Dili la Mexime, Yanga bado kidogo tu

Friday January 17 2020

Dili la Mexime- Yanga bado kidogo tu -kocha Mkuu wa Kagera Sugar- Meck Mexime -mchakato wa kujiunga na Yanga-Azam FC-Uwanja wa Chuo cha Sheria-

 

By Charity James

ALIYEKUWA kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Meck Mexime amethibitisha kukamilisha mchakato wa kujiunga na Yanga kama kocha msaidizi.
Hata hivyo, amesema kuwa kwa sasa bado yuko na klabu yake na kwamba, baada ya kukamilisha baadhi ya taratibu ataweka hadharani ni wakati gani atajiunga na mwajiri wake mpya.
Mexime, ambaye amepeleka kilio Jangwani kwa kuwafunga bao 3-0 Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, amesema amefanya mazungumzo na mabosi wa Yanga, lakini bado haijawa wazi muda wa kuanza majukumu hayo mapya hadi taratibu zingine zitakapokamilika.
"Kuhusu kutambulishwa leo hapana sio kweli, nipo njiani na timu tunakwenda Kagera na tumeanza safari jana Alhamisi kutoka Dar es Salaam. Mambo yakikamilika nitarejea Dar es Salaam kwa hatua zingine zaidi,” alisema.
Wakati huohuo, Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Fredrick Mwakalebela ameweka wazi kuwa wameshindwa kumtambulisha Mexime leo Ijumaa kama walivyopanga kutokana na kutokamilika baadhi ya taratibu.
"Kwa upande wa Mexime tumemalizana na kilichobaki na uongozi wa Kagera Sugar ambao, bado wana mkataba naye wa miezi sita hivyo mazungumzo baina yetu yakikamilika basi muda wowote atatambulishwa na kuanza kazi Jangwani,” alisema.

Advertisement