezaji wa timu hizo. Haya ndio maisha ya kina Mkwasa, Jamhuri Kihwelo, Fred Felix Minziro na Suleiman Matola. Wenyewe wamekubali maisha haya na hapana shaka hayawasumbui.

Kwa sasa Mkwasa angeyapisha matukio yanayoendelea ambayo hayana umuhimu wala tija tena. Bahati nzuri ataendelea kubakia kuwa shabiki wa Yanga milele na milele. Ndivyo walivyotengenezwa wachezaji wa zamani wa klabu hizi.

Kitu ambacho Yanga wanapaswa kujifunza siku nyingine ni kutokuwa na makocha watatu ndani ya msimu mmoja.

Labda wangeweza kumbakiza Mkwasa mpaka mwishoni mwa msimu akiwa kama kocha mkuu kabla ya kumpa timu Luc mwishoni mwa msimu huu. Labda timu ingeweza kutulia kidogo mpaka mwishoni mwa msimu.

Advertisement